METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, February 15, 2020

SPIKA WA BUNGE MHESHIMIWA NDUGAI KUZINDUA PROGRAMU YA KULIOMBEA TAIFA


SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kesho anatarajiwa kuzindua Programu ya Kitaifa ya Kuliombea Taifa ambayo inalenga kumshirikisha Mungu vipaumbele na sera zinazotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano ili matokeo chanya yazidi kuonekana kila sekta.

Uzinduzi huo utafanyika jijini Dodoma katika Chuo cha Mipango ndani ya Ukumbi wa Mwalimu Nyerere kwa uratibu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania.

Hayo yameelezwa leo na Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania,Nabii Joshua Aram Mwantyala wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.

Amesema, Spika Ndugai atakuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa programu hiyo ambayo baada ya Jiji la Dodoma itaendelea katika majiji na mikoa mingine hapa nchini.

"Ndugu waandishi wa habari baada ya hapa Dodoma, Programu ya Kuliombea Taifa itaelekea mkoani Songwe, Singida, Mbeya, Tabora, Iringa, Shinyanga, Njombe,Simiyu, Ruvuma, Mara, Mtwara, Mwanza, Lindi, Kagera, Pwani, Geita, Tanga,Kigoma, Kilimanjaro, Katavi, Atrusha, Rukwa, Manyara, Zanzibar na Dar es Salaam.Tunaamini kupitia programu hii Mungu anaenda kutenda mambo makuu kwa Taifa letu na kila mmoja atashuhudia maendeleo na baraka kubwa,"amesema Nabii Joshua.

Nabii Joshua amesema, programu hiyo ya Kitaifa ni mpango endelevu wa huduma yake wa kuendelea kuunganisha Watanzania katika maombi na toba.

"Ndugu waandishi wa habari katika programu hii ya Kitaifa kwa ajili ya kuliombea Taifa, pia tutajikita zaidi kumuombea Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Joseph Magufuli na wasaidizi wake kuanzia ngazi za chini hadi juu ili Mungu azidi kuwapa moyo na nguvu za kuendelea kuwatumikia Watanzania.

"Viongozi wetu hawa mara nyingi wamekuwa wakikutana na majaribu mengi na hata kukatishwa tamaa kutokana na kazi nzuri ambazo wanafanya, lakini wengine wanaona kana kwamba hawafanyi chochote, jambo ambalo si sahihi hata kidogo.

"Kila mmoja wetu anatambua namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais Dkt.Magufuli alivyoibadili Tanzania kwa kipindi kifupi sana kuanzia kwenye mifumo ya uongozi, utekelezaji wa miradi ya maendeleo, uibua na uboreshaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kwa maslahi ya Taifa letu na mingine mingi. Hii ni hatua muhimu mno kwa Taifa letu, hivyo sisi watumishi wa Mungu kazi tuliyonayo ni kuhakikisha tunaendelea kuwaombea na kuwatia moyo kwa kazi nzuri wanazofanya,"amefafanua Nabii Joshua.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com