Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (aliyeshika sahani) akikagua ubora wa mahindi yaliyohifadhiwa katika ghala la Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Shinyanga leo
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (aliyevaa koti la bluu) akiongea na watumishi wa NFRA Kanda ya Shinyanga wakati alipokagua ghala la hifadhi ya mahindi leo mjini Shinyanga,
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya ( ) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Kituo cha Afya ya Mimea Kanda ya Shinyanga wakati alipotembelea kuongea na watumishi wa taasisi hiyo iliyo chini ya wizara ya Kilimo.
Picha na Habari na Wizara ya Kilimo.
Wizara ya Kilimo imeiagiza Wakala wa Taifa wa
Hifadhi ya Chakula (NFRA) kubuni njia muafaka ya kuongeza mapato kwa kuhifadhi nafaka zaidi na kufanya biashara ya
mazao ya kilimo.
Agizo hilo limetolewa leo (28.04.2020) mjini Shinyanga na Katibu Mkuu
wa Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakati alipofanya ziara ya kukagua shughuli
zinazofanywa na wakala kanda ya Shinyanga.
“Kuanzia sasa nataka kuona NFRA inafanya kazi
kwa kujitegemea zaidi bila kutegemea fedha za serikali kwa kubuni mikakati ya
kutumia uwepo wa vihenge vya kisasa na ghala vinavyojengwa na serikali hapa
Shinyanga” alisema Kusaya
Alibainisha kuwa serikali inatekeleza mradi
mkubwa wa shilingi Bilioni 15.24 wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi kwa kujenga
vihenge (silos) sita zenye uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 na ghala moja kubwa
lenye uwezo wa kuhifadhi tani 10,000 za nafaka katika eneo la Ibadakuli mkoani
Shinyanga.
Alieleza kuwa mradi huo ni wa mafanikio kwani
utawezesha uhifadhi wa mazao toka kwa wakulima kuongezeka toka tani 14,500 za
sasa hadi tani 44,500 kwa mwaka utakapokamilika mwezi Juni mwaka huu.
“Tafuteni mbinu itakayoifanya NFRA mhifadhi
nafaka nyingi zaidi kama mahindi,choroko,maharage ,mpunga na ziada muweze kuuza
na kupata fedha za kujiendesha kibiashara ikiwemo kutumia fursa ya mahitaji
makubwa ya nafaka hususan chakula kwenye nchi za jirani na Tanzania” alisitiza
Kusaya.
Katika hatua nyingine Kaimu Meneja wa Kanda ya
Shinyanga Meriana Yateri ameishukuru serikali kwa uamuzi wake wa kujenga
vihenge vya kisasa na ghala kwani vitasidia kuongeza uwezo wa kanda na nchi
kuhifadhi mazao mengi yatakayotumika wakati wa dharura na majanga.
0 comments:
Post a Comment