Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati wa kukabidhi matrekta kwa wakulima wanaokopeshwa na Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) katika Mji mdogo wa Kibaigwa Mkoani Dodoma, leo tarehe 23 Mei 2020. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Spika wa Bunge la Tanzania Mhe Job Ndugai akisisitiza jambo wakati wa kukabidhi matrekta kwa wakulima wanaokopeshwa na Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) katika Mji mdogo wa Kibaigwa Mkoani Dodoma, leo tarehe 23 Mei 2020.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe Deogratius Ndejembi wakati wa hafla ya kukabidhi matrekta kwa wakulima wanaokopeshwa na Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) katika Mji mdogo wa Kibaigwa Mkoani Dodoma, leo tarehe 23 Mei 2020.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akimkabidhi Bi Khadija Ngolo ambaye ni Mkulima kutoka Kondoa wakati wa hafla ya kukabidhi matrekta kwa wakulima wanaokopeshwa na Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) katika Mji mdogo wa Kibaigwa Mkoani Dodoma, leo tarehe 23 Mei 2020.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb), Spika wa Bunge la Tanzania Mhe Job Ndugai (Mb) wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa kampuni ya AGRICOM, Wafanyakazi wa Mfuko wa Pembejeo za Kilimo -AGITF pamoja na wakulima wakati wa kukabidhi matrekta kwa wakulima wanaokopeshwa na Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) katika Mji mdogo wa Kibaigwa Mkoani Dodoma, leo tarehe 23 Mei 2020.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Serikali imebainisha kuwa sekta ya kilimo imeendelea kuwa muhimili muhimu katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Katika kipindi cha miaka mitano, Pato la Taifa linalotokana na kilimo, kwa kutumia bei za Mwaka 2015 limeongezeka kwa asilimia 17 kutoka Shilingi trilioni 25.2 Mwaka 2015 hadi Shilingi trilioni 29.5 Mwaka 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amebainisha hayo leo tarehe 23 Mei 2020 wakati wa kukabidhi matrekta kwa wakulima wanaokopeshwa na Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) katika Mji mdogo wa Kibaigwa Mkoani Dodoma.
Mhe Hasunga amesema kuwa sekta ya Kilimo imeendelea kutoa ajira kwa Watanzania kwa asilimia 58 Mwaka 2018, imechangia asilimia 28.2 ya Pato la Taifa ambapo sekta ndogo ya mazao imechangia asilimia 16.2.
Amesema kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa upatikanaji wa pembejeo zote za kilimo unakuwa kwa wakati zikiwemo mbegu bora, mbolea sahihi, viuatilifu sahihi na zana bora za kilimo.
Baadhi ya Mikakati ambayo Serikali imeiweka kwa lengo la kuinua kilimo nchini na kipato cha mkulima ni pamoja na kujenga miundombinu ya umwagiliaji, kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya mbolea, kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya uongezaji wa thamani ya mazao, kuimarisha mifumo ya uuzaji wa mazao, kuimarisha ushirika, kuimarisha huduma za ugani na mafunzo, kuwekeza katika utafiti wa kilimo, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya uhifadhi wa mazao n.k.
Amesema kuwa katika Mwaka huu wa fedha 2019/2020, Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Pembejeo za kilimo (AGITF) imetoa mikopo 93 yenye thamani ya Shilingi 836,359,000 ikiwemo tisa (9) ya mitambo ya mashambani, 80 ya Pembejeo, mmoja (1) wa Ukarabati, miwili (2) ya Miundombinu ya Kilimo na mmoja (1) wa fedha za kuendeshea shughuli za shamba.
Amebainisha kuwa huo ni ushahidi tosha wa nia njema ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwasaidia wakulima nchini ili waweze kuondokana na kilimo duni kisicho na tija.
“Sanjari na hilo, Wizara imeendelea kuhamasisha matumizi ya zana bora za kilimo ili kuongeza ufanisi katika shughuli za kilimo. Kutokana na jitihada hizo za Serikali, Wizara kupitia Mfuko wa Pembejeo katika kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi 2020 imetoa mikopo mbalimbali yenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 15.1 ambayo kwa pamoja imesaidia kuzalisha ajira takribani 864” Amekaririwa Mhe Hasunga
Kwa upande wake Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Job Ndugai ametoa Rai kwa wananchi waliokopeshwa matrekta kuhakikisha kuwa wanayatumia vizuri kuzalisha ili waweze kufanya marejesho kwa wakati na kwa kiwango kilichoainishwa kwenye Mikataba ya mikopo yao.
Amesema kuwa Uaminifu katika marejesho ya mikopo yao utawawezesha kumaliza deni kwa wakati na kuepusha ongezeko la gharama linalotokana na riba ya adhabu.
Kadhalika, Spika Ndugai ameishauri Wizara ya Kilimo kuongeza muda kwa wakulima hao kuanza kurejesha mkopo ambapo amependekeza walau mwaka mmoja kuliko muda mchache wa miezi sita ambao umewekwa kwa sasa.
Pia Spika Ndugai ameishauri Wizara ya Kilimo kutathimini namna inavyoweza kujenga Mabwawa kwa ajili ya kilimo cha Umwagiliaji katika Wilaya ya Kongwa.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment