METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, May 8, 2020

DKT KALEMANI NA MHE.ZUNGU WAKAGUA MABWAWA YA KIDATU NA MTERA

Waziri wa Nishati Dkt.Medard Kalemani (wa pili kulia) Waziri wa Nchi Ofisi wa Makamu Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Hassan Zungu,(wa tatu kulia) na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said(wa kwanza kulia) wakiwasili kwenye ukaguzi wa Bwawa la Mtera ambalo lipo Mkoani Iringa, tarehe 7 Mei mwaka huu.
Waziri wa Nishati Dkt.Medard Kalemani(wa kwanza kushoto) Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe.Loata Ole Sanare(katikakati) Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said(kulia) wakielekea kwenye ukaguzi wa Bwawa la kidatu, Mkoani Morogoro, Mei 7,2020 
Waziri wa Nishati Dkt.Medard Kalemani(mwenye shati la bluu) akizungumza na waandishi wa Habari mara baada kumaliza kufanya ukaguzi wa Bwawa la Kidatu Mkoani Morogoro, Mei 7,2020.
Waziri wa Nchi Ofisi wa Makamu Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Hassan Zungu (katikati), akizungumza na waandishi wa Habari mara baada kumaliza kufanya ukaguzi wa Bwawa la Mtera Mkoani Iringa, Mei 7,2020.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said(aliyevaa miwani) akizungumza na waandishi wa Habari mara baada kumaliza kufanya ukaguzi wa Bwawa la Kidatu Mkoani Morogoro, Mei 7,2020.
Picha ya taswira ya Bwawa la Kidatu ambalo Waziri wa Nishati Dkt.Medard Kalemani na Waziri wa Nchi Ofisi wa Makamu Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Hassan Zungu walifanya ziara ya ukaguzi kwenye Bwawa hili lililopo Mkoani Morogoro, Mei 7,2020.
Waziri wa Nishati Dkt.Medard Kalemani tarehe 7 Mei mwaka huu amefanya ziara ya kikazi kwenye kwenye vituo vya kufua umeme kwa maji vya Mtera na Kidatu vilivyopo Mkoani Morogoro na Iringa.
Katika ziara yake hiyo aliambatana na Waziri wa Nchi Ofisi wa Makamu Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Hassan  Zungu, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said pamoja na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Nishati na Ofisi ya Makamu wa Rais(Mazingira).
Akizungumza na waandishi wa habari, wakati akiwa kwenye ziara hiyo Dkt. Kalemani alisema lengo la ziara hiyo ni kuhakikisha kuwa maji ya kutosha yanapatikana ya kuzalisha umeme wa kutosha na wa uhakika pamoja na kuangalia athari za mazingira kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha nchini.
Dkt. Kalemani alisema, kufuatia athari zilizojitokeza kipindi cha mvua wameunda timu ambayo itakuwa chini ya Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said itakayoshirikisha wataalamu mbalimbali ili kuja na mipango ambayo itasaidia kuondoa athari zilizojitokeza katika mabwawa hayo.
Amesema kuwa, Bwawa la Kidatu lina kimo cha mita 450 ambavyo ndio kimo chake cha juu cha kujaa kwa maji na ikitokea yamejaa zaidi ya hapo yanahitajika kufunguliwa, na kuruhusiwa  kwenda mbele ili kwenda kulijaza Bwawa la Rufiji, na kuwataka wataalamu wanaohusika na shughuli hiyo kuhakikisha wanapoyafungulia hayaleti madhara yoyote ya kimazingira.
Ameongeza kuwa,waatalamu hao wanapofunguliwa  maji hawapaswi kuwafungulia na kuwacha yakizaga badala yake wayafungulie ili kwenda kwenye mkondo wake unaostahili, kwakuwa yanapozagaa ndio madhara yanapotokea  kwa wananchi ambao wanaishi kandokando ya maeneo hayo.
“ Tuna jukumu kubwa la kuhakikisha maji hayaleti madhara nilipokuja kipindi cha nyuma niliona madhara kwenye baadhi ya maeneo na ndio maana nikaunda timu kupitia kwa Katibu Mkuu na baadhi ya viongozi wa Mikoa inayozunguka bwawa hili wafanya uratibu ili kuhakikisha yasiendele kuleta madhara kwa wananchi wanaoishi jirani na maeneo hayo lazima tuyalinde mazingira yetu” alisema Kalemani.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya mito kuwa wachukue tahadhari ili wasije wakathirika kipindi cha mvua kubwa, na kuwataka kutunza vyanzo vya maji na kulima kwa ustarabu bila kuathiri vyanzo hivyo.

Pia, amewataka waatalamu kutoka Shirika la Umeme Tanzani(TANESCO) kuhakikisha kipindi ambacho kuna maji ya kutosha na umeme umezalishwa wa kutosha wahakikishe kuwa umeme hauzimwi nchini kwasababu hakuna sababu ya kufanya hivyo katika kipindi hiki.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi wa Makamu Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Hassan, amesema lengo la Serikali ni kulinda vyanzo vya maji kwasababu maji yakikosekana umeme utashindwa kuzalishwa nchini na umeme usipozalishwa uchumi wa nchi yetu utayumba na nchi inategemea umeme na umeme wa bei chini ni umeme unaotokana na vyanzo vya maji.
“vyanzo vya maji vilindwe, vyanzo hivi visipolindwa vitashindwa kusafirisha maji kwenda kwenye miradi mikubwa kama mradi wa umeme wa Julius Nyerere kwahiyo lazima tuliende vyanzo vyetu kwa umakini zaidi” Alisema.
Aidha, amesema ametoa siku kumi kwa timu iliyoundwa ambayo ipi chini ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, kutoa taarifa rasmi ya namna gani sasa ya kwenda kuhakikisha vyanzo vya maji vinalindwa na umeme wa uhakika unapatikana nchini.
Nae, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said, amesema kuwa yeye na pamoja na timu ambayo imeundwa watakaa na wataalamu mbalimbali ili kuangalia data za miaka ya nyuma ili waweze kuona watazitumiaje kuweka mipango ya kuzuia uharibifu usitoke kwenye vyanzo hivyo vya umeme.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com