Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Rukwa, Swagile Msananga amewatoa hofu wananchi wa Mkoa huo kuwa, hawatakuwa na haja ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za sekta ya ardhi katika ofisi za kanda zilizopo mkoa wa Mbeya baada ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi nchini, kuanzisha ofisi za ardhi za mikoa zikiwa na lengo la kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.
Msananga amesema kuwa lengo la wizara kuwapunguzia wananchi gharama za usafiri kufuata huduma ambazo hivi sasa zinapatika katika ofisi hizo zilizopo katika jengo la Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa, huku akifafanua huduma zinazotolewa kuwa ni pamoja na masuala ya mipango miji, uthamini, upimaji na ramani, usajili wa hati na kusaini hati.
“Sasa Wananchi badala ya kufunga safari kwenda mbeya kupata huduma, hizo safari sasa hazitakuwepo tena, huduma zote zitapatikana hapahapa, na halmashauri zote ambazo tunazihudumia pia zitaleta nyaraka zao hapa kwaajili ya kupata idhini na hati zitasainiwa hapahapa, na nyaraka zote zitasajiliwa hapa.”
“Kwahiyo napenda niwape wananchi taarifa kwamba ofisi ya Kamisha wa Ardhi Mkoa wa Rukwa imeshaanza kazi rasmi na tunawakaribisha mpate huduma zote na tunaahidi kwamba tutawapa huduma katika ubora na uadilifu,” Alisema.
Hivi karibuni tarehe 10, Mei 2020 akiwa jijini Dodoma Waziri wa Ardhi Maendeleo ya Makazi Mh. William Lukuvi alisema Wizara hiyo imeanzisha ofisi za ardhi katika kila Mkoa ili kutoa huduma zote zilizokuwa zinatolewa kwenye ofisi za Kanda na Makao Makuu.
0 comments:
Post a Comment