Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akioneshwa namna maziwa yanavyo
poozwa katika makonteni maalum baada ya kuchemshwa ili kutengeneza mtindi
katika kiwanda cha kuchakata maziwa cha Mather Dairies kilichopo Ikwiriri
Wilaya ya Rufiji mkoa wa pwani alipotembela kukagua kiwandani hapo Januari 23,
2020. Anayetoa maelezo hayo ni Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho Mzee
Abdallah Nyarando. (PICHA ZOTE NA OFISI YA
WAZIRI MKUU)
Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akiangalia moja ya pakiti iliyo
na bacteria maalum wanaotumika kuchachusha na kugandisha maziwa ili kutengeneza
maziwa mtindi katika kiwanda hicho.
Mkurugenzi Mtendaji wa
Kiwanda cha Kuchakata maziwa cha Mather Dairies Mzee Abdallah Nyarando akitoa
maelezo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah
Kairuki kuhusu mtambo wa kupooza maziwa akiwa kiwandani hapo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akiteta jambo na Mkurugenzi
Mtendaji wa Kiwanda cha Kuchakata maziwa cha Mather Dairies Mzee Abdallah
Nyarando pamoja na mke wake wakati wa ziara yake kiwandani hapo.
NA. MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji nchini Mhe. Angellah Kairuki
amewaasa wananchi kuthubutu uwekezaji katika maeneo yenye tija kwa kuzitumia
fursa za uwekezaji zilizopo ili kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo yao
na nchi kwa ujumla.
Ametoa kauli hiyo tarehe 23
Januari, 2020 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika kiwanda cha
kuchakata maziwa ya mtindi cha Mather Dairies kilichopo Kijiji cha Ikwiriri
Wilaya ya Rufiji katika Mkoa wa Pwani alipotembelea kiwandani hapo ikiwa ni
eneo la mwisho kutembelea katika ziara yake ya siku 6 Mkoa wa Pwani.
Akiwa katika kiwanda hicho
kilichowekeza mtaji wa zaidi ya milioni 300 chenye uwezo wa kuchakata zaidi ya
lita 2000 kwa siku ambazo hutengeneza maziwa ya mtindi aina ya Yogurt Full
Manyonyo, waziri alitoa hamasa hiyo kwa Watanzania kuzichangamkia fursa na
kuwatoa shaka kuwa hakuna Mwananchi asiyeweza kuwekeza kikubwa ni kuwa na nia
na uthubutu.
“Ni ukweli kuwa, kila uwekezaji
Mtanzania anaweza kuufanya muhimu kuwa na ujuzi, teknolojia pamoja na mtaji
pasipo kutia shaka na kujiamini,”alifafanua Waziri Kairuki
Aliongezea kuwa, ikiwa uwezo wa
kuwekeza ni mdogo kwa kuzingatia ukosefu wa ujuzi wananchi wanapaswa kutumia
fursa za mafunzo ya ukuzaji ujuzi unaotolewa katika vyuo mbalimbali na kutumia
watu wenye uzoefu inapofaa kulingana na aina ya uwekezaji unaotaka kuufanya.
Aliwaasa watanzania kuacha tabia
ya kukatishana tamaa na kuona namna ya kushikamana kuweza kuwekeza katika sekta
mbalimbali.
“Kumekuwa na tabia ya
kukatishana tamaa pindi mtu anapothubutu kuona fursa na kuichangamkia, ni rai
yangu kwa wananchi kuona watanzania tunawekeza kufanya mambo makubwa katika
maeneo yote yenye fursa, na kuzitumia vyema mamlaka zilizopo kwa kupata msaada
ya ushauri elekezi na miongozo ya namna bora ya kuwekeza,”alifafanua
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
Kiwanda hicho Mzee Abdallah Nyarando alieleza namna alivyoanza uwekezaji wake
mwaka 2010 kwa mtaji wa shilingi milioni 20 na hadi kukamilika kwa kiwanda
hicho ametumia jumla ya shilingi Milioni 300, na kuweza lengo ni kuongeza
thamani ya maziwa, kuzalisha ajira na kujipatia kipato.
“Kiwanda hiki kimeweza
kusaidia zaidi ya vijana 12 ambao wamekuwa wa msaada katika kuzalisha na kuuza
maziwa maeneo mablimbali nchini ikiwemo; Masasi, Kibiti, Rufiji, Mtwara na Dar
es Salaam,”alisema Mzee Nyarando.
Alitoa wito kwa wananchi
kuondokana na hofu za kuwekeza katika maeneo mbalimbali na kueleza zipo faidi
za kuwekeza katika nchi yao na kujipatia kipato ili kujikwamua kiuchumi.
Akiwasilisha taarifa yake kwa
Waziri Kairuki Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Mhe. Juma Njwayo alieleza kuwa Tanzania
ina fursa nyingi za kusaidia kundi kubwa la vijana katika kujikwamua kiuchumi
kwa kuangalia maeneo muhimu ya uwekezaji katika Nyanja mbalimbali.
Aliongezea kuwa, wananchi hawana
budi kujiajiri kwa kutumia nguvu kazi walizonazo na kuzichangamkia fursa za
Wilaya yake ambazo alizibaini ni pamoja na shughuli za kilimo, ufugaji, uvuvi
na biashara na kuwataka kuzitumia kwa kuzingatia uwepo wa miundombinu muhimu ya
kuvutia uwekezaji.
“Wilaya yetu ina vivutio vingi
ikiwemo ardhi inayokubali mazao mbalimbali kama mahindi, mpunga, korosho, mazao
jamii ya mikunde na mbogamboga na matunda aina ya matikiti hivyo
zitumieni kwa tija na kuhakikisha tunaondokana na ukosefu wa ajira,”alieleza
Juma
Alitumia fursa hiyo kutoa rai
kwa wawekezaji kuona maeneo yenye rutuba na kuwekeza katika mazao hayo na
kubainisha fursa zilizopo katika ufugaji kwa kuzingatia uwepo wa mabwawa ya
asili maji katika wilaya hiyo.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment