Bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 imeongezeka hadi kufikia kiasi cha sh.
bilioni 40.1 kutoka sh. Bilioni 30.9 kwa mwaka wa fedha uliopita ili kutekeleza
majukumu yake kwa ufanisi.
Akiwasilisha hotuba ya Bajeti hiyo Bungeni
Jijini Dodoma, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison
Mwakyembe amesema kuwa ongezeko la sh.
bilioni 9.2 ambalo ni sawa na zaidi ya asilimia 29.2 itaenda kutekeleza miradi
ya maendeleo.
“Katika mwaka wa fedha ujao fedha zitaenda
kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara
la Afrika yenye kiasi cha sh. milioni
515, Chuo cha Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) kilichotengewa sh. milioni
250 kwa ajili ya ukarabati wa chuo hicho pamoja na Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kiasi cha
sh. milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, mabweni pamoja na
viwanja vya michezo”, alisema Mhe.Mwakyembe.
Dkt. Mwakyembe ameongeza kuwa miradi mingine
itakayotekelezwa ni ujenzi wa eneo Changamani la michezo Dar es Salaam na
Dodoma ambao umetengewa kiasi cha sh. milioni 650, mradi wa upanuzi wa usikivu
redio za TBC Taifa na TBC FM ambao umetengewa kiasi cha sh. bilioni 5 pamoja na
mradi wa Habari kwa Umma ambao umetengewa kiasi cha sh. bilioni 1
inayofanya miradi yote kutekelezwa kwa
jumla ya sh. bilioni 7.7.
Akizungumzia sekta ya michezo, Mhe.Waziri
amesema kuwa ni sekta ambayo inaimarisha
afya na kulitangaza Taifa ndio maana leo nchi inasikika katika matangazo ya
Premier League na UEFA kupitia vijana wanaocheza michezo ya kulipwa nje ya nchi
akiwemo Mbwana Samatta pia mafanikio ya
timu ya wanawake ya mpira wa miguu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,
Dkt.Hassan Abbasi amesema kuwa Serikali imefanya mambo makubwa kwa sekta za
Wizara hiyo muhimu kwa nchi, na fedha zilizopitishwa zitaenda kuboresha mkakati
wa kuitangaza lugha ya Kiswahili ambayo ni bidhaa adhimu Duniani kwa kuwekeza
kununua vifaa vya ukalimani, kufundisha wakalimani, kutengeneza vitabu ambavyo
vitakuwa ni miongozo ya ufundishaji wa lugha ya Kiswahili kwa wageni.
“Kwa mara ya kwanza tumepata bajeti kwa ajili
ya taasisi yetu ambayo ni Kampuni yetu ya Magazeti ya Serikali (TSN) ambayo kwa
miaka mingi ilikuwa inajitegemea na kujiendesha kibiashara lakini kwa sasa
Serikali imefanya uamuzi TSN watalipwa mishahara na Serikali ili waweze
kuwekeza katika maeneo mengine”, alisema Dkt. Abbasi.
Aidha, Dkt. Abbasi alifafanua kuwa mafanikio
yaliyopo katika Wizara hiyo yametokana na ushirikiano ambao inaupata kutoka kwa
wadau mbalimbali wakiwemo vyombo vya habari na wanahabari, wasanii,
wanautamaduni na wanamichezo wote nchini.
Akichangia mjadala wa bajeti hiyo, Mhe. Amina
amesema kuwa usimamizi mzuri na
utekelezaji wa majukumu ya Wizara hiyo umefanya sekta zake zifanye vizuri
ikiwemo sekta ya habari ambayo tofauti na nchi nyingi Duniani, Tanzania ina
jumla ya televisheni zilizosajiliwa 44
pamoja na vituo vya redio 186.
Kwa mwaka wa fedha 2020/2021, Wizara inatarajia
kukusanya jumla ya shilingi 960,000,000 kupitia Idara ya Habari - MAELEZO na Maendeleo
ya Michezo, kwa upande wa Taasisi saba zilizo chini ya Wizara, kiasi
kinachokadiriwa kukusanywa ni jumla ya shilingi 40,171,264,000.
0 comments:
Post a Comment