Viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa, viongozi wa dini, viongozi wa chama cha mapinduzi na watumishi wa kata ya kawekamo wilayani Ilemela wamepongeza na kushukuru maendeleo yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa diwani wa kata hiyo Mhe Japhes Rwehumbiza.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti ndani ya kikao cha kamati ya maendeleo ya kata (WDC) kwaajili ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kumuaga diwani huyo, kwa niaba ya wenyeviti wenzake, Mwenyekiti wa mtaa wa Kawekamo ‘B’ Bi Moshi Malima amesema kuwa kilichofanyika kwa kipindi cha miaka mitano ya Uongozi wa diwani Rwehumbiza na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Mhe Dkt John Magufuli mbunge akiwa Mhe Dkt Angeline Mabula ni miujiza na haikuwahi kutokea ndani ya kata yao kwani miradi mbalimbali ya maendeleo imetekelezwa kwa ubora na haraka ikiwemo ujenzi wa daraja la nyakurunduma, upimaji shirikishi, upatikanaji wa maeneo kwaajili ya ujenzi wa kituo cha afya, jengo la polisi na ofisi ya kata, ujenzi wa madarasa ya sekondari na msingi, ujenzi wa matundu ya vyoo, ujenzi wa barabara ya mjini kwenda uwanja wa ndege, ukarabati wa barabara za mitaa na utoaji wa mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu
‘.. Kwakweli miaka mitano ya uongozi wako na mwenzako Dkt Angeline Mabula chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli haijawaki kutokea, Tunajivunia maendeleo tulioyapata chini yenu ..’ Alisema
Kwa upande wake afisa maendeleo kata ya Kawekamo, Ndugu Teresphory Barusha Kwa niaba ya watumishi wengine, Akamshukuru diwani Japhes Rwehumbiza kwa mchango wake wa kuhakikisha watumishi hao wanakuwa na nidhamu ya kazi katika kuwahudumia wananchi, ameshirikiana nao katika kutatua kero na changamoto za wananchi na watumishi kwa ujumla, Huku Mwalimu Khalid Kazinja wa shule ya Sekondari Kilimani akipongeza jitihada za diwani huyo katika kuhakikisha ujenzi wa madarasa matatu ya shule yake unakamilika sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya maji na umeme jambo lilikuwa kero kwa muda mrefu.
Viongozi wa dini walioalikwa katika kikao hicho akiwemo Imamu wa msikiti wa Pasiansi Mzee Mahmoud akapata wasaa wa kumpongeza na kumshukuru diwani huyo kwa ushirikiano alioutoa katika kipindi cha uongozi wake sanjari na jitihada zake katika kuwaunganisha bila kujali itikadi zao za kidini pamoja na kutatua kero zilizokuwa zikiwakabili ikiwemo upatikanaji wa hati miliki katika kiwanja cha msikiti wao, Huku mchungaji Godfrey Jacob wa kanisa la KKKT Kiloleli akampongeza kwa umakini, usikivu na kutenda haki katika kuhakikisha wananchi wake wanapata maendeleo.
Nae katibu wa CCM kata ya Kawekamo Bi Neema Mapesa akatumia fursa hiyo kumpongeza diwani huyo kwa uongozi wake uliofanikisha utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015/2020 kiasi cha kufanya wepesi katika kunadi wagombea watakaoteuliwa na chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2020.
Akihitimisha Mhe Japhes Rwehumbiza mbali na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo, akawashukuru viongozi hao kwa namna walivyoshirikiana katika kipindi cha uongozi wake huku akiwaomba kuendelea kuwa pamoja na kumuombea kwa Mungu ili kata hiyo izidi kusonga mbele.
0 comments:
Post a Comment