METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, May 4, 2020

UVCCM YAIPONGEZA SERIKALI VITA DHIDI YA KORONA


Umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi UVCCM wilaya ya Ilemela umeridhishwa na kupongeza jitihada zinazochukuliwa na Serikali katika kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 unaotokana  na virusi vya Corona.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Comred Faida Bituro katika viwanja vya kituo cha polisi Kirumba  wilayani humo wakati akikabidhi ndoo thelathini za vitakasa mikono kwa mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Dkt Mathias Severine Lalika ili vikatumike kwa wananchi hasa wa maeneo ya sokoni, vituo vya afya na wale wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za ununuzi wake ambapo amesema kuwa Serikali chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwemo ya utoaji wa elimu ya tahadhari juu ya ugonjwa wa corona na kuwahudumia wagonjwa waliokwisha athirika na ugonjwa huo

'.. Kwa niaba ya umoja wa vijana wilaya ya Ilemela, tunaipongeza Serikali kwa hatua inazochukua dhidi ya kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19, Vita hii ni yetu sote tunapaswa kuiunga mkono Serikali yetu ..' Alisema

Aidha Mwenyekiti huyo amempongeza mkuu wa wilaya ya Ilemela na wataalamu wa afya wa wilaya hiyo kwa jitihada zao katika  kuhakikisha  ugonjwa huo hauenei zaidi katika wilaya hiyo huku akimshukuru Rais Mhe  Magufuli kwa kutowazuia wananchi kuendelea na shughuli zao za kila. 

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Dkt  Mathias Severine Lalika akipokea ndoo hizo za vitakasa mikono ameishukuru jumuiya hiyo kwa msaada walioutoa sambamba na kuwaahidi kuutumia vyema  huku akiwaomba wadau wengine kuiga mfano wa vijana hao katika kuunga mkono Serikali dhidi ya mapambano ya ugonjwa huu wa Covid-19 unaosumbua dunia kwa sasa.

Nae Diwani wa kata ya Kawekamo Mhe Japhes Rwehumbiza amemshukuru mkuu wa wilaya ya Ilemela kwa namna anavyosimamia vita dhidi ya ugonjwa huo sanjari na kuwaasa wananchi kutopuuza tahadhari zinazotolewa na wataalamu wa afya wa viongozi katika kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19.

Akihitimisha kaimu mkurugenzi ambae pia ndie mganga mkuu wa wilaya ya Ilemela Dkt Charles Marwa Samson mbali na shukrani amewakumbusha wananchi kuendelea kujikinga na ugonjwa huo kwa kuhakikisha wananawa mikono mara kwa mara kwa kutumia sabuni na maji yanayotiririka, kuvaa barakoa, kuepuka mikusanyiko, kujiepusha na safari zisizo za lazima na kutosalimiana kwa kushikana mikono.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com