NGUMI ni miongoni mwa michezo ambayo
imeitangaza na kuipa heshima Tanzania duniani kutokana na mabondia wake
kuonyesha uwezo mkubwa na kushinda katika mapambano mbalimbali ya Kimataifa.
Kutokana na sababu mbalimbali za kiutendaji wa viongozi wa mchezo huu,
ulipoteza sifa yake Kitaifa na Kimataifa na kudidimiza maendeleo yake hapa
nchini. Eleuteri Mangi wa Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dodoma anaelezea jinsi mchezo huo
unavyorejesha heshima iliyokuwa nayo Tanzania Kitaifa na Kimataifa katika miaka
ya 1970.
Mchezo wa ngumi ni miongoni mwa michezo
inayofahamika na kupendwa sana na watu wengi duniani. Kama ilivyo kwa michezo
mingine kama vile mpira wa miguu, mchezo huu umekuwa ni chanzo cha ajira na
hivyo kujipatia umaarufu mkubwa ambapo vijana wengi wanajiunga kwa lengo la
kujipatia kipato. Ndiyo kusema, michezo ni kiwanda kikubwa kinachobeba ajira
lukuki kwa vijana na wataalam wa michezo mbalimbali nchini na duniani kote.
Mchezo wa ngumi nchini Tanzania ulianza
kufahamika katika miaka ya 1950 ambapo miaka ya 1970 mabondia wake walianza
kufahamika katika mashindando mbalimbali ya Kimataifa. Medali ya kwanza ya
Kimataifa ililetwa na Titus Simba mwaka 1974 katika michezo ya Jumuiya ya
Madola iliyofanyika nchini Uingereza na mwaka 1998 bondia mwingine Michael
Yombayomba aliiletea Tanzania medali nyingine katika mashindano hayo ya Jumuiya
ya Madola yaliyofanyika nchini Malasia.
Huo ndio ulikuwa mwanzo wa Tanzania kufahamika
Kimataifa katika medani ya mchezo wa ngumi ambapo wanamasumbwi wengine kama
vile akina Makoye Isangula, Stanrey Mabesi, Benjamin Mwangata, Shaaban Matumla
na wengine walitamba na kuiletea Tanzania medali mbalimbali. Hata hivyo, kuzuka
kwa vyama vingi vya ngumi nchini kumekuwa chanzo cha kushuka kwa mchezo huo
katika kipindi cha muongo mmoja uliopita kutokana na viongozi wake kutoelewana
kiutendaji kutokana na sababu mbalimbali.
Kwa kulitambua hili, Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Johh Pombe
Magufuli kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeanza kuchukua
hatua kadhaa kuweza kurejesha heshima ya Tanzania Kitaifa na Kimataifa kupitia
mchezo wa ngumi.
Kuundwa kwa Kamisheni ya Kusimamia Ngumi za
Kulipwa nchini (TPBRC) ni mwanzo mpya unaodhihirisha nia ya dhati ya Waziri
mwenye dhamana ya masuala ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison
Mwakyembe (Mb). Utekelezaji wa agizo la kuanzisha TPBRC nchini umeanza kuleta
manufaa kutokana na shabaha ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka
2015-2020 katika kukuza michezo.
Ilani hiyo katika ukurasa wake wa 218 Ibara ya
161 imetamka “Katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi ya CCM 2015-2020 imebainisha CCM itaielekeza Serikali kuimarisha sekta
ya michezo ili kuinua kiwango cha michezo
nchini ikiwa ni pamoja kuifanya sekta ya michezo kutoa fursa
za ajira hususani kwa vijana”.
Kama michezo mingine, mchezo wa ngumi za
kulipwa unaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa Na. 12
ya mwaka 1967 na marekebisho yake Na. 6 ya mwaka 1971 pamoja na kanuni za
Usajili Na. 442 za mwaka1999.
Sheria hiyo iliyofanyiwa marekebisho ya Sheria
Na. 3 kifungu cha 18 ya mwaka 2018 kwa mamlaka aliyonayo Waziri mwenye dhamana
ya michezo nchini yameongeza wigo na kutambua michezo ya ridhaa na michezo
mingine ambayo yamepelekea kuundwa kwa Kamisheni ya Ngumi za kulipwa nchini.
Chombo hicho kimeleta mafanikio katika mchezo
wa ngumi za kulipwa nchini na umekuwa na mchango mkubwa katika kuajiri vijana
ambao wamekuwa na mafanikio kwa mtu mmoja mmoja akiwa mchezaji na taifa kwa
ujumla.
Katika kuthamini michezo nchini ikiwemo
masumbwi, Rais Dkt. Magufuli ni mpenda michezo amekuwa mstari wa mbele katika
kutambua na kuwatuza wanamichezo wanapofanya vizuri katika mashindano
mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Mapema mwezi Machi mwaka 2019, Rais
alidhihirisha uzalendo wake kwa michezo nchini kwa kuwapa wachezaji, viongozi
wao na bondia Hassan Mwakinyo zawadi ya viwanja vya kujengea nyumba mkoani
Dodoma kama ishara ya kuonyesha alivyofurahishwa kwa juhudi za wachezaji na
viongozi wao kuipa Tanzania ushindi.
“Nimeamua niwape zawadi kidogo kwa niaba ya
watanzania, nitawapatia viwanja vya kujenga nyumba wachezaji wote wa Taifa
Stars na viongozi wao, bondia Hassan Mwakinyo pamoja na mwalimu wako, zawadi
hiyo pia kwa Peter Tino na Leodegar Tenga” alisema Rais Dkt. Magufuli.
Bondia Hassan Mwakinyo anapongezwa kwa kazi
nzuri anayoendelea kuliwakilisha taifa vema katika mashindano mbalimbali
duniani ikiwemo kumtwanga Amel Tinampay raia wa Ufilipino kwa point katika
mchezo uliofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Novemba, 2019.
Hakika mchezo wa ngumi za kulipwa umekuwa
mwanzo mpya wa mabondia nchini kufanya vizuri katika mapambano waliyoshiriki.
Bondia Abdallah Paziwapazi alimchapa
Zulipikaer Maimaitiali raia wa China kwa
Knock Out katika pambano la
WBO Asia Pacific Super
Middle Title lililofanyika
nchini China mwezi Agosti, 2019 wakati Hamis Maya alimtwanga Piergiulia
Ruhe raia wa Ujerumani kwa Knock Out katika pambano la Global Boxing Council
Intercontinental Welter lililofanyika nchini Ujerumani mwezi Novemba, 2019.
Mabondia wengine waliofanya vizuri na kuliletea
Taifa sifa nzuri ni pamoja na Bondia Bruno Melkiory Tarimo (Vifua Viwili)
ambaye alimpiga Nathaniel May raia wa Australia kwa point katika pambano la
Boxing Federation International Super Feather Title lililofanyika nchini
Australia mwezi Desemba, 2019 na Bondia Salimu Jengo aliyemchapa Suriya
Tatakhun raia wa Thailand kwa KO katika pambano la Universal Boxing
Organization World Light Title lililofanyika Jijini Tanga mwezi Januari, 2020.
Akiwasilisha Bajeti ya Wizara yake ya Makadirio
ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2020/2021 Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amewapongeza wachezaji wa Kitanzania
wanaozidi kuongezeka na kufuzu vigezo vya kimataifa na kucheza michezo ya kulipwa katika nchi mbalimbali na kupeperusha vyema bendera
ya Tanzania.
“Nawapongeza wanamichezo wote nchini kwa
kupeperusha vyema bendera ya nchi yetu katika mashindano mbalimbali ya
kimataifa na hivyo kuitangaza na kuiletea heshima kubwa nchi yetu” alisema Dkt.
Mwakyembe.
Waziri Mwakyembe aliendelea kusema “Namshukuru
sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake thabiti na
hatua anazochukua kuimarisha michezo nchini. Nampongeza Makamu wa Rais na
Waziri Mkuu kwa kuipa wizara yangu ushirikiano mkubwa na msaada katika
kuendeleza michezo nchini. Pia niwapongeze watanzania kwa hamasa na uzalendo
wanaouonesha kwa timu zetu”.
Kwa upande wake Promota Shomari Kimbau ambaye
ni mdau wa mchezo wa masumbwi ameipongeza Serikali kwa kwa nia yake ya dhati ya
kusaidia na kusimamia mchezo huo na kuamini usimamizi bora wa mchezo huo nchini
ni mwanzo mpya wa Mchezo wa Ngumi za Kulipwa.
“Lazima yawepo mazingira mazuri ya kusimamia
mchezo huu, ili upendwe na watu wengine pamoja na kurudisha imani kwa wadau na
wawekezaji waweze kuwekeza fedha zao. Hiki kinachofanywa na Serikali ni kitu
kizuri na kinafaa kuungwa mkono na wadau wa mchezo huu” anasema Kimbau.
Awali Ngumi za Kulipwa zilisimamiwa na Vyama
tofauti tofauti ikiwemo Chama cha Wataalamu wa Mchezo wa Ngumi Tanzania (TPBO),
Pugilistic organization of Tanzania (PST) na Tume ya Wataalamu wa Mchezo wa
Ngumi Tanzania (TPBC).
Mtindo huo wa kuongoza mchezo wa ngumi za
kulipwa ulikuwa na namna ya vionozi na wachezaji kutoelewana wenyewe kwa
wenyewe kabla ya Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuingilia kati mgogoro huo na kuamua
kufanya mabadiliko katika mchezo wa Ngumi za Kulipwa ndipo TPBRC ilipoanzishwa
na kupewa mamlaka ya kusimamia Ngumi za Kulipwa mnamo mwaka 2018.
Kwa mujibu wa BMT, baada ya kuundwa
Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa yapo
mafanikio yanayodhihirisha kuimarika kwa
mchezo huo yanayochagizwa kuwepo kwa viongozi waliopatikana kwa uchaguzi
uliofanyika Machi 31, 2019 ambao ni Joe Anea (Rais), Agapita Basil Jambwale
(Makamu wa Rais), Yahya Poli (Katibu Mkuu), Bakari Songoro (Mweka Hazina),
Hamisi Kimanga na Nassoro Chuma (Wajumbe).
Aidha, kuunganishwa kwa wadau wa ngumi za
kulipwa umeibua mwamko mpya kwa wadau hao, mabondia wanafanya vizuri katika
mashindano ya kimataifa ndani na nje ya nchi, kuongezeka kwa idadi ya wakuzaji
wa mchezo wa ngumi, kuongezeka kwa
mapambano 35 ambayo yamefanyika kati ya Aprili, 2019 hadi Machi, 2020.
Fauka ya hayo, wadhamini kujitokeza kuwekeza
katika kusimamia na kuhakikisha haki za mabondia zinazingatiwa ikiwemo kupitiwa
kwa mikataba yao ya mapigano kabla ya pambano pamoja na kuimarika kwa mahusiano
ya vyombo vya kusimamia michezo katika nchi tofauti pamoja na vyama
vinavyoshindanisha mikanda tofauti duniani ikiwemo, WBO, WBA, WBC, ABU na UBO.
Hatua hiyo imesaidia wanachama wa Ngumi za
kulipwa waliosajiliwa kwa muda wa miaka mitatu kuanzia 2016 hadi 2019 kufikia
22, taswira ambayo inaonesha kuongezeka kwa mwamko wa kuanzisha na kusajili
vikundi vya sanaa na michezo nchini.
Kulingana na takwimu hiyo, kati ya vikundi 22,
vikundi 17 vinajihusisha na mchezo wa ngumi, sanaa na michezo mingine wakati
vikundi vitano tu vilivyoanzishwa na kusajiliwa vinajihusisha na mchezo wa
ngumi pekee.
Kwa hakika jambo hili linaonesha wazi kuwa
Serikali ya Awamu ya Tano imetekeleza agizo
la CCM katika ilani yake
iliyotolewa wakati wa uchaguzi wa 2015 kwani
kwa takwimu hizo ni kweli Serikali kwa kishirikiana na sekta binafsi
imeweza kuanzisha vituo vya kuendeleza vipaji vya wanamichezo mahiri na
kutumika kama vituo vya maandalizi ya wanamichezo wanaoiwakilisha Tanzania
katika michezo ya kimataifa.
Kwa mantiki hiyo, mwandishi wa makala hii
amebainisha kuwa mwamko wa kuanzisha michezo shirikishi ni mkubwa zaidi kuliko
mchezo mmoja mmoja na hatua hii Serikali inapaswa kupongezwa kwani chanda
chema huvishwa pete.
Kwa nafasi mafanikio haya na nafasi hii,
mwanamichezo anayeshriki katika mchezo wa ngumi akiwa katika kikundi mazoezi
(gym) anayonafasi kubwa zaidi ya kuwa mwanamasumbwi bora zaidi ya yule ambaye
yupo kweye masumbwi pekee.
Hatua hiyo inamsaidia mwanamichezo kuwa bora
katika mchezo katika kikundi ambacho kinahusisha mchezo zaidi ya mmoja ana
fursa ya kupata vifaa vinavyomsaidia kufanya mazoezi ya uhakika, utimamu wa
mwili na kupata msaada wa kitaalamu katika mchezo husika kutoka kwa walimu
mbalimbali wanaokuwepo wakati wa mafunzo na mazoezi yanayompa motisha
unaompelekea kuwa mwanamichezo bora.
Hakika Kamisheni ya Kusimia Ngumi za Kulipwa
imekuwa mwarobaini wa mchezo huo ambapo migogoro ya mara kwa mara imekuwa ni
historia ikiwemo mapromota kuvamia tasnia hiyo na kuharibu mustakabali mzuri wa
mchezo huo nchini.
Ni ukweli usiopingika, kila lenye mafanikio
halikosi kuwa na changamoto, mchezo wa ngumi za kulipwa bado unakabiliwa na
changamoto ya kutokuwepo kwa makocha wenye viwango vya kimataifa wenye nyota
zinazotakiwa, vifaa vya kufanyia mazoezi, uhaba wa wadhamini pamoja na maeneo
ya kufanyia mazoezi na ulingo unaotumika wakati wa mashindano. Kwa hakika
Serikalia ya Awamu ya Tano itaendelea kuzitatua changamoto zote zilizosalia na
kwa hakika mambo yatakuwa mazuri hivi punde.
Mafanikio haya yaliyofikiwa ni makubwa mno kwa
mchezo huu ulionza kuchezwa hata kabla nchi yetu haijatawaliwa na wakoloni
katika karne ya 19. Mchezo huu ulichezwa katika viwanja vikubwa vyenye
mikusanyiko mikubwa ya watu (Coliseum) huko Roma na (Arena) huko Athina,
iliyokuwa katika hekalu kubwa la ufalme wa Wayunani (Ugiriki) la Akropolis.
Viwanja hivyo vilikuwa ndio mwanzo wa ulingo wa kisasa kwani japokuwa ulingo wa
kisasa ni wa mraba lakini mwanzo wake ni Arena ya mduara.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment