Na Mathias Canal, Runzewe-Geita
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli amewaambia wananchi Wilayani Bukombe
Mkoani Geita kuwa wamepata Mbunge Doto Biteko ambaye ni mwaminifu kwao na
serikali kwa ujumla hivyo wanapaswa kumuunga mkono ili atekeleze majukumu yake
kwa ufasaha kwa mujibu wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka
2015-2020.
Rais Magufuli ameyasema hayo
wakati akihutubia mamia ya wananchi wa Wilaya ya Bukombe wakati wa uzinduzi wa
barabara ya Uyovu-Bwanga yenye urefu wa kilomita 45 huku akisisitiza kuwa tangu
amchague Mhe Biteko (Mb) kuwa Naibu Waziri wa Madini anafanya kazi nzuri kwa
manufaa ya watanzania.
"Ndugu zangu wananchi mimi
nitawashangaa sana kama mtaanza kubadilika badilika nakumbuka nilikuja hapa
nikawaomba kura na nikamuombea kura Doto na nyinyi baada ya kumpa kura nyingi
nikaamua kumpa unaibu Waziri ili awatumikie vizuri" Alikaririwa Mhe Rais
Dkt Magufuli
Rais Magufulu alisema kuwa, Mhe
Biteko alikuwa mwenyekiti wa kamati Maalumu ya Bunge ya kuchunguza
uchimbaji na biashara ya Madini ya Tanzanite hivyo akafanya kazi nzuri ya
kujitoa kwa ajili ya watanzania.
JPM kwa msisitizo mkubwa
ameongeza kuwa wakazi wa Jimbo la Bukombe wana Mbunge mzuri ambaye anawasemea
kila kitu hivyo uwepo wake serikalini utaongeza tija na manufaa kwa watanzania.
"Yaani waheshimiwa
wananchi Hamkukosea kumchagua Mbunge Doto tena niwaambie sijui kama mtampata
Doto mwingine inawezekana ana sura mbaya lakini ni kiongozi bora tena bado
kijana anapaswa kuwatumikia vyema wananchi kwani ndio mtakaomsaidia katika
maisha yake ya badaye" Alisisitiza Rais Magufuli
Pasina hiyana hapo hapo Rais
Magufuli alimgeuzia kibao Mhe Doto na kumsihi kwa sifa hizo asije akabweteka
kwani wananchi na Taifa kwa ujumla linamtegemea sana.
Naye Mbunge wa Jimbo hilo la
Bukombe Mhe Doto Mashaka Biteko amempongeza Rais Magufuli kwa namna ya kipekee
ya ufanyaji kazi kwani amewakumbuka wananchi wa Wilayani ya Bukombe ambapo
pamoja na Ujenzi wa barabara aliyoizindua ya Uyovu-Bwanga yenye urefu wa
kilomita 45 pia alitoa fedha kwa ajili ya Ujenzi wa shule ya msingi Ibamba,
ambayo ipo kwenye Kata ya Uyovu kwani baada ya tangazo la elimu bure jumla ya
wanafunzi 1250 walijiandikisha darasa la kwanza hivyo Rais Magufuli akaamua
kuongeza Ujenzi wa vyumba vya madarasa 8 na matundu 20 ya vyoo ili kukabiliana
na wingi wa wanafunzi hao.
Pia alimshukuru Rais Magufuli
kwa kutenga fedha kwa ajili ya Ujenzi wa barabara ya kutoka Uyovu kuelekea
Namonge mpaka Malandula, kutoa kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya
Upanuzi wa kituo cha afya Uyovu, jumla ya milioni 400 kwa ajili ya Ujenzi wa
kituo cha afya cha Ushirombo na magari mawili kwa ajili ya kubeba wagonjwa
(Ambulance).
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment