Serikali
imeziunganisha benki zake mbili za
biashara, Benki ya Posta Tanzania (TPB Bank Plc) na Benki ya Uwekezaji Tanzania
(TIB Corporate Limited) ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za
uendeshaji.
Akizungumza
leo (Jumatatu Juni 1, 2020) jijini Dodoma,
Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka alisema kuwa Serikali imeendelea kuchukua
hatua mbalimbali zenye lengo la kuboresha utendaji wa mashirika na taasisi za
umma ikiwemo kuunganisha taasisi zinazotekeleza majukumu yanayofanana, ili
kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji.
“Kwa
muktadha huu, Serikali imeamua kuunganisha benki zake mbili za biashara, yaani
Benki ya TPB na Benki ya TIB Corporate kuanzia tarehe 01 Juni 2020. Kwa hatua
ya awali, Benki ya TPB itachukua mali na madeni ya Benki ya TIB Corporate na
muunganiko huu utafanya benki kuwa na mali takribani trilioni moja”, alisema
Mbuttuka
Alifafanua
Mbuttuka amesema Serikali imechukua uamuzi huu kwa lengo la kuboresha utendaji
wa benki inazozimiliki ili kuwa na benki moja ya biashara ambayo ni imara.
Aidha, muungano huu unalenga kuleta mageuzi makubwa ya kiutendajii, kimfumo,
kimuundo, na kitaswira ili benki hii iweze kuhimili ushindani wa kibiashara
kwenye sekta ya fedha.
“Muunganiko huo hautakuwa na athari katika
huduma za kibenki, wala hakuna mfanyakazi atakayepoteza ajira. Aidha, Serikali inapenda kuuhakikishia umma kuwa
itaendelea kuhakikisha utendaji wa benki zake unaimarika na maslahi ya wenye
amana na wateja wote yanalindwa kwa mujibu wa sheria, kanuni, na taratibu za
usimamizi wa benki na taasisi za fedha”, alioneza Mbuttuka.
Kwa mujibu
wa Msajili wa Hazina, wateja wote wa Benki ya TPB na Benki ya TIB Corporate
wataendelea kuhudumiwa kwenye matawi yao ya sasa hadi hapo watakapotaarifiwa
vinginevyo.
0 comments:
Post a Comment