METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, July 2, 2020

DKT MABULA AZINDUA MPANGO WA MATUMIZI YA BIMA YA AFYA ILIYOBORESHWA CHIF KWA MADEREVA NA MAKONDAKTA MWANZA


Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula amezindua mpango wa matumizi ya Bima ya afya iliyoboreshwa CHIF kwa madereva, makondakta wa mkoa wa Mwanza na familia zao kwa gharama nafuu ya shilingi elfu thelathini kwa watu sita kwa kila kaya kwa maana ya baba, mama na watoto wanne itakayowawezesha kuhudumiwa katika zahanati, kituo cha afya, hospitali ya wilaya mpaka mkoani pindi wanapougua.

Akizungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa mpango huo, Katibu wa Mbunge huyo Ndugu Kazungu Safari Idebe amepongeza Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Mhe Dkt John Magufuli kwa kuboresha sekta ya huduma za afya na uanzishwaji wa mpango huo wenye lengo la kusaidia watu masikini waweze kupata huduma za afya kwa gharama nafuu na urahisi huku akiwaasa madereva hao kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo

'.. Mbunge wenu amenituma niwaambie kuwa yupo pamoja nanyi, anatambua changamoto zinazowakabili na ataendelea kushirikiana nanyi katika kuzitafutia ufumbuzi, tembeeni kifua mbele chini ya Serikali yenu hii ya hapa kazi tu si mnaona mambo mazuri na makubwa yanafanyika ..' Alisema

Aidha Katibu Kazungu amewahakikishia ushirikiano wa mbunge wao Dkt Angeline Mabula katika kuendelea kuwatumikia sanjari na kutoa fedha taslimu kwaajili ya kuwakatia bima hiyo kaya 10 kwa maana ya idadi ya watu 60 wasioweza kuchangia huduma hiyo kwa makundi ya wajane, wagane, yatima, wazee na watu wengine wasiojiweza.

Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha madereva na makondakta mkoani Mwanza MWARREDA Ndugu Mjarifu Manyasi mbali na kumshukuru mbunge huyo,  Ameongeza kuwa zoezi la uandikishaji wa bima ya afya iliyoboreshwa kwa wanachama wake ni zao la ushauri uliotolewa na mbunge huyo mapema mwaka huu alipotembelea ofisi yao na kukuta changamoto  wanayoipata wanachama hao pindi wanapopata ajali katika maeneo ya kazi sambamba na kuongeza kuwa zoezi hilo litaendeshwa kwa siku kumi kuanzia Julai 01, hadi Julai 10, 2020 likitegemea kugusa idadi ya watu 2,000.

Akihitimisha Bi Edina Ruben moja ya wajane walionufaika na msaada wa kulipiwa bima ya afya iliyoboreshwa kutoka kwa Mbunge huyo, Ameshukuru  na kuomba viongozi wengine waige mfano huo kwa kuwakumbuka watu wasiojiweza katika jamii na kutatua changamoto zinazowakabili.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com