Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe.Martin Shigela (katikati) akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (wa kwanza kushoto) mara baada ya mazungumzo yao kuhusu mkakati wa kukuza kilimo cha mpunga mkoani Tanga leo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa na Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Mlingano Dkt.Catherine Sendoro wakati alipotembelea kituo hicho wilayani Muheza
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akipata maelezo ya namna mbegu bora za mkonge zinavyozalishwa kwenye vitalu kwa njia ya maabara.Kulia ni Mtafiti wa zao la mkonge Gelleson Mkongwe wa kituo cha TARI Mlingano akitoa maelezo
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (aliyeinama) akiangalia mbegu bora za zao la mkonge zilizozalishwa kwa njia ya maabara ya sayansi katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Mlingano wilaya ya Muheza mkoa wa Tanga.
Watumishi wa sekta ya kilimo nchini wametakiwa
kufanya kazi kwa kujiamini na weledi ili kuongeza tija katika kuhudumia
wakulima na hivyo kufanya sekta ya
kilimo iwe na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.
Kauli hiyo imetolewa leo (27.04.2020) wilayani
Muheza mkoa wa Tanga na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakati
alipoongea na watumishi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Mlingano na wale
wa Chuo cha Mafunzo Kilimo
(MATI)Mlingano.
“ Watumishi msijione wanyonge kwenye shughuli
zenu,nataka mjiamini na muwe wabunifu katika kutekeleza kazi za wananchi ili
tija iongezeke kwa wizara na taasisi zake kutoa huduma bora “ alisema Kusaya
Kusaya alisema ni wakati muafaka sasa watafiti
wa zao la mkonge kujikita katika kutoa matokeo chanya ya mbegu kwani kuna
maeneo mengi nchini kama wilaya za Kahama,Kishapu,Kilosa na Geita wameonesha
nia ya kuanzisha mashamba ya zao la mkonge.
Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa kituo cha
TARI Mlingano ,Mkuu wa kituo hicho Dkt.Catherine Senkoro alisema uzalishaji wa mbegu mpya za mkonge
zenye uwezo mkubwa wa mavuno umefikia
mbegu 500,000 kati mahitaji ya wakulima ya mbegu 1,600,000 kwa mwaka.
Dkt.Senkoro alisema kwa sasa wana mkakati wa
kuzalisha mbegu bora za mkonge kwa kutumia teknolojia ya maabara na vipando ili
kuweza kufikia lengo la kuzalisha mbegu 2,000,000 ifikiapo mwaka 2021.
Kufuatia hali hiyo Katibu Mkuu aliagiza taasisi
ya TARI Mlingano kuhakikisha inazalisha mbegu 5,000,000 kwa mwaka na kuwa
Wizara yake itatoa fedha za kuwezesha utafiti na uboreshaji maabara ya kupima
afya ya udongo na ile ya kuzalisha mbegu bora za mkonge.
“Wizara ya Kilimo ipo tayari kusaidia kituo
hiki kupata fedha za kutosha ili kuzalisha mbegu bora za mkonge na kuwafikia
wakulima wengi zaidi kama alivyoagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati
alipotembelea kituo hiki Machi mwaka huu” alisema Kusaya
Kwa mujibu wa Dkt.Senkoro kwa sasa ekari moja
inazalisha tani moja ya mkonge wakati China wanazalisha tani tano kwa ekari na
kusema taasisi hiyo inahitaji kuongezewa nguvu ili izalishe mbegu bora zenye
kutoa matokeo makubwa kwa wakulima.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu huyo
alitembelea na kuongea na watumishi wa wa Vyuo vya mafunzo ya Kilimo ambapo aliwataka wawe watulivu wakati
serikali ikifanya maboresho na ukarabati
wa miundombinu ya chuo hicho.
Kusaya aliwakumbusha watumishi hao kuwa kazi ya
ualimu ni ya wito hivyo wasichoke badala
yake waifanye kwa moyo na jitihada kufundisha vijana na wakulima mbinu bora za
kilimo.
Katika kuhakikisha watumishi wanakuwa na weledi
wa kazi,Katibu mkuu Kusaya amewataka watumishi kujitokeza na kuomba nafasi ya
kwenda masomoni kujiendeleza kielimu na kuwa serikali itawezesha .
“Katika kipindi hiki nataka watumishi wa wizara
ya Kilimo na taasisi waweze kujiendeleza kwa mafunzo ya muda mrefu au mfupi ili wasaidie serikali kuboresha
utoaji huduma na tija katika usimamizi wa sekta ya kilimo nchini .” alisisitiza
Kusaya
Nao watumishi
Mary Zakayo na Valentine Njau wa chuo cha MATI Mlingano walimuomba
Katibu Mkuu asaidie waweze kupata stahili zao za malipo ya likizo na madeni ya
vibarua.
Akijibu maombi hayo ,Kusaya alisema kuanzia
mwezi ujao Mei watumishi hao watalipwa
madeni yao kwani Wizara imepokea tayari shilingi Bilioni Tano kulipa madeni ya
watumishi na watoa huduma kwa taasisi zote chini ya Wizara ya Kilimo.
0 comments:
Post a Comment