METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, March 12, 2020

WANARUKWA WAHAMASISHWA, KUJALI NA KUWEKEZA KATIKA AFYA ILI KUTIMIZA MALENGO YAO

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (waliokaa Katikati) katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi wa Dini na Serikali pamoja na Watumishi wa mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Meneja wa NHIF, Dkt. Janet Pinda akitoa elimu juu ya huduma ya vifurushi vya Bima ya Afya mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo pamoja na Wakurugenzi wa halmashauri, Wakuu wa Wilaya na Viongozi wa Dini.

Meneja wa NHIF, Dkt. Janet Pinda.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wananchi wa Mkoa huo kutafakari namna ya kujali na kuwekeza katika afya kwa kutahadharisha kuwa kufanya hivyo ni jambo lisiloepukika ili kuweza kutimiza malengo ya kuimarisha afya zao na hatimae kujizatiti katika kuujenga uchumi wa mkoa kuanzia katika ngazi ya familia na hivyo kuwataka kujiunga na huduma za bima ya afya zinazotolewa na serikali nchini.
Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikifanya maboresho mbalimbali katika huduma za Afya ili kuhakikisha wananchi wake wanakuwa na Afya njema ambapo kwa kupitia Wizara ya Afya iliweza kuboresha Mfuko wa Huduma ya Afya ya Jamii (CHF) kutoka kutibiwa mahala ulipokatia kadi hadi kupata huduma kupitia kituo chochote cha kutolea huduma za afya nchini.
Aidha, ameongeza kuwa kutokana na takwimu za mkoa wa Rukwa kuwa chini katika kujiunga na mifuko hiyo amewataka, Wakurugenzi wa halmashauri, Wakuu wa Wilaya, atumishi wa vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na kuwaomba Viongozi wa Dini kuhamasisha wananchi wengi zaidi kujiunga na huduma mpya ya vifurushi vya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili kupata huduma bora na ya wakati.
Katika kipindi cha nusu mwaka wa 2019/2020 Mkoa wa Rukwa ulilenga kusajili wanachama 1,287 wa NHIF wasio Watumishi wa Serikali, lakini Wanachama waliosajiliwa ni 437 ambao ni sawa na asilimia 34 ya lengo.  Kwa upande wa huduma ya vifurushi vya NHIF tangu mpango huu uzinduliwe Wanachama 15 tu wameandikishwa kati ya Wanachama 523 waliolengwa kuandikishwa sawa na asilimia 2.8 (2.8%),” Alisema.
Halikadhalika, Amewataka wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanawasilisha michango ya watumishi wao wanaolipwa mishahara kwa mapato ya ndani pamoja na waheshimiwa madiwani ili kuepuka kuzorotesha juhudi kubwa zinazofanywa na serikali juu ya kuboresha huduma za afya kwa watumishi na viongozi wake na kuonya kuwa kutofanya hivyo kutasababisha huduma zao kusitishwa hali itakayopelekea fedheha kwa watumishi na waheshimiwa madiwani.
Mh. Wangabo ameyasema hayo katika ufunguzi wa kuitambulisha rasmi huduma ya vifurushi vya Mfuko wa Taifa wa Biama ya Afya katika semina iliyowajumuisha Wakurugenzi wa halmashauri, Wakuu wa Wilaya, Viongozi wa Dini pamoja na wataalamu wa sekta ya Afya ngazi ya mkoa
Wakati akitoa maelezo juu ya huduma hiyo ya vifurushi Meneja wa NHIF Mkoa wa Rukwa Dkt. Janeth Pinda amesema kuwa tangu kuzinduliwa kwa huduma hiyo wamekuwa wakitoa elimu kuanzia ngazi ya mtaa, vijiji na kata na hatiame kufanya semina na viongozi wa juu katika ngazi ya mkoa ambao wana ushawishi mkubwa kwa wananchi ndani ya mkoa na kwa kufanya hivyo kutawawezesha kufikia malengo ya serikali katika kutoa huduma bora kwa wananchi na hivyo kuomba ushirikiano kutoka kwa viongozi hao.
“Kuanzishwa hasa kwa hivi vifurushi vipya ilikuwa ni kuongeza wigo wa wananchi katika mfumo wa bima ya afya, kwasababu kama inavyofahamika kwa hapo awali ilikuwa kwa wananchi ama wafanyakazi ambao wako katika sekta rasmi, lakini wale ambao hawakuwa katika sekta rasmi haikuwa rahisi kuwafikia ili waweze kupata huduma za bima ya afya,” Alisema.
Hata hivyo alisema kuwa nia ya mfuko huo ni kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na elimu ya afya ili aweze kuona umuhimu wa kuwekeza katika afya na kueleza kuwa mfuko huo mfuko huo kwasasa unatoa huduma kwa wananchi wote kwa kuangalia kipato cha muhusika huku wakiwa na kauli yao kuwa “Tumekufikia, Jipimie”.
Ili kuongeza wigo wa wananchi katika mfumo wa bima ya afya, NHIF imeanzisha vifurushi vipya vya bima ya afya vyenye majina ya Najali Afya, Wekeza Afya, na Timiza Afya ambapo kwa kufanya hivyo mwananchi miongoni mwa huduma nyingine nyingi mwananchi anaweza kupata aina 27 za huduma za upasuaji mdogo na aina 14 za huduma za upasuaji mkubwa katika kifurushi cha Najali Afya ambacho ndio kifurushi cha chini kwa bei ya Shilingi 192,000 kwa mwaka.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com