Nianzie
wapi kumuelezea Mzee wa Uwazi na Ukweli? Hebu nianzie kwenye kitabu chake cha Maisha Binafsi ya Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Benjamin William Mkapa chenye jina la “Maisha Yangu, Dhamira Yangu: Rais wa Tanzania Akumbuka” alichokizindua
hapo Novemba 12, 2019 ambapo Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli alikuwa Mgeni Rasmi, Mzee Mkapa anasimulia kuwa maono yake: ni maisha ya
hali ya juu, amani, utulivu na umoja, utawala bora, jamii iliyoelimika na
uchumi shindani wenye uwezo wa kukua kiendelevu na mgawanyo shirikishi wa
kipato.
Ni
dhahiri kuwa kifo cha Rais Mstaafu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Benjamin William Mkapa kilichotokea hapo jana Julai 24,
2020 ni pigo kwa taifa, Afrika pamoja na dunia kufuatia mchango wake ulioakisi
mabadiliko ya uchumi, mahusiano ya kimataifa na mapinduzi katika sekta za umma
na binafsi.
Kama mjuavyo ni katika uongozi wa Mzee Mkapa ambapo mikakati
mbalimbali ya kimaendeleo ilianzishwa, baadhi ni Dira
ya Taifa 2025, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania
(MKUKUTA), Mpango wa Kurasimisha Biashara na Mali za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) na Mini Tiger Plan 2020.
Aidha,
Rais Mkapa alianzisha Bima ya Taifa,
Mageuzi katika Elimu, na Mradi wa Maji ziwa Victoria, halikadhalika Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini (TASAF), mageuzi haya yalihitaji kiongozi makini mwenye
mapenzi kwa taifa lake lakini aliyeishi na kuamini ndoto zake za kuleta
maendeleo kwa wananchi wake.
Shughuli za maendeleo na ukuaji wa uchumi
Wakati wa uongozi wake Mzee Mkapa aliyekuwa Rais, mwandishi
wa habari na mwanadiplomasia nguli
aliweza kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kisiasa, na kijamii,
ikiwa ni pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa kupitiliza malengo na
kukusanya kiasi cha sh. bilioni 133 kwa mwezi kati ya Julai na Novemba 2004,
kulingana na takwimu za Serikali, kudhibiti mfumuko wa bei kutoka asilimia 30
hadi chini ya 5.5 na kukua kwa uchumi
kwa asilimia sita.
Duru za siasa za ndani na kimataifa
Itakumbukwa kuwa Mkapa ni Rais wa kwanza nchini Tanzania
kuingia madarakani kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika zama za siasa
za vyama vingi mnamo mwaka 1995.
Akiwa amebakiza takriban miezi kumi tu kumaliza kipindi chake
cha kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Benjamin William Mkapa
aliwahi kukemea tabia ya watu wanaotishia kuvunja amani katika nchi
aliyoipokea kutoka kwa wenzake
waliomtangulia ikiwa na amani na utulivu.
Alionesha wazi kuwa mfumo wa siasa wa vyama vingi
haukuanzishwa nchini ili kudhoofisha utaifa, umoja na mshikamano kwa taifa.
“Hatukuanzisha mfumo wa siasa wa vyama vingi ili watu wetu
wachukiane, watishane kwa kunoa mapanga waumizane, wauane au waharibiane mali
zao,” alisema Mzee Mkapa.
Hakuna shaka kwamba utawala wa Rais Mkapa
ulijaa mambo mengi mazuri ambayo hayataweza kufutika katika kizazi hiki na mara
kadhaa alihubiri juu ya amani, na
kuheshimu haki za binadamu ikiwemo haki
ya kuishi.
Katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu, ni vyema tukakumbuka aliyowahi
kusema Rais Mkapa mwaka 2005 wakati
ambapo nchi ilifanya Uchaguzi Mkuu.
“Tuje tuwaogope sana wanaohubiri chuki kwa
kisingizio cha ushindani wa kisiasa. Ushindani tunaotaka sisi ni wa hoja, wa
fikŕa, wa mikakati na mipango ya maendeleo.
Tunashindanisha ilani za uchaguzi
wa vyama. Ningependa vyama vyetu vyote vya kisiasa viwe na malengo makuu
yanayofanana yaani umoja, amani, upendo, maendeleo na ustawi wa taifa na
wananchi. Tunachotofautisha na tunachoshindania kiwe mipango na mikakati ya
kufikia malengo hayo makuu,” alisema Mzee Mkapa.
Aidha, Mzee Mkapa alikuwa mpatanishi wa mgogoro wa Burundi ambapo alizitaka
pande husika katika nchi hiyo kushikamana na kuheshimu mchakato wa amani na
hatua zilizopigwa za kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo. Pia,
alihusika katika upatanisho wa migogoro
ya nchi za Sudani ya Kusini, Congo
Mashariki, na Kenya.
Katika hali isiyotarajiwa na wengi ni kwa
kiongozi aliyewahi kuwa Rais kukiri wazi juu ya udhaifu wake, ambapo aliyekuwa
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Rwekaza Mukandala
amechambua wasifu wa Mzee Mkapa katika kitabu chake cha Maisha Yangu, Dhamira Yangu: Rais
wa Tanzania Akumbuka, anaandika, “Mheshimiwa Mkapa anakiri kuwa, kabla
hajawa Rais, hakujua kuwa kazi moja wapo ya Rais ni kutoa pole. Mojawapo ya
mapungufu yangu ni kwamba si mwepesi wa kuonyesha hisia zangu. Mrithi wangu
Rais Kikwete ni mzuri sana katika hili. “Anasema Mheshimiwa Mkapa, ameandika
Profesa Mkandala.
Mwisho kabisa Mzee Mkapa, anamalizia kwa
kusema; Nitamuachia Mungu wangu na nyinyi kuamua ni tofauti gani nimeifanya
humu duniani.
Kama taifa yapo mengi ya kujifunza kutoka
kwa Mzee Mkapa na kumuenzi ni pamoja na kuthamini mchango uliosaidia kuleta
maendeleo ya kijamii, kiasiasa na kiuchumi.
0 comments:
Post a Comment