Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Mohamed
Aboud Mohamed akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu Mkutano wa kwanza wa
Kamati ya Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya Menejimenti ya Maafa kwa
Nchi Wanachama Jumuiya ya MaendeIeo Kusini mwa Afrika, tarehe 16
Februari, 2020, Ukumbi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) Mnazi mmoja.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa,
Zanzibar, Makame Khatibu Makame akitoa Ufafanuzi kwa Waandishi wa Habari kuhusu
masuala ya menejimenti ya maafa kuhusu Mkutano wa kwanza wa Kamati ya
Mawaziri wenye dhamana ya menejimenti ya Maafa kwa Nchi wanachama wa Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrikatarehe 16 Februari, 2020, Ukumbi wa Shirika la
Utangazaji Zanzibar (ZBC) Mnazi mmoja.
Baadhi ya waandishi wa Habari wakifuatilia Mkutano wa
Waandishi wa Habari na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mhe.
Mohamed Aboud Mohamed (hayupo pichani) wakati wa akifafanua kuhusu Mkutano
wa kwanza wa Kamati ya Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya Menejimenti
ya Maafa kwa Nchi Wanachama Jumuiya ya MaendeIeo Kusini mwa Afrika,
tarehe 16 Februari 2020, Ukumbi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) Mnazi
mmoja.
Kama tunavyoeelewa kuwa kufuatia Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), uliofanyika mwezi Agosti 2019
ambapo, Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania alipokea rasmi uenyekiti wa jumuiya hiyo, hali hiyo imepelekea
mkutano mbalimbali ya Kisekta kufanyika hapa Tanzania.
Mkutano huu unafanyika kutokana na umuhimu mkubwa wa
Mawaziri wa nchi wanachama wa SADC wanaohusika na masuala ya maafa kukutana kwa
lengo la kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya namna bora ya kukabiliana na
matukio ya maafa yanayoukabili ukanda huu yakiwemo vimbunga,
mafuriko, ukame, na hata ajali za baharini ambayo yamekuwa yakisababisha athari
kubwa kwa maisha ya watu na mali.
Sote ni mashuhuda athari za Kimbunga Idai na Keneth
vilivyotokea katika nchi za Madagascar, Malawi, Msumbiji na Zimbabwe
vilipelekea vifo vya maelefu ya watu na wengine kutoonekana kabisa na
kupelekea mahitaji ya kiasi cha dola bilioni 10 za Kimarekani kwa
ajili ya kurejesha hali.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano
wa Kwanza wa Kamati ya Mawaziri wanaohusika na Menejimenti ya Maafa kwa Nchi
Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika utakaofanyika katika hoteli
ya Madinat Al Bahri Mbweni, tarehe 18 – 21 Februari, 2020, hapa
Zanzibar. ambapo Kaulimbiu ya Mkutano huu: “Ushiriki wa Kisekta kwenye
Kupunguza madhara ya maafa ni njia bora ya kujenga uhimili katika ukanda wa
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika” (SADC)
Mkutano huu unakuja kipindi ambacho nchi nyingi wanachama
katika ukanda huu zimekuwa zikiathiriwa na majanga ya asili mara kwa mara na
kusababisha madhara makubwa. Hali iliyoonesha wazi umuhimu wa mashirikiano
ya kikanda katika kukabiliana na maafa ili kupunguza athari za
maafa, kukuza uwezo wa kujiandaa na kukabiliana kwani mara nyingi
athari zinazotokana na majanga ya kimaumbile yakiwemo ukame, mafuriko, maradhi
ya mlipuko na mengineyo, hupelekea vifo kuharibu miundombinu muhimu ikiwemo
barabara na hudumaza msingi za jamii kama vile afya na elimu na kupelekea
gharama kubwa katika kurejesha hali baada ya maafa kutokea.
Katika hatua ya kujenga mataifa yenye uhimili katika
kukabiliana na maafa, SADC imefanikiwa katika kuimarisha mifumo ya tahadhari za
mapema inayoendana na majanga ya Hali ya hewa, kuandaa vikao vya mwaka
kwa nchi wananchama kwa ajili ya kujikinga, kujiandaa na
kukabiliana na maafa pamoja na kuandaa mipango ya dharura na kutoa mafunzo
ya utafutaji na uokozi kwa majanga ya baharini kwa nchi wananchama.
SADC imetekeleza program ufanyaji wa tathmini na uchambuzi
wa usalama wa chakula kwa nchi wananchama 14 zilizoathiriwa na majanga
yanayoendana na hali ya hewa yakiwemo ukame, imeandaa mpango na mkakati wa
pamoja kwa ajili ya kujikinga na kukabili maafa. Mikakati yote hiyo ni kwa
ajili ya kupunguza athari za maafa katika kanda hii. Mnamo mwaka 2017-2018
takribani watu wapatao milioni 7 waliathiriwa na maafa idadi ambayo ni ndogo
ikilinganishwa na watu milioni 17 walioathirika katika miaka ya 2015-2016.
Kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imekamilisha
kuandaa nyaraka zote muhimu katika masuala ya kukabiliana na maafa ikiwemo
sheria ya Usimamizi wa Maafa ya Kitaifa Na. 7 ya 2015, Sheria ya
Kukabiliana na Maafa Zanzibar No. 1 ya mwaka 2015, Sera za Kukabiliana na
Maafa, Mipango ya Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa na Mkakati wa Mawasiliano
Wakati wa Maafa na rasimu ya Mkakati wa Kukabiliana na Maafa pamoja kuanzisha
vituo vya mawasiliano na operesheni za dharura na vituo vya uokozi hasa kwa
majanga ya baharini.
Mkutano huu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
unalenga katika kushajihisha juhudi zilizopo katika kukabiliana na maafa kwa
kuziwezesha nchi wanachama kuandaa mikakati ya uhimili kutokana na athari za
maafa, kuandaa mkakati wa kujiandaa na kukabiliana na maafa. Aidha, mikakati
hii itaisaidia sana juhudi za ukanda huu katika kupunguza athari za maafa na
kuimarisha uwezo wa nchi husika katika kukabiliana na maafa pamoja na kurejesha
hali baada ya maafa kutokea.
Nachukua fursa hii kuwakaribisha waandishi wa habari na
wananchi kwa ujumla kufuatilia juu ya Mkutano huu ambao utakuwa ni fursa tosha
ya kutangaza utalii wetu na kukuza uchumi wan chi pamoja na kupunguza athari za
maafa.
0 comments:
Post a Comment