METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, February 6, 2020

RC MTAKA AWAPONGEZA WALIMU NA WANAFUNZI UFAULI ELIMU YA MSINGI NA SEKONDARI MKOANI SIMIYU

Na Mathias Canal, WazoHuru Blog

Uongozi wa Mkoa wa Simiyu umewapongeza walimu kwa kufaulisha vizuri na kuufanya mkoa huo kuingia katika mikoa 10 bora katika mitihani yote ya kitaifa ngazi ya Msingi na Sekondari, kadhalika uongozi wa mkoa huo umemzawadia mwanafunzi aliyepata ufaulu wa daraja la kwanza Pointi saba-Yohana Lameck Lugedenga kiasi cha Tsh Milioni 1 ambapo Mameneja wa Bank ya CRDB Tanzania-wamemzawadia kijana huyo Hundi yenye thamani ya Tsh Milioni 2.2

Akizungumza na mtandao wa WazoHuru Blog Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka amesema kuwa Kwenye mitihani ya darasa la saba, wanafunzi wanne wa mkoa wa Simiyu waliingia kumi bora kitaifa kwa shule za serikali, kila mwanafunzi amepatiwa laki 3, huku kwa upande wa walimu wote ambao wanafunzi wao walipata Alama A kwenye masomo yao kidato cha nne, kila alama A ya kidato cha nne Mwalimu amepata Tsh 30,000.

Shule ya msingi ya Mwaukoli-Meatu iliingia 10 bora kitaifa kwa shule za serikali-imezawadiwa kiasi cha Tsh Milioni 2, shule 3 za msingi zilizoongeza ufaulu kwa miaka 3 mfululizo kila shule imewazawadiwa kiasi chaTsh laki 5.

Mtaka amesema kuwa Shule 3 za msingi zilizoongoza kwa kuwa alama A nyingi katika kila somo zimepata zawadi za fedha, Mhe Mtaka amezipongeza Halmashauri zote kwa kutenga fedha za motisha za elimu kwa walimu wote wa msingi na sekondari, kadhalika amewapongeza wadau wote wa mkoa wa Simiyu, Bank za CRDB, NMB, na TPB kwa mchango wao mkubwa katika kambi za kitaaluma mkoani Simiyu.

"Zaidi ya yote tumekubaliana walimu wetu wote ndani ya Mkoa kupewa kipaumbele cha kwanza wanapokwenda kwenye ofisi au taasisi za umma kupata huduma katika mantiki ya kwamba, Mwalimu anapokaa kwenye foleni kusubiri huduma, mamia ya wanafunzi wake darasani wana athirika kwa kupoteza kipindi kwa siku hiyo" Alikaririwa Mhe Mtaka

Rc Mtaka ameagiza mahala popote ambapo ofisi ya serikali inahusika (Hospitali, Ofisi za Halmashauri na maeneo mengine ya umma) Mwalimu akifika akajitambulisha kwa kitambulisho chake basi ahudumiwe haraka ili aweze kurejea kwenye kituo chake cha kazi mapema. "Rumeyashauri Mabenki pia yaje na namna bora ya kuwasaidia mikopo midogo walimu ambao hawakopesheki baada ya kufikia ukomo wa kukopa kwa sheria ya BOT" Alisema Mhe Mtaka

Ameongeza kuwa ili kuwaondoa kwenye kadhia ya kukopeshwa na watu au taasisi binafsi ambazo zimegeuka kuwa mwiba kwa walimu kutokana na riba kubwa hali inayosababisha baadhi ya walimu kushuka morali ya kufundisha na wengine kukwepa kwenda vituoni pao pa kazi kwa kuogopa kudaiwa, uongozi wa mkoa huo umewahakikishia walimu kuendelea kuwalinda na kutunza utu na heshima yao.

Rc Mtaka amewaomba viongozi wenzake ndani ya mkoa kujiepusha na lugha au kauli za kuwakatisha tamaa, kejeli au vitisho. Sambamba na hayo Mhe Mtaka amewapongeza wazazi, walezi, sekta binafsi, viongozi wa dini, viongozi wa kisiasa, watumishi, walimu na wanafunzi kuibeba ajenda ya elimu kama kipaumbele cha kwanza.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com