METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, June 10, 2020

DKT. ABBASI: WATAKAOSHINDWA KUFUATA MWONGOZO AFYA MICHEZONI WATACHUKULIWA HATUA KALI


Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi akiendelea na ukaguzi wa miundombinu katika Kiwanja cha CCM Kirumba, Mkoani Mwanza.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi akizungumza na waandishi wa Habari katika Uwanja wa Nyamagana, Mkoani Mwanza

Wachezaji wakifanya mazoezi katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mkoani Mwanza ikiwa ni maandalizi ya mechi zitakazofanyika katika uwanja huo hivi karibuni.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, leo tarehe 9 Juni, 2020, ameendelea na ziara ya kukagua, pamoja na mambo mengine, utayari wa viwanja mbalimbali vya soka kabla ligi hazijaanza.


Akiwa jijini Mwanza jana Dkt. Abbasi aliwaeleza wadau wa michezo kuwa Serikali imechukua uamuzi mgumu wa kufungua michezo yote nchini na tayari ratiba za mechi mbalimbali katika Ligi Kuu ya Soka Nchini imetoka na timu zimeanza mazoezi, vilevile Serikali imetoa ruksa kwa mashabiki watakaotaka kuhudhuria  viwanjani waruhusiwe kwa taratibu maalam.

Katika hatua nyingine Dkt. Hassan Abbasi amesisitiza kuzingatiwa kwa Muongozo wa Afya Michezoni ikiwemo mashabiki na wachezaji kunawa kwa maji tiririka na sababu au kutumia vipukusi kabla ya kuingia viwanjani, kupimwa joto na mashabiki kukaa kwa kuachiana mita moja na kusisitiza yeyote atakayekiuka taratibu hizo atachukuliwa hatua stahiki ikiwemo viwanja husika kufungiwa kutumika kwa ligi.

“Tumefanya mazungumzo na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mheshimiwa Katibu Tawala wa Mwanza na wadau mbalimbali na wote wako tayari kuhakikisha yale yote ambayo Serikali imeagiza kwenye mwongozo yanazingatiwa,” alisema Dkt. Abbas wakati akiongea na wadau wa michezo Mkoani Mwanza akiwa Uwanja wa CCM Kirumba. 

Katika ziara hiyo Dkt. Abbasi ameambatana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Yusuf Singo na walitembelea pia kukagua viwanja vya CCM Kirumba na Nyamagana.

Katika hatua nyingine, leo akiwa Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza na baadaye mkoani Shinyanga, Dkt. Abbasi amewapongeza wadau binafsi waliojenga viwanja vya Gwambina (Misungwi); na Uwanja wa Mwadui Complex na uwanja mwingine mpya vilivyoko Shinyanga Mjini.

“Uwekezaji huu ni mkubwa na umechangia juhudi za Serikali katika ujenzi wa miundombinu ya michezo namwagiza Mkurugenzi wa Michezo awaletee wataalamu wetu ili washirikiane nanyi utaalamu katika baadhi ya maeneo hasa utunzaji wa nyasi za viwanja," aliagiza.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com