METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, May 29, 2020

MTU MMOJA MBARONI KWA WIZI WA MAJI KAGERA


Mtu mmoja mkazi wa Mtaa wa Kabale Kangaiza  Kata Ijuganyondo Manisipaa ya Bukoba Mkoani Kagera anayefahamika kwa jina la Novat Danstan anashikiliwa na jeshi la polisi baada ya kukutwa akiwa amejiunganishia Maji ya Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA), bila mita na huku akitumia maji hayo kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kuuza kwa wateja wengine. 
 Hali hiyo imebainika me 28,2020 wakati  BUWASA wakiendelea   oparesheni yake ya kuwarudishia huduma ya Maji wateja ambao walisitishiwa huduma hiyo, ikiwa ni katika harakati za mapambano dhidi ya Corona, kufuatia uhitaji wa huduma hiyo muhimu hasa kipindi hiki. 
Kwa mujibu wa Mtuhumiwa huyo, anadai kuwa yeye alihamia eneo hilo baada ya Mwajiri wake (jina limehifadhiwa) kumtaka ahamie katika nyumba yake akiwa kama mwangalizi na mlizi wa eneo hilo, wakati akihamia hapo anadai kuwa alikuta Maji yakiwa yamekatwa japo kulikuwa na mvujo, hivyo alitumia nafasi hiyo kuunganisha bomba na kuanza kutumia Maji hayo pasipo kujua nini kinaendelea juu ya Maji hayo.
“Nina miezi miwili tangu nimehamia hapa, nilikuta hapa pamekanda hapaeleweki ndipo nilipoanza kupatengeneza na hapo ndipo niligundua uwepo wa bomba la maji na tep iliyokuwepo ilikuwa ikivuja na kusababisha maji kumwagika, nikaona nichukue fursa hiyo kuunganisha tep mpya maana nilisoma shule namna ya kuunganisha maji na nikaanza kutumia japo sikujua utaratibu ukoje.” Alisema Mtuhumiwa huyo. 
Nae mwajiri wake alipoulizwa juu ya hilo, amedai kuwa hamkumuagiza Mtuhumiwa kufanya tukio hilo aliloliita Wizi, na kwamba kazi aliyompa ni kulinda Mali zake na si vinginevyo.
Akizungumza kwenye eneo la tukio Mkurugenzi Mtendaji wa BUWASA Bwn. John Sirati amesema kumbukumbu zinaonesha kuwa akaunti ya mteja wa maji hayo ni inajulikana Kwa jina la Faustine Buchwa ambae awali alikuwa akitumia Maji hayo kabla ya kusitishiwa mwaka 2017, hivyo mtuhumiwa amekutwa kajiunganishia huduma hiyo bila kulipia wala hana mita na Mamlaka haina taarifa, hivyo kusababisha upotevu wa Maji mengi.
“Mteja huyu tulimsitishia huduma ya maji tangu mwaka 2017 baada ya kushindwa kulipia bili ya maji na tukaondoa mita moja kwa moja, ila tumesikitishwa na tukio hili ambalo ni hujuma kwa mamlaka, mtu huyu amejiunganishia maji bila kulipia na tunaamini maji haya yameanza kutumika kwa muda murefu hadi sasa tulipobaini na baya Zaidi anayauza kwa watu wengine.” Alisema Bw. Sirati. 
Sirati ameongeza kuwa zoezi la kubaini wateja waliojiunganishia Maji kinyemela ni endelevu, na kwamba kufuatia agizo la Waziri mwenye dhamana kuwarudishia huduma wateja waluositishiwa, hivyo BUWASA inawataka wateja hao kufika Ofisini na kuingia Makubaliano namna ambavyo wataweza kulipia bili zao za awali wakati wakiendelea kutumia huduma ya Maji upya. 
Aidha ametoa wito kwa wananchi wanaotumia maji ya mamlaka hiyo kuwasiliana na mamlaka pale wanapohitaji huduma ya maji ama tatizo lolote linalohusiana na maji kuliko kuchukua hatua wenyewe hali itakayowapelekea kupambana na mkono wa sharia.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com