Benki ya Dunia imeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 50 duniani za
uchumi wa kipato cha kati, ikiwa ni ya pili baada ya Kenya katika nchi za
Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, baada ya ukuaji wa uchumi unaosukuma pato la
mwananchi kukua (Per capita GNI) mwaka 2020.
Tanzania imeingia kwenye uchumi wa kati
miaka mitano kabla ya lengo la Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, jambo
ambalo ni la kujivunia.
Akizungumza
katika Mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Katibu Mkuu Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan
Abbasi alisema kwa mujibu wa Dira ya
Taifa ya Maendeleo, 2025 katika ukurasa wa pili, kipengele 1.2 “Uchumi
wa kipato cha kati umehusishwa na kuwa na nchi ambayo umaskini unapungua,
uchumi imara unaojengwa na kuimarika kwa uzalishaji viwandani unaimarika na
wananchi wanapata maendeleo”.
Dkt. Abbasi
alisisitiza kuwa uchumi wa kipato cha
kati umegawanyika katika madaraja mawili daraja la chini ambapo ni kuanzia dola
za Kimarekani 1036 hadi 4045 na daraja la juu ni dola 4046 hadi 12,535 na mwaka huu Tanzania
imepanda daraja kuwa uchumi wa kipato cha kati daraja la chini, pamoja na nchi
za Algeria na Benin.
Aidha, Dkt.
Abbasi alifafanua siri 10 zilizoisaidia Tanzania kutajwa kufikia daraja la
uchumi wa kipato cha kati na Benki ya
Dunia hapo Julai 1, 2020 kuwa ni nchi yenye amani na utulivu, na hivyo ni msingi muhimu nyuma ya mafanikio ya nchi ya Tanzania kuingia katika uchumi wa kipato cha kati
kwani bila amani hakuna kufanyakazi, hakuna
kuzalisha na hakuna kuongeza kipato. Na hivyo viongozi, wanahabari na wananchi kwa ujumla wamesisitizwa
kuwekeza akili zao katika kuimarisha amani iliyopo na kukataa chokochoko
zozote zile zinazoweza kuharibu misingi ya maendeleo.
Siri ya pili ni mipango thabiti ya
maendeleo, ambapo Dkt. Abbasi alisema kuwa moja ya kanuni muhimu ya kuendelea ni kuwa na
mipango inayokuwekea malengo makubwa (Olympic targets). Serikali itaendelea
kuweka mipango mbalimbali ya maendeleo ya muda mrefu na mfupi, akitolea mfano
mwaka 2020 Serikali ilianza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025
ambayo moja ya malengo ni kufikia uchumi wa kati.
Kwa mujibu
wa Dkt. Abbasi siri ya tatu ni utekelezaji
usioyumba, katika miaka 59 ya Uhuru na mitano ya Awamu ya Tano Serikali
imejitahidi kusimamia eneo hilo kwa
kuhakikisha mipango inayowekwa inatekelezwa kwa kina (3feet implementation).
Siri
nyingine ni maamuzi magumu, “Moja
ya mafanikio ya Serikali ya Tanzania kwa Awamu zote na sasa tumeimarisha katika
Awamu ya Tano ni wakati fulani Serikali kufanya uamuzi mgumu ambao wakati
fulani ulionekana kuwa ni ndoto lakini baadaye ukaleta mafanikio makubwa kwa
jamii, tumepambana na wala rushwa na wahujumu uchumi, tumewekeza katika
miundombinu mikubwa, tumekataa pia baadhi ya nadharia za kimagharibi kwenye
utendaji wetu na utungaji wetu wa sera za maendeleo” alisema Dkt. Abbasi.
Aidha, Dkt.
Abbasi alitaja siri nyingine kuwa ni azma
ya kujitegemea, nidhamu katika matumizi, kutekeleza miiko ya uongozi, kuwekeza
kwenye miradi inayochechemsha uchumi, maendeleo ya vitu na sekta binafsi yenye tija.
0 comments:
Post a Comment