Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa walipotembelea katika daraja lililokata mawasiliano kati ya Mkoa wa Rukwa na Katavi katika kijiji cha Muze Wilayani Sumbawanga.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiwa na kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wakizungumza na vijana waliojitolea kujaza kifusi katika moja ya madaraja yaliyosombwa na mafuriko katika kijiji cha Lwanji bonde la Ziwa Rukwa, Wilayani Sumbawanga.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa hela ya soda kwa vijana waliojitolea kujaza kifusi katika daraja lililokatika la mto Lwanji katika Kijiji cha Lwanji kwa juhudi zao za kuwawezesha wananchi wanaotumia daraja hilo kuwezea kuendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
………………
Mvua zinazoendelea kunyesha katika mkoa wa Rukwa zimeendelea kusababisha maafa baada ya kusomba madaraja manne katika barabara ya Kasansa – Kilyamatundu inayounganisha mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi iliyopo bonde la ziwa Rukwa Wilayani Sumbawanga huku ikisababisha vifo vya watu watatu katika wilaya ya Kalambo na Nkasi mkoani humo.
Mvua hizo zilizosomba madaraja katika vijiji vya Muze, Kifinga, Lwanji na Msia vilivyopo Wilaya ya Sumbawanga imesababisha kukatika kwa mawasiliano baina ya kata na kata, kijiji na kijiji pamoja na mikoa hali iliyoleta taharuki kwa wananchi wanaoishi katika bonde hilo lenye kata 13 na wakulima wengi wa mpunga wanaosafirisha bidhaa zao katika mikoa ya jirani.
Aidha, Mvua hizo zimesababisha vifo vya Mama mjamzito na mwanawe kwa kusombwa na maji yam to Kalambo huko wilayani Kalambo na kifo cha mwanafuzi wa darasa la 4 mwenye umri wa miaka 12 katika Wilaya ya Nkasi ambae pia alisombwa na maji wakati akitoka shuleni kurudi nyumbani.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alipofanya ziara ya kutembelea maeneo yaliyokumbwa na maafa hayo na hivyo kuwatahadharisha wananchi kuacha tabia ya kulazimisha kupita katika njia ya maji pindi wanapoona mvua ni kubwa na hivyo kuwataka kusubiri mvua ipungue ndipo waendelee na shughuli zao.
“Mimi niwaombe ndugu zangu hasa kinamama na watoto, mnapoona mvua zimekuwa nyingi maji yanaweza yakajaa wakati wowote, jihadharini msipite, acheni maji yapungue halafu mpite, lakini msiwe wabishi, mkiwa wabishi mtabebwa na mafuriko, hasa watoto wadogo hawalelewi kitu wanadhani maji kama hivi anaona kama yametulia anasema mimi nitapita tu, kwahiyo waambieni watoto nyumbani wachukue tahadhari, mkiona kuna mvua kuna mafuriko watoto wasiende kwenye shughuli zao muwazuie kuokoa maisha yao” Alisisitiza
Na kuongeza kuwa hali hiyo si ya kudumu ni ya muda tu kwani serikali kupitia wakala wa barabara nchini TANROADS inaendelea na matengenezo ya dharura katika maeneo hayo ili kurudisha hali ya mawasiliano baina ya vijiji, kata pamoja na mikoa ili wananchi waendelee na shughuli zao za kila na hivyo kuwataka wakala hao kuweka kambi katika maeneo yaliyoharibiwa na mvua.
“Bonde la ziwa rukwa limeshakatika kimawasiliano kabisa kwasababu magari yanayotokea Mbeya, kule Somgwe kupitia daraja letu la Kilyamatundu pale hawawezi kufika Muze mpaka huko Katavi kama hapa hapatakuwa pameshughulikiwa kwahiyo weka nguvu kubwa sana Meneja wa TANROADS hapa ili kuhakikisha wananchi wetu wanapata usafiri wao wa kawaida ndani ya muda mfupi,”Alisema.
Kwa upande wake Meneja wa TANROADS mkoa wa Rukwa Mhandisi Masuka Mkina amesema kuwa tayari wamekwisha omba fedha za matengenezo ya dharura kutoka makao makuu na kuwataka wananchi kuacha tabia ya kufanya shughuli za kibinaadamu katika kingo za mito ili kuweza kuokoa miundombinu hiyo kuharibiwa na mafuriko.
“Nichukue nafasi hii kuwaomba viongozi wa vijiji na wengine watusaidie kwasababu sheria ya mazingira inasema wasifanye kazi karibu na mito na panapotukwamisha ni huko juu ambapo watu wanalima wanaharibu mazingira kwahiyo maji yanakuja kwa nguvu matokeo yake yanasomba miundombinu yetu na kutuacha kama hivi tukiwa wakiwa kabisa,” alisema
Kwa upande wao wananchi katika maeneo hayo waliiomba serikali kuharakisha matengenezo ya haraka kwani atahri wanayoipata ni kubwa katika upande wa kiuchumi na kijamii, miongoni mwa wananchi Erasmus Muhagama alisema, “Mi naiomba serikali iharakishe hili zoezi maana mawasiliano ndio yameshakatika”.
Nae Magdalena Tangi alisema, “Kwakweli kuna shida watu hawapiti safari zimekuwa ngumu, usafiri umekuwa wa pikipiki gharama kubwa kwahiyo wananchi tunapata shida sana kama hivi mlivyoona barabara zimekatika toka Muze mpaka hapa Msia sijui huko mbele sasa”.
Barabara hiyo Kasansa – Kilyamatundu yenye urefu wa kilomita 178 iliyopo kwenye bonde la ziwa Rukwa lenye kata 13 ni kiungo muhimu sana kwa kuunganisha mkoa wa Rukwa na mikoa ya Songwe na Katavi hasa katika shughuli za kiuchumi kwani asilimia kubwa ya wakazi wa bonde hilo ni wakulima wa mpunga, mahindi, alizeti pamoja na kufanya ufugaji.
0 comments:
Post a Comment