Halmashauri za
jiji la Dar es salaam zimetakiwa kuwa na kiwango kimoja cha tozo za ushuru wa
takataka ili kuondoa matabaka ya ulipaji wa tozo hiyo katika kata mbalimbali
za jiji hilo.
Hayo
yameelezwa mapema jana jijini Dar es salaam na Meneja wa Idara ya Utafiti na
Uchambuzi wa TGNP Mtandao, Happy Maruchu katika Semina za Jinsia na
Maendeleo(GDSS) ambapo waliangazia katika vyanzo vya mapato ikiwemo kodi na
tozo mbalimbali za halmashauri zinavyoweza kuwagusa wananchi hususani wenye
mahitaji maalum.
Meneja huyo alisema
kuwa katika semina hiyo mambo makubwa yaliyoibuka ni kero ya ukusanyaji wa Takataka katika mitaa mbalimbali, na wananchi wengi wamelalamika kuwa zoezi hilo
limekuwa likiendeshwa kiholela kwa ukusanyaji wa fedha na pia kukosa ufanisi
katika uchukuaji wa takataka hizo.
“Wengi
waliopewa dhamana ya ukusanyaji wa takataka wamekuwa wakilazimisha watu kulipa
fedha kwa wakati na ukiangalia wao wenyewe hawachukui taka hizo kwa wakati, na
kusababisha takataka kukaa muda mrefu hali inayofanya wananchi kuwa kwenye
hatari ya kuugua maradhi ya mlipuko” alisema Maruchu.
Aliendelea
kusema kuwa wanasemina pamoja wananchi wote wanajiandaa kujengeana uwezo ili
kuweza kutoa maoni yao kwa mwaka wa fedha unaokuja ili kutoa maoni yao katika
ngazi ya halmashauri kuona kama wanaweza kupata utatuzi wa kero hii kubwa
inayosumbua wananchi wengi kwa sasa.
Mmoja kati
ya wakazi wa Manispaa ya Ubungo Bw. Hans Obote alisema kuwa kero kubwa kwa
upande wake ni kuwa na matabaka katika halmashauri moja na nyingine, Ambapo
kama Ubungo utakuta wanalipa elfu tatu kwa kaya moja na kama nyumba ina
wapangaji wanaweza kulipa mpaka elfu 15 kwa nyumba moja, Na kwa maeneo mengine kama
kinondoni wao wanalipa elfu tano kwa nyumba moja bila kuangalia idadi ya wakazi
wa nyumba husika.
Aidha aliongeza
kuwa kwa huu utaratibu wa kila kaya ilipe na kuna wanafunzi waliopanga kwenye
nyumba hizo na wao unakuta hawapiki wala hawana njia yoyote ya kuzalisha takataka, Cha ajabu mwisho wa mwezi wanatakiwa kulipa sawa na mtu mwingine mwenye
familia kubwa ambaye yeye kila siku anazalisha Takataka.
Aliendelea
kusisitiza kuwa hali hii pia inawakumba wafanyabiashara wengi wadogo ambapo
kila eneo unakuta limewekewa kiwango chake kwa mfano kuna maeneo wanatakiwa
kulipa elfu tano, lakini wengine wanapangiwa kulipa elfu saba mpaka elfu kumi, Na
akipigiwa hesabu kulipa eneo la biashara na mahali anapoishi gharama zake
zinakuwa kubwa sana hali inayowaumiza wafanyabiashara wengi hasa wadogo.
Na mwisho
kabisa alisema kuwa jiji la Dar es salaam linatakiwa kuwa na sheria moja
itakayoweza kufanya kazi katika halmashauri zote kwani hali hii inawaumiza
wananchi wengi hasa wenye vipato vidogo.
Muwezeshaji wa Semina ambaye pia ni Meneja wa Utafiti na Uchambuzi wa TGNP Mtandao, Happy Maruchu akitoa ufafanuzi wa jambo mapema jana katika Semina za Jinsia na Maendeleo GDSS.
Mkazi wa Mabibo jijini Dar es salaam Msafiri Shababi akitoa maoni yake kuhusu changamoto za kodi katika Wilaya yao ya Ubungo.
Kundi la Wakazi wa Wilaya ya Kinondoni wakijadili changamoto za kikodi katika wilaya yao.
Kundi la Wakazi wa Halmashauri ya Ilala wakijadili changamoto za wilaya yao kwa upande wa Kodi.
Kundi la wakazi wa Halmashauri ya Ubungo wakijadili changamoto za Kodi katika Wilaya yao.
Semina ikiendelea.
0 comments:
Post a Comment