Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omary Mgumba akiwa ndani ya moja ya ghala la Bodi ya Mazao Mchanganyiko ya kuhifadhia maharage kiasi cha tani 1,700 ambayo yanataraji kuuzwa hivi karibuni
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omary Mgumba akiwa pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko Dkt. Anselm Moshi ndani ya ghala la kuhifadhia mahindi ambayo yanataraji kuuzwa kwa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) hivi karibuni
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omary Mgumba akiwa pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko Dkt. Anselm Moshi ndani ya moja ghala la kuhifadhia mazao jana mara baada ya Naibu Waziri kuitembelea Taasisi hiyo Mtaa la Mbugani, Jijini Dodoma
Na Issa Sabuni, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Naibu Waziri Kilimo Mhe. Omary Mgumba aipongeza Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (Cereal and Other Produce Board of Tanzania – CPB) kwa kutengeneza faida ya shilingi Bilioni 3.9 baada ya kufanya vyema kwenye uuzaji wa mahindi, unga wa mahindi na maharage katika kipindi cha muda mfupi kuanzia Mwezi Julai 2019 hadi Mwezi Machi, 2020.
Naibu Waziri Mgumba alitoa pongezi hizo siku ya Jumamosi tarehe 17 Mei, 2020 mara baada ya kufanya ziara fupi kwa ajili ya kujionea namna ambavyo Watendaji wa Bodi wanavyotekeleza majukumu yao wakati huu wa ununuzi wa mazao kutoka kwa Wakulima.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Dkt. Anselm Moshi, amemwambia Naibu Waziri Mgumba kuwa faida hiyo imekuja baada ya Bodi hiyo kununua kiasi cha tani 9,537.9 za mahindi na kuzisagisha ambapo zilitoa tani 7,629.6 za unga wa mahindi wenye thamani ya shilingi bilioni 7.62 pamoja na pumba zenye thamani ya milioni 572 katika vinu vyake vya Arusha, Iringa na Dodoma.
Dkt. Moshi ameongeza kuwa, Bodi imefanya vizuri kwenye uuzaji wa nafaka na mazao mengine ambapo katika kipindi cha kuanzia Mwezi Julai, 2019 hadi Machi, 2020 Bodi imeuza ndani na nje ya nchi Jumla ya tani 15,000 za mahindi zenye thamani ya shilingi bilioni 7.7 na tani 29.27 za maharage zenye thamani ya shilingi milioni 55.61 ambapo katika mchanganuo; Tani 5,000 za mahindi zimeuzwa nchini Rwanda, tani 10,000 za mahindi zimeuzwa ndani ya nchi, ikiwemo tani 6,000 ziliuzwa kwa Shirika la Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa (WFP). Huku tani 29.27 za maharage zikiuzwa hapa hapa nchini kwa Mfanyabiashara mmoja.
Waziri Mgumba licha ya kuipongeza Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Menejimenti ya Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko amesema Taasisi hiyo, ijikite katika kuendelea kununua mazao ya kutosha kutoka kwa Wakulima wa hapa nchini lakini pia iendeleee kufanya biashara na kutengeneza faida mara dufu.
“Nawapongeza saana na mmekuwa Taasisi ya mfano chini ya Wizara yetu ya Kilimo; Niwaombe tu, endeleeni kununua mazao ya Wakulima kwa kuwa mtawahakikishia masoko ya mazao yao lakini pia mtaongeza ushindani sokoni, nendeni Benki, mkakope na kama mtaihitaji msaaada wetu sisi Viongozi wenu tupo, tutawasaidia kwa ajili ya kupata ruhusa ya kupata hakikisho la Serikali kutoka Wizara ya Fedha na Mipango”. Amesisitiza Mhe. Omary Mgumba.
Akijibu pendekezo hilo la Naibu Waziri, Dkt. Moshi amesema Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko imepanga katika msimu wa kilimo wa 2020/2021 kununua na kuuza tani 170,000 za mahindi, mtama, maharage na mchele na kuongeza kuwa tayari Taasisi hiyo imepata zabuni ya kuuza tani 132,000 za mahindi, mchele, mtama mweupe na maharage kwa Shirika la Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa (WFP).
Dkt. Moshi ameongeza kuwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko imekamilisha andiko la Mradi wa kuuza mihogo mikavu tani milioni 1.2 kwa mwaka nchini China na kwa sasa Taasisi ipo katika hatua ya kupata ardhi zaidi ya hekta 100,000 kwa ajili ya kufanya uwekezaji mkubwa wilayani Kilwa (Lindi) kwa kushirikiana na Kampuni tatu kutoka China ambapo lengo ni kujenga kiwanda cha kuzalisha ‘ethanol’ na wanga ‘starch’ itakayotokana na mihogo na mihogo mingine itasindikwa na kuwa chipsi za mihogo kwa ajilio ya kusafilishwa kwa matumizi ya chakula.
0 comments:
Post a Comment