Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) George Simbachawene amesema Serikali imefanya
mapitio ya Sera ya Mazingira ya mwaka 1997 ili kuzingatia changamoto mpya za
kimazingira zinazojitokeza mara kwa mara.
Akiwasilisha taarifa ya
Utekelezaji wa Majukumu na Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Baraza la Taifa
la Hifadhi na Usimazi wa Mazingira (NEMC) kwa kipindi cha Julai – Desemba 2019
mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira amesema Ofisi
imeendelea kuratibu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 1997
pamoja na Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004.
Simbachawene amesema Rasimu ya
Mwongozo wa mita 60 katika kuhifadhi vyanzo vya maji katika bahari, maziwa na
mito imeandaliwa; Rasimu ya Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2020 imeandaliwa
na ipo katika hatua ya kuwasilishwa katika vyombo vya maamuzi; na Itifaki ya
SADC ya Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo Endelevu iliridhiwa na Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Rasimu ya Mwongozo wa Uwekezaji
katika usimamizi wa Taka imeandaliwa; Kanuni za Usumamizi wa Taka za
kielekroniki za mwaka 2019 zimeandaliwa; Kanuni za Usimamizi wa Taka hatarishi
za mwaka 2009 zimepitiwa na Mwongozo
wa Kitaifa wa kufanya tathmini ufuatiliaji na utoaji taarifa za hewa ukaa umeandaliwa”
Simbachene alisisitiza.
Awali, Katibu Mkuu wa Ofisi ya
Makamu wa Rais Mhandisi Joseph Malongo amesema Ofisi hiyo inatarajia kuandaa
mkutano mkubwa utakaowakutanisha viongozi kutoka Serikali Kuu na Mamlaka za
Serikali za Mitaa kuzungumzia agenda ya Mazingira ikiwa ni pamoja na kuhamasisha
wananchi kushiriki katika shughuli za utunzaji wa mazingira nchini.
Kwa upande mwingine Mkurugenzi
Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel
Gwamaka amesema Baraza linaendelea na Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria ya Mazingira
kwa kufanya Kaguzi za Mazingira.
“Baraza limefanya ukaguzi katika miradi 870 ili kuhakikisha uzingatiaji wa
Sheria ya Mazingira nchini. Vilevile. Kaguzi hizo zilifanyika katika shughuli
za kiuchumi na kijamii zenye kuweza kuleta athari kwa mazingira” Gwamaka
alisisitiza.
Kuhusu
Udhibiti wa Taka Hatarishi, Baraza kwa kushirikiana na
mamlaka nyingine za Serikali lilishiriki katika zoezi la ukaguzi wa makontena 151 ya chuma chakavu yaliyokuwa yanatakiwa
kusafirishwa nje ya nchi ikiwa ni kujua uhalali wa kuendesha biashara hiyo na
kukagua shehena ya makontena hayo ili kubaini aina ya chuma chakavu kilichopo
ndani ya makontena. Aidha, hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa
Mazingira ya mwaka 2004 ikiwemo kutozwa faini, zilichuliwa dhidi ya Makampuni
yaliyokaguliwa na kukutwa na makosa.
Dkt.
Gwamaka amesema kuwa Baraza limesajili jumla ya Miradi
664 (Miradi 387 ya Tathmini za Athari kwa Mazingira na Miradi 277 ya kufanyiwa
Ukaguzi wa Athari za Mazingira) ikiwa ni asilimia 55 ya miradi ambayo
imekusudiwa kufanyiwa mapitio.
“kwa kipindi
cha mwaka wa fedha 2019/20. Kwa kipindi hicho miradi ipatayo 375 imeidhinishwa
kupata vyeti, hii ikiwa miradi 225 kwa ajili ya Tathmini za Athari kwa
Mazingira (Environmental Impact
Assessment) na Miradi 150 Kwa ajili ya Ukaguzi wa Athari za Mazingira (Environmental Audit). Aidha miradi
mingine ipo katika hatua tofauti za upembuzi.
Mbunge wa
Babati Vijijini Mhe. Jitu Vrajlal Son ameshauri Serikali kuongeza kasi ya
utoaji wa elimu ya mazingira katika ngazi zote za Serikali na kuhimiza
uanzishaji wa Mfuko wa mazingira nchini.
0 comments:
Post a Comment