![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/796261e6-dd1c-44d1-b4cc-12bd16e1c45e.jpg)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi wakati alipowasili
kwenye uwanja wa ndege wa Lindi, Oktoba 8, 2019. Kushoto ni Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye
Ulemavu, Jenista Mhagama.
*************************
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amewasili wilayani Ruangwa, mkoani Lindi ili kushiriki
mbio za mwenge kitaifa hapo kesho. Mwenge huo umewasili mkoani humo leo.
Akizungumza
na viongozi wa kitaifa na kimkoa mara baada ya kuwasili mkoani humo,
Waziri Mkuu amesema kesho ataungana na wakazi wa Ruangwa kuupokea mwenge
huo. “Kesho nitaungana na wana Ruangwa ili kesho kutwa uendelee wilaya
ya Nachingwea,” amesema.
Waziri Mkuu
ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruangwa, amesema: “Nimeiona hamasa kubwa
waliyonayo wanaLindi huu ya mapokezi ya mwenge wa uhuru lakini kikubwa
zaidi ni ugeni mkubwa wa wageni akiwemo Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli.”
Amesema mbali
ya maadhimisho ya kumaliza mbio za mwenge nchi nzima, mwaka huu
Tanzania inaadhimisha kumbukumbu ya miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa.
“Tuendelee
kuwahamasisha wanaLindi na Watanzania wote washiriki kwenye makongamano
yanayofanyika nchini kote. Kumbukumbu ya Baba wa Taifa isaidie
kuelimisha vijana wetu ambao hawajui historia ya kazi za waasisi wa
Taifa letu.”
“Pia walioko
madarakani, watumie fursa hii. Waige na kuenzi kazi za viongozi kama
Mwalimu Nyerere na pia wajenge tabia ya kujua tabia ya ulipotoka, na
mahali ulipo.”
Mapema,
akitoa taarifa ya maandalizi ya kilele cha mbio za mwenge kwa Waziri
Mkuu, Waziri wa Nchi OWM – Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na
Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema mbio hizo zilianza Aprili 2,
mwaka huu na leo zimeingia Lindi ambao ni mkoa wa 31.
Alisema hadi
kufikia tarehe 14, ambayo ni siku ya kilele utakuwa umepita katika
Halmashauri 195 za nchi mzima. “Katika kipindi hicho chote, vijana wetu
sita ambao ni wakimbiza mwenge, walizindua miradi ambayo wameridhika
nayo na ile yenye dosari, hawakusita kuikemea,” alisema.
Alisema
makongamano mbalimbali yameandaliwa ili kuenzi kifo cha Baba wa Taifa
ambaye Oktoba 14, atatimiza miaka 20. Pia vijana 88 ambao walipanda
mlima Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu hizo watashiriki sherehe
hizo mjini Lndi.
0 comments:
Post a Comment