Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma tarehe 5 Januari 2020
Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga akisisitiza jambo kuhusiana na kufutwa kwa vyama vyao ushirika ambavyo vimekwenda kinyuma na taratibu, miongozo ya kanuni na sheria ya vyama hivyo. Waziri Hasunga ametoa tamko hilo tarehe 5 Januari 2020 jijini Dodoma kwenye mkutano wake na wandishi wa habari.
Wandishi wa habari wakifuatilia mkutano wao na Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga jijini Dodoma tarehe 5 Januari 2020
Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Dk Benson Ndiegi akizungumza na wandishi wa habari kwenye mkutano wa Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga tarehe 5 Januari 2020 jijini Dodoma.
SERIKALI inakusudia kuvifuta vyama vya ushirika vipatavyo 3,436 ambavyo vimeshindwa kutekeleza majukumu yake ya msingi na havipatikani huku vingine vikiwa havijulikani vilipo.
Kwa kuzingatia matakwa ya sheria no 6 ya mwaka 2013 ya vyama vya ushirika kifungu 100 na kanuni ya 26, Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga amemuagiza Mrajisi wa vyama hivyo kutoa notisi ya siku 90 kwenye gazeti la serikali ya kusudio la kuvifuta.
Akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma tarehe 5 Januari 2020, Mhe Hasunga amesema asilimia kubwa ya vyama vilivyokusudiwa kufutwa ni vyama vya ushirika wa akiba na mikopo ambavyo ni asilimia 73.8.
Amesema vyama hivyo vingi ni matokeo ya mfumo wa uwezeshaji wa wananchi kiuchumi ujulikanao kama Jakaya Kikwete Fund ambao ulilenga kuwawezesha wananchi kiuchumi.
" Katika mpango huu wa JK Fund wananchi wengi walianzisha SACCOS kwa lengo la kupata mikopo kutoka kwenye mfuko huo, Aidha vyama ambavyo havikupata mkopo havikuendelea na majukumu yake na hata vilivyopata mikopo baada ya kupata walitelekeza vyama hivyo jambo linalopelekea kuwa na SACCOS nyingi hewa," Amesema Mhe Hasunga.
Amevitaka vyama ambavyo orodha yake itapatikana kwenye tangazo la mrajisi litakalotolewa kwenye gazeti la serikali, mtandao wa wizara ya kilimo na mtandao wa Tume ya Ushirika kujitokeza na kutoa sababu za kwanini wasifutwe kwenye orodha ya vyama vya ushirika.
" Tunavitaka vyama vyote vya ushirika nchini kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo. Vyama vyote vinatakiwa kuwahudumia wanachama wake na siyo vinginevyo," Amesema Mhe Hasunga.
Mhe Waziri amesema mpaka sasa daftari la mrajisi wa vyama vya ushirika lina jumla ya vyama 11,149 vilivyoandikishwa kati ya vyama hivyo, 3,436 havijulikani vilipo, vyama 1,250 vimesinzia na vyama 6,463 vipo hai.
Amesema sababu zinazopelekea kufutwa kwa vyama hivyo ni kushindwa kuwa na ofisi huku viongozi wake wakiwa hawajulikani, Chama kushindwa kufanya shughuli zake ndani ya miezi sita tangu kiandikishwe pamoja na idadi ya wanachama kupungua kwa mujibu wa mahitaji ya kisheria.
Sababu nyingine ni vyama hivyo kushindwa kutekeleza takwa la kisheria la kutayarisha makisio ya mapato na matumizi na kuyapeleka kwa mrajisi kuyapitisha, kutayarisha taarifa ya mwaka, kufunga mahesabu na kuyapeleka COASCO kwa ukaguzi, kutofanya mikutano ya mwaka ya wanachama na bodi zao.
Katika orodha ya vyama vya ushirika kimkoa vinavyokusudiwa kufutwa kwenye daftari la mrajisi wa vyama, Mkoa wa Mwanza unaongoza ukiwa na jumla ya vyama 393, Pwani ya pili yenye vyama 335 huku Kagera ikishika nafasi ya tatu kwa vyama 301.
Kwa upande wake Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, Dk Benson Ndiegi amesema serikali haitowavumilia viongozi wa vyama ambavyo vitakaidi maagizo hayo yaliyotolewa na Mhe Waziri.
" Baada ya agizo hili la Mhe Waziri na baada ya kutoa notisi hizo kwenye gazeti la serikali tutakua tayari kupokea maelezo na taarifa kutoka kwenye vyama na wale ambao watakua wanafutwa waje na wanaamini wana nafasi ya kuendelea kuwepo inabidi waje na vielelezo vyao," Amesema Dk Ndiegi
0 comments:
Post a Comment