METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, June 9, 2020

RAIS MAGUFULI AWEKA REKODI MPYA NAKALE


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ameweka rekodi mpya isiyofutika kwa Wanakijiji cha Nakale ambapo tangu wapate Uhuru hawajawahi kuwa na umeme lakini leo hii umeme umewaka kwa mara ya kwanza.

Wanakijiji hao wa Nakale kilichopo kata ya Mihambwe wamefurahi kupata umeme wa REA kwani hawakutarajia kabisa na ni mshangao kwao.

"Tangu tupate Uhuru nilikuwa sitegemei kabisa Kijiji chetu cha Nakale kupata umeme, Mimi kabisa leo hii nyumba yangu ina umeme nina furaha ya ajabu. Sasa hivi nitapata vinywaji baridi, nikitaka kufungua biashara ya kuchomelea vyuma naweza, uwekezaji wowote unaweza kufanyika kwa sababu tuna umeme wa uhakika sasa. Sina zawadi ya kumpa Rais Magufuli ambaye ni Mchapa kazi na kiongozi anayejali Wanyonge zaidi ya dua njema kwake na kumuunga mkono kwenye ujenzi wa Taifa letu." Alisema Mzee Dadi Samri Amri mnufaika wa umeme wa REA kijijini hapo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nakale naye hakusita kutoa shukrani kwa Rais Magufuli na kuwasihi Wananchi kuchangamkia fursa ya kuwa na umeme.

"Umeme huu tumeupokea kwa mikono miwili na tunamshukuru Rais Magufuli kwa umeme wa REA. Nawasihi Wananchi wangu wajiunge na umeme huu wenye gharama nafuu." Alisema Ally Chande Namkaka, Mwenyekiti Serikali ya Kijiji cha Nakale.

Hayo yamejitokeza wakati wa ziara ya kikazi aliyoifanya Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu kijijini hapo ambapo amewasihi wasambazaji umeme wa REA kuongeza kasi ya uwashaji wa umeme kwenye vijiji vilivyosalia.

"Wananchi wameupokea umeme wa REA kwa furaha na pongezi tele kwa Rais Magufuli. Nawaelekeza wasambazaji umeme wa REA awamu ya tatu kipindi cha pili ambao utekelezaji wake umekwisha anza, waongeze kasi ya uwashaji umeme kwenye vijiji vilivyosalia kama ilivyo  kwenye ratiba." Alisisitiza Gavana Shilatu.

Kwenye ziara hiyo ya kikazi, Gavana Shilatu aliambatana na Mwenyekiti Serikali Kijiji Nakale, Mtendaji Kijiji Nakale Pamoja na Wajumbe Serikali Halmashauri ya Kijiji Nakale kushuhudia utekelezaji uwashwaji wa umeme wa REA kijijini Nakale.

Utekelezaji mradi wa REA awamu ya tatu kipindi cha pili ambao umeanza mwezi huu wa sita ambapo kila Kijiji kitakuwa na wanufaika 53 wa umeme huo kwa kuanzia ambapo vijiji vyote vilivyosalia vitawashwa umeme ndani ya Tarafa ya Mihambwe.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com