METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, February 12, 2020

NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE OMARY MGUMBA AANZA ZIARA YA KIKAZI NCHINI KENYA

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe Omary Mgumba (Mb) amewasili Jijini Mombasa nchini Kenya Kenya ambapo atashiriki vikao vya  wadau wa Tasnia ya kahawa Duniani vinavyofanyika kwa siku nne mfululizo kuanzia tarehe 11/02/2020 hadi 14/02/2020.

Jana, tarehe 11/02/2020, Mhe Mgumba ameshiriki katika Mdahalo Maalumu uliondaliwa na Taasisi ya Kimataifa ya MARKUP kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Umoja wa Nchi za Afrika Mashariki (EAC). 

Mdahalo huo uliongozwa na Bw. Peter Mathuki, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya EABC na kuhusisha viongozi mbalimbali kama vile; Waziri kutoka Ofisi ya Rais ya nchi Burundi inayohusiana na masuala ya mahusiano ya Afrika Mashariki, Bi. Isabelle Ndahayo; Mwakilishi wa nchi ya Rwanda nchini Kenya, Bw. Richard Masozera; Mkurugenzi wa Kitengo cha masuala ya Uhamiaji na Viwanda katika EAC, Bw. Kenneth Bagamuhunda; Mkurugenzi Mkuu wa Shirikisho la wafanyabiashara wa kahawa wa Kenya, Bi. Faith Karimi; Mkurugenzi wa Mipango kutoka Shirika la kimataifa la GIZ na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Africa Coffee Academy. 

Mkutano huo wa siku nne unahusisha washiriki zaidi ya 600 ambao ni wakulima wa kahawa, wanunuzi wa kahawa, wachakataji wa kahawa, wasafirishaji pamoja na wadau mbalimbali waliopo katika tasnia ya kahawa duniani kutoka nchi zaidi ya 30 duniani, Kauli mbiu yake ni “Kuondoa vizuizi vya kibiashara katika Umoja wa Nchi za Afrika Mashariki ili kuongeza uuzaji wa kahawa nje ya nchi"

Majadiliano ya Mkutano huo yamelenga kuhakikisha vizuizi vyote vya kibiashara katika tasnia ya kahawa katika nchi za Afrika Mashariki vinaainishwa na kutengenezewa Mikakati madhubuti ya kuvipunguza ili kuhakikisha kahawa zinazozalishwa katika nchi za Afrika Mashariki zinapata masoko ya uhakika katika mabara ya Ulaya, Asia, Amerika n.k.

Katika mkutano huo Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mgumba, amezungumzia Mikakati mbalimbali iliyoanzishwa na kutekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuhakikisha wakulima wa kahawa pamoja na wadau wote waliopo katika mnyororo wa thamani katika tasnia ya kahawa wananufaika na biashara ya kahawa nchini Tanzania sanjari na nje ya nchi. 

Mgumba alisema kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Kilimo inakamilisha zoezi la kuhakiki wakulima wote wakiwemo wa zao la kahawa ili kuwa na taarifa sahihi za wakulima zitakazosaidia kuandaa Mipango na Mikakati ya kuwasaidia wakulima wote nchini. 

Pia, amesema kuwa, Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi na Taasisi ya TaCRI inayojihusha na kufanya tafiti za sekta ya kilimo zikihusisha zao la kahawa zinaendelea kuwasaidia wakulima wa kahawa namna ya kuongeza uzalishaji, tija, matumizi bora ya pembejeo ili kuhakikisha uzalishaji unafikia viwango vinavyohitajika na walaji duniani kote. 

Vilevile, amesema Tanzania inaanda Sera ya Kilimo ili kuwa na Sera inayoakisi hali ya sasa ya kilimo nchini Tanzania na itakayosaidia kuandaa Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali itakayosaidia kuimarisha usimamizi wa Sekta ya Kilimo ikihusisha tasnia ya kahawa; uhamasishaji wa kilimo cha Mkataba kwa wakulima na wanunuzi ili kuhakikisha uwepo wa masoko ya mazao; upunguzaji wa Ushuru na Tozo mbalimbali katika Sekta ya kilimo nchini, uwepo wa uuzaji wa moja kwa moja wa kahawa kwa wanunuzi (direct selling) pamoja na uanzishaji wa Kanda nne za uuzaji wa zao la kahawa (Kanda ya Ziwa, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Magharibi na Kanda ya Kaskazini) ili kupunguza gharama za usafirishaji wa kahawa kwa wakulima na wanunuzi pia. 

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com