METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, March 18, 2020

Katibu Mkuu Kilimo Gerald Kusaya aiagiza TPRI kufanya utafiti na kudhibiti viuatilifu feki

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya
Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia za unyunyiziaji viuatilifu(TPRI) Mhandisi Julius Mkenda (Kulia)akitoa maelezo kwa Katibu mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya ya matumizi ya mabomba na vinyunyizi.
Katibu Mkuu wizara ya Kilimo Ndg Gerald Kusaya akikagua mangala ya kuhifadhia nafaka ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula wakati akiwa katika ziara ya kikazi Jijini Arusha.

Na Innocent Natai, TPRI-Arusha

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya amekasirishwa na kitendo cha baadhi ya watendaji  wa Wizara hiyo kukaimu nafasi za watu kwa zaidi ya miezi sita bila sababu ya msingi suala linalowafanya washindwe kutekeleza majukumu yao kwa uhuru,Ufanisi mkubwa na kuweka malengo na mikakati yenye manufaa zaidi.

Kusaya ameyasema hayo katika ziara yake ya kuzitembelea taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Kilimo Mkoani Arusha,(Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Kudhibiti Visumbufu katika Ukanda wa Kitropiki (TPRI), Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ( CPB ) ziara yenye lengo la kufahamiana na watumishi na kupata taarifa za utendaji kazi wa Taasisi hizo.

Akizungumzia changamoto hiyo amesema kwa kipindi kifupi tangu awepo Wizara ya Kilimo ameshuhudia baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo wakiendelea kuitwa makaimu kwa muda mrefu bila sababu ya msingi.

“Jana kwenye baraza la wafanyakazi niliwaambia hili suala na leo nasema,mtu awekaimu kwa sababu ya kukaimu kwa muda mfupi eidha kwasababu mkuu wa taasisi ametoka na isizidi miezi sita na aikizidi huko kutakuwa sio kukaimu”Alisema Kusaya.

Aidha ameeongeza kuwa endapo anayekaimu anayosifa ya kuwa kwenye ile nafasi haitaji kuwa kwenye ile nafasi kwa muda mrefu aangaliwe kwa muda mfupi na endapo ataonekana anayosifa za kuwa kwenye nafasi ile basi apewe ile nafasi ili aendelee na majukumu yake na endapo anayekaimu hana sifa basi atafutwe mwenye sifa na kupewa ile nafasi.Ikiwa ni ili kuwaondolea hofu watendaji na kuwafanya wafanye maamuzi kwa kujiamini na waweze kuweka mipango madhubuti ya kuleta maendeleo.

Aidha Kusaya  ameridhishwa na kazi zinazofanywa na Taasisi hizo ikiwemo ya TPRI na kuwataka kuongeza juhudi za kufanya tafiti mbalimbali za visumbufu vya mazao na  mimea ili kuhakikisha wanawasaidia wakulima kujikwamua kiuchumi.


Pia amewataka wataalamu na wakaguzi kutoka Taasisi hiyo ya TPRI kuhakikisha wanatokomeza viuatilifu visivyo na ubora vinavyoingizwa hapa nchini kwa njia za panya,Sambamba na hilo ameahidi kushirikiana bega kwa bega na TPRI kuhakikisha wanaokutwa wanauza au kusambaza viuatilifu vilivyoisha muda wa matumizi,Visivyo na ubora(Bandia) wanapata adhabu itakayowafanya wajute kufanya biashara hizo.

Aidha pia Kusaya amewataka watendaji wa  Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA)  kanda ya Arusha kuzidi kutekeleza majukumu yao vyema ili kuhakikisha taifa linakuwa na hifadhi yakutosha ya chakula ili panapotokea changamoto ya uhaba wa chakula serikali iwezekutatua changamoto hiyo.

Aidha ameipongeza Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ( CPB )kutokana na jitihada watendaji wake wanazozionyesha za kuhakikisha wakulima wa Mikoa ya Kanda ya Kaskazini kuondokana na adha ya masoko ya kuuzia mazao yao hususani mahindi ili kutumia wanayoyatumia katika kiwanda cha CPB kilichoanza  uzalishaji hivi karibuni.

CPB ambayo zamani ilijulikana kama ‘Monaban’ imekuwa ikinunua mazao ya wakulima wa kanda ya Kaskazini na kuzalisha bidhaa mpya ya unga wa dona ijulikanayo kwa jina la ‘Dona bora’ unga unaopendwa ambapo pia utasaidia serikali kuongeza pato kupitia biashara wanazozifanya.

Ziara ya Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya inatarajiwa kuendelea kwa siku moja zaidi mkoani Arusha na baadae kwa siku moja Mkoani Kilimanjaro ambapo mkoani hapo atatembelea Bodi ya Kahawa 
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com