Waziri wa
Nishati, Dkt. Medard Kalemani ( kulia) na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey
Zambi,(kushoto)wakiteta jambo wakati wa
uzinduzi wa ujenzi wa miundombinu ya usambazaji
gesi asilia kwa matumizi ya majumbani katika eneo la Mnazi mmoja mkoani
Lindi Mei 30,2020.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani
akizungumza na wakazi wa eneo la Mnazi Mmoja mkoani Lindi wakati wa uzinduzi wa
ujenzi wa miundombinu ya usambazaji gesi
asilia kwa matumizi ya majumbani katika eneo hilo Mei 30,2020.
Waziri wa
Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa Serikali kupitia Shirika la
Maendeleo ya Petroli nchini ( TPDC) itasambaza na kuunganisha bila malipo
(bure) miundombinu ya usambazaji wa Gesi asilia kwa matumizi ya majumbani kwa
wateja wa awali katika mikoa yote nchini
itayofikiwa na huduma hiyo.
Dkt.
Kaleamni alisema hayo wakati akizindua mradi wa ujenzi wa miundombinu ya usambazaji
wa gesi asilia kwa matumizi ya majumbani katika Kijiji cha Mnazi Mmoja, mkoani
Lindi, Mei 30, 2020 na kuwataka wakazi wa eneo hilo kuchangamkia fursa hiyo ili
kujiletea maendeleo na kuondokana na uchafuzi wa mazingira, gharama kubwa za kununua mkaa na kuni pamoja
na adha kutafuta kuni porini kwa ajili ya kupikia.
Aliweka
wazi kuwa baada ya wateja hao kuunganishiwa miundombinu ya kusambaza gesi
asilia katika nyumba zao,Taasisi kama vile Shule, Hospitali au sehemu za
biashara kama vile Mahoteli, au Migahawa,
mteja atawekewa mita ya kupimia kiasi cha gesi anayotumia itakayofanya kazi
kama LUKU za umeme.
Alisema
baada ya kufungiwa miundombinu hiyo ya kusambaza gesi asilia, mteja atatakiwa
kununua uniti za gesi kulingana na mahitaji yake kama ilivyo katika umeme, na
kuzitumia endapo zitaisha kabla ya kuongeza nyingine, mita itafunga hadi pale
atakaponunua uniti zingine kuongezea, mfumo huo unaitwa malipo kabla ya
kutumia( Pre- Paid System).
Aidha, Dkt.
Kalemani alisema kwa familia ya watu sita(6) inakadiriwa kutumia kiasi cha gesi
ya shilingi 30,000 tu, kwa mwezi kwa matumizi yote ya kupikia bila kubagua aina
ya vyakula vinavyotumia muda mrefu jikoni kama vile Maharagwe ikilinganishwa na
gunia la mkaa ama kuni.
“Watanzania
wenzangu mnataka serikali iwape nini tena jamani,imegundua gesi asilia nchini
kwetu inayotuzalishia umeme, sasa tunasambaziwa gesi hii majumbani ili tuitumie
kupikia vyakula vyetu na hatulipii chochote wakati wa kuunganishwa kwa hawa
wateja wa awali, zaidi tutalipia kile tunachotumia na ni gharama ndogo mno
ukilinganisha na matumizi ya kuni na mkaa, hebu jitokezeni kwa wingi mfungiwe
gesi katika majumba yenu”, Alisema Dkt. Kalemani.
Vilevile
alieleza kuwa, serikali imeamua kufanya hivyo ili kuhamasisha matumizi ya gesi
asilia iliyopatikana kwa wingi hapa nchini, pamoja na kupunguza ukataji wa miti
hovyo kwa ajili ya kuni na kuchoma mkaa ili kusaidia juhudi za kutunza na
kuhifadhi mazingira yetu.
Alisema
mradi wa usambazaji wa gesi asilia ni endelevu, ambapo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 wateja wapya 2,000
wataunganishia gesi majumbani, 300 kati yao wanatoka Mkoa wa Lindi na vitongoji
vyake.
“Wakina
mama sasa mtaondokana na adha ya kutembea porini kutafuta kuni na kubeba mizigo
ya kuni, pia matumizi ya gesi majumbani kutaimarisha na kudumisha ndoa na
familia kwa kuwa hakutakuwa na sababu ya mtu kuchelewa kutoka kuokota kuni, au
kuzamia porini akichoma mkaa, na hata mabinti zetu watakuwa salama zaidi”,
alisisitiza Dkt. Kalemani.
Alitaja
mikoa inayofuata sasa katika utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya kusambaza
gesi asilia kuwa ni pamoja na Morogoro, Dodoma na Singida: Mkoa wa Dar es
Salaam ukiongoza kwa kuwa na nyumba, mahoteli, viwanda na magari yanayotumia
gesi asilia.
Kwa upande
wake Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC , Dkt. James Mtaragio aliwatoa hofu watumiaji
wa gesi asilia majumbani kuwa usanifu na ujenzi wa miundombinu hiyo imezingatia
hatua zote za usalama ili kuhakikisha matumizi ya gesi hiyo yanakuwa salama
zaidi kwa mtumiaji na jamii kwa ujumla na hivyo kuwaomba wananchi kuondoa hofu katika
matumizi ya gesi asilia kwa shughuli za kupikia.
“Usalama wa
gesi hii unasababishwa na tabia yake kwani ni nyepesi kuliko hewa tunayovuta
hivyo kama ikitokea imevuja basi hupotelea hewani mapema na haiwezi kulipuka
wala kusababisha moto, vilevile usambazaji wa gesi hii ni salama zaidi kwa kuwa
husambazwa katika mgandamizo mdogo kwa njia ya bomba tofauti na gesi nyinyine,
ni imani yangu kuwa wananchi wengi mtatumia gesi hii kwakuwa ni salama zaidi na
nigharama nafuu mno,” Alisema Dkt. Mataragio.
Akizungumzia
gharama za matumizi ya gesi hiyo ikilinganishwa na mkaa pamoja na kuni,dkt.
Mataragio Alisema kuwa kwa ulinganishi matumizi ya mkaa si chini ya shilingi
4,500 kwa wiki,wakati matumizi hayohayo kwa kutumia gesi ni shilingi 1000 tu.
Naye mkuu
wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi alisema kuwa Mkoa wa Lindi umeandika historia
nyingine iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu ya ujenzi wa miundombinu ya
usambazaji wa gesi asilia itakayokuwa ikitumika kwa kupikia majumbani,
mahotelini kwenye taasisi za afya, elimu na matumizi mengineyo kama viwandani
na kuendeshea magari.
Zambi
aliishukuru serikali kupitia Wizara ya Nishati na TPDC kwa kutenga fedha
zitakazowezesha utekelezaji wa mradi huo katika Mkoa wa Lindi na baadae kote
nchini aidha aliwashukuru wanalindi kwa ushirikiano waliouonyesha katika
kipindi chote cha kutekeleza mradi huo na kuwaomba waendelee na moyo huo wa
kizalendo
“Wanalindi
tuchangamkie fursa hii, matumizi ya gesi asilia ni rahisi zaidi ukilinganisha
na nishati aina yoyote ile,mnajua wenyewe mnavyonunua mkaa bei ghali, kuni na
hata kuhangaika kutafuta kuni porini na wakinamama na binti zetu ndiyo
waathirika wakubwa, hima sasa tukujitokeze kuunganishiwa gesi ambayo ni bure
kabisa”, Alisema Zambi.
Tukio hilo
la uzinduzi wa gesi asilia, lilihudhuriwa pia na naibu waziri wa nishati, Mhe.
Subira Mgalu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said, baadhi ya
wambunge wa Mkoa wa Lindi na viongozi wengine waandamizi kutoka Wizara ya
Nishati na taasisi zilizochini yake, pamoja na viongozi wa dini, chama na
serikali wa mkoa kwa ujumla.
Kwa mujibu
wa takwimu zilizopo, kati ya futi za ujazo trilioni 57.54 za gesi asilia
zilizogunduliwa nchini, kiasi cha futi za ujazo trilioni 1.3 zimetengwa kwa
matumizi ya majumbani,viwandani,taasisi mbalimbali na kwenye magari, kiasi
hicho kitatumika kwa takribani miaka 30 ijayo.
0 comments:
Post a Comment