METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, March 10, 2020

WAZIRI MKUU AZINDUA MKAKATI WA KUPAMBANA NA UNYANYAPAA WA VVU NCHINI



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Kampeni ya Kitaifa  ya Viongozi wa Dini  na Bunge  katika  kuongeza jitihada za kupunguza unyanyapaa dhidi ya Ukimwi kwenye ukumbi wa Msekwa jijini   Dodoma, Machi 10, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wa dini wakati alipowasili kwenye ukumbi wa Msekwa jijini Dodoma, Machi 10, 2020 kuzindua Kampeni ya Kitaifa  ya Viongozi wa Dini  na Bunge  katika  kuongeza jitihada za kupunguza unyanyapaa dhidi ya Ukimwi. Kushoto ni Spika wa Bunge, Job Ndugai, wa tatu kushoto  ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama,Watano kushoto ni Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai na wa sita kushoto ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inatambua nguvu kubwa waliyonayo viongozi wa dini katika jamii na itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati katika kuyatekeleza na hatimaye kufikia malengo yanayotarajiwa katika mwitikio wa UKIMWI Tanzania.

“Serikali inaunga mkono tamko na maazimio mliyoyafikia leo hii na itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati katika kuyatekeleza na kufikia malengo yanayotarajiwa katika mwitikio wa UKIMWI Tanzania. Sote tunatambua nafasi na nguvu mlizonazo viongozi wetu wa dini katika jamii,” amesema.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Machi 10, 2020) kwenye ukumbi wa Msekwa, Bungeni jijini Dodoma wakati akizungumza na viongozi wa dini, wabunge, na wadau mbalimbali wa mashirika ya WAVIU kwenye uzinduzi wa kampeni ya kushirikisha viongozi wa dini kutokomeza unyanyapaa ili kufikia malengo ya kitaifa ya mwitikio wa UKIMWI nchini.

Kampeni hiyo inayoitwa “Hebu Tuyajenge, Tufikie 95-95-95: Tanzania bila Unyanyapaa Inawezekana, Viongozi wa Dini Tuongozee njia” inalenga kuhamasisha umma wa Watanzania waungane kutokomeza unyanyapaa dhidi ya VVU na UKIMWI Tanzania.

Akizungumza na viongozi hao, Waziri Mkuu amesema ana imani kubwa watalisimamia vizuri suala la unyanyapaa na ukatili wa kijinsia kwa kuwa jamii inawasikiliza, inawaheshimu na kuwaamini sana wao kuliko inavyowasikiliza wanasiasa au hata wanavyosikiliza na kuamini vyombo vya habari.

“Tambueni kwamba mnayo kazi kubwa ya kufanya katika kuhakikisha unyanyapaa na ukatili wa kijinsia unakwisha kabisa katika jamii yetu. Niendelee kuwaomba viongozi wetu wa dini kupitia ibada katika madhehebu yenu, vyombo vyenu vya habari, jumuiya, makongamano mbalimbali, taasisi zenu za elimu na afya, tuhakikishe tunatoa ujumbe wa kutia hamasa, elimu na upendo ili hatimaye wanaume, vijana na watoto wengi wazifikie huduma za VVU sambamba na kutambua haki na usalama wa mtoto.”

Amesema Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, itaendelea kutekeleza na kuboresha huduma za za afya ikiwa ni pamoja upimaji wa Virusi Vya UKIMWI, matibabu ya magonjwa nyemelezi pamoja na kupiga vita unyanyapaa wa aina zote kwa WAVIU.

Amesema Tanzania inaungana na nchi nyingine duniani zinazoamini katika kutokomeza unyanyapaa na ubaguzi wa aina zote lengo likiwa ni kutokomeza ubaguzi uwe wa kiitikadi au kijamii. “Kwa pamoja tuungane kukemea vitendo vya unyanyapaa na ubaguzi kutokana na madhara makubwa kwa watu wetu na Taifa kwa ujumla wake.”

Amesema licha ya dini zote kukemea ubaguzi na unyanyapaa, bado unyanyapaa, ukatili wa kijinsia hasa kwa watoto vimeshamiri katika jamii. “Watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU), hukumbwa na kadhia ya unyanyapaa katika jamii zetu. Kadhalika, watoto wa umri mdogo nao wanatendewa ukatili mkubwa sana kama vile kunajisiwa na kutelekezwa,” amesema.

“Vitendo vya namna hii hudhoofisha jitihada za kutokomeza maambukizi ya VVU kwani huwafanya watu kuogopa kujitokeza kupima VVU. Mtu huhofia kwamba ikijulikana ana maambukizi atabaguliwa na hivyo, kuishi maisha ya mateso yatokanayo na msongo wa mawazo na aibu ya kunyanyapaliwa.”

Katika kongamano hilo la siku moja, Mhashamu Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Mbeya na Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC); Askofu Mark Walwa Malekana wa Kanisa la Waadventista wa Sabato (SDA); Askofu Alinikisa Cheyo wa Kanisa la Morovian na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo (CCT); Askofu Peter Konki wa Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuberi (BAKWATA) walitoa ahadi zao za kuunga mkono kampeni hiyo kupinga unyanyapaa kwa kutumia ibada na taasisi zilizo chini yao na kisha kutia saini Tamko Rasmi la Viongozi wa Juu wa Taasisi za Dini kuhusu ushiriki wao katika mwitikio wa UKIMWI nchini.

Mapema, kongamano hilo lilipokea shuhuda kutoka kwa Mchungaji Prof. Gideon Byamugisha (61) wa kutoka Uganda, Mbunge kutoka Zambia wa chama cha United Party for National Development (UPND), Bi. Princess Kasune (45) na Bi. Pundensiana Mbwiliza (25), mfanyabishara ya mikoba ya vitenge kutoka Mwanza, Tanzania ambao wameishi na VVU kwa kati ya miaka 10 - 25 na wamekuwa mstari wa mbele kuvunja ukimya kuhusu hali zao na kupiga vita unyanyapaa.

Naye Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muunguno wa Tanzania, Mhe.  Job Ndugai alisema uamuzi wa kujuisha viongozi wa dini kwenye masuala ya kitaifa ulianza mwaka jana jijini Mwanza ambako waliowaomba viongozi wa dini wawasidie kuihamasisha jamii kuhusu tatizo la ugonjwa wa kifua kikuu.

“Tuliona kuwa kuweka msisitizo kwenye Kifua Kikuu peke yake haitoshi; tukaona ni vema tushirikiane nao tena ili watusaidie kusukuma uelewa miongoni mwa jamii kuhusiana na suala hili la VVU,” alisema.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com