Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Mamlaka ya Maendeleo
ya Biashara Tanzania (TanTrade) inapenda kuwataarifu Taasisi za Umma, Sekta
Binafsi, Jumuiya za Wafanyabiashara na Wananchi wote kwa ujumla kuwa inaendelea
na maandalizi ya Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es
Salaam yanayotarajiwa kuanza tarehe 1 hadi 13 Julai, 2020 katika Uwanja wa
Maonesho wa Mwl. J. K. Nyerere, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.
Lengo la Maonesho haya ni kutoa fursa ya kutafuta masoko ya
mazao na bidhaa za kilimo, viwanda na huduma nchini.
Kauli Mbiu ya Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar
es Salaam (DITF) ni “Uchumi wa Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu” ikilenga
kutambua mchango wa Sekta ya Kilimo na Viwanda katika kuzalisha ajira na
kujenga biashara endelevu.
Uratibu wa Maonesho unazingatia kanuni za Afya kwa lengo la
kuhakikisha kuwa Uwanja wa Maonesho unakuwa salama kwa Waoneshaji na
Watembeleaji kwa kuchukua hatua zote stahiki za kujikinga na maambukizi ya
COVID-19. Ili kuendana na hali halisi na kufikia wigo mkubwa zaidi wa
Wazalishaji na Wanunuzi, Mikutano yote ya ana kwa ana ya Wafanyabiashara (B2B)
itaandaliwa na kuratibiwa kwa njia ya mtandao.
Lengo la Mikutano hii
ni kuimarisha upatikanaji wa masoko endelevu ya bidhaa na huduma. Aidha, ili
kurahisisha utembeleaji wa Maonesho, watembeleaji watapata fursa ya kununua
tiketi kupitia simu za mikononi. Vilevile, Watembeleaji kutoka ndani na nje ya
nchi watapata fursa ya kutembelea Maonesho kupitia mtandao (Live streaming and
virtual exhibition).
Kutakuwa pia Banda Maalumu litakalo tangaza bidhaa za kilimo
yakiwemo mazao ya kimkakati. Wizara ya Viwanda na Biashara inatoa wito kwa
Wafanyabiashara, Wamiliki wa Viwanda vyote nchini, Wakulima, Taasisi za Umma,
Halmashauri za Wilaya na Taasisi Binafsi kushiriki katika Maonesho haya ili
kuongeza wigo wa masoko ya bidhaa za kilimo, viwanda, mifugo, uvuvi na madini
zinazozalishwa nchini na kuhamasisha Wananchi kupenda bidhaa zinazozalishwa
hapa nchini.
0 comments:
Post a Comment