Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa anaongea na watumishi wa Chuo cha Kilimo ( MATI) Mubondo ( hawapo pichani)
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (aliyevaa suti) akitizama shamba darasa la mapapai katika chuo cha Kilimo Mubondo wilaya ya Kasulu alipotembelea chuo hicho leo.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa ameshika chupa ya asali inayozalishwa na chuo cha Kilimo Mubondo wilaya ya Kasulu.Kushoto ni mkufunzi wa kilimo na ufugaji nyuki kibiashara Mwl.Elias Lubimbi akitoa maelezo .
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa ameshika mche bora wa mchikichi aina ya Tenera unaozalishwa katika shamba la Wakala wa Mbegu (ASA) kituo cha Bugaga wilaya ya Kasulu Mkoa wa Kigoma hivi leo.
Katibu Mkuu Wizara ya Killimo Bw.Gerald Kusaya (aliyevaa suti ya blu ) akiongea na Askari na Maafisa wa JKT Bulombora Kigoma alipotembelea kukagua utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu kuhusu uzalishaji miche bora ya zao la mchikichi.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akikagua shamba la mbegu bora ya mihogo inayozalishwa kwenye Kituo cha Wakala wa Mbegu (ASA) Bugaga wilayani Kasulu leo.
Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo ( MATI) vimeagizwa
kuhakikisha vinatumia wataalam wakufunzi na rasilimali ardhi kuzalisha mazao
mengi bora ili kuwa na uhakika wa kipato na kujiendesha kibiashara.
Agizo hilo limetolewa leo Jumanne na Katibu
Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya wakati alipotembelea Chuo cha Kilimo
Mubondo Wilaya ya Kasulu Mkoa wa Kigoma.
" Tumieni sayansi kuzalisha mazao ya
kilimo kwa kuhakikisha mnapima udongo na kujua virutubishi vinavyofaa ili mjue
zao gani na aina gani ya mbolea ili kuwa na mavuno ya kutosha kuwezesha vyuo
kujipatia mapato " Kusaya
Katibu Mkuu huyo alisema lengo la serikali
kuanzisha vyuo vya mafunzo ya kilimo ni kufundisha vijana na wakulima wengi
kanuni bora za kilimo ili waweze kutoa mchango katika kukuza sekta ya kilimo
nchini.
Amevitaka vyuo hivyo kutumia vema ardhi iliyopo
na teknolojia kutoa mafunzo bora na
kuzalisha mazao kibiashara ili wanafunzi
wanaohitimu waweze kuwa mahili katika kujitegemea na kuongeza ajira kupitia
kilimo na chuo kupata mapato .
" Vijana wengi watakapofanya vema na
kufanikiwa katika kuanzisha shughuli za uzalishaji mali kupitia kilimo ndio
itakuwa nafasi ya vyuo hivi kujitangaza na kuvutia vijana wengine na wakulima
kuja kujifunza " alisisitiza Katibu Mkuu huyo
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Kilimo MATI
Mubondo Hanif Nzury aliomba serikali ikipatie Chuo hicho trekta ili kiweze kutumia
kuongeza uzalishaji zaidi wa mahindi, alizeti na michikichi ombi ambalo Katibu
Mkuu alilikubali na kuahidi kulifanyia kazi.
Aidha Katibu Mkuu Kilimo amewataka Maafisa
Ugani kote nchini kuwasaidia wakulima kwa kuwatembelea na kuwapa ushauri juu ya
kanuni bora za kilimo .
Katika hatua nyingine Kusaya ameziagiza taasisi
zote chini ya Wizara ya Kilimo kuhakikisha wanashirikiana na Halmashauri nchini
kupima maeneo hayo na kupata hatimiliki ikiwa na lengo la kuyaepusha na uvamizi toka kwa wananchi
Wizara ya Kilimo inasimamia vyuo 14 vinavyotoa
Mafunzo ya stashahada (Diploma) na astashahada ( Certificate) pamoja na vituo vya utafiti 17 nchini.
“ Waziri Mkuu yuko mstari wa mbele kuhakikisha
nchi inajitosheleza kwa mafuta ya kula hivyo endeleeni kuzalisha miche mingi ya
michikichi ili wakulima wapande na hatimaye tupate mavuno mengi
yatakayotosheleza mahitaji ya mafuta” alisema Kusaya.
0 comments:
Post a Comment