Baadhi ya miundombinu iliyojengwa
na Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) katika shule ya msingi
Buhangija iliyopo mkoani Shinyanga.
Darasa lililojumuisha watoto wenye mahitaji maalum na wale wa kawaida katika shule ya msingi Buhangija
Mtoto mwenye ulemavu wa kutokuona
akitumia kifaa maalum kwa ajili ya kuandikia katika shule ya msingi
Buhangija. Kifaa hicho ni moja ya vifaa vilivyonunuliwa kwa ajili ya
watoto wenye mahitaji maalum katika shule hiyo.
……………….
Serikali kupitia Mpango wa Lipa
Kulingana na Matokeo (EP4R) imetumia kiasi cha shilingi milioni 286.6
kwa ajili ya kukarabati na kujenga miundombinu katika shule ya msingi
Buhangija ya Mkoani Shinyanga.
Akizungumza shuleni hapo Mwalimu
Mkuu wa Shule hiyo Selemani Kipanya amesema mwaka 2018 Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia iliipatia shule hiyo fedha hizo kwa ajili ya
kujenga vyumba vinne vya madarasa, mabweni mawili na matundu 18 ya vyoo.
“Majengo haya yamesaidia sana
kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na vyooni pamoja na
kuboresha mazingira ya kufundushia na kujifunzia,” amesema Mwalimu
Kipanya.
Mwalimu Kipanya amesema shule hiyo
ambayo ni jumuishi ina jumla ya wanafunzi 1,052 ambapo kati yao 230 ni
wenye mahitaji maalum na kwamba wanafunzi hao wenye mahitaji maalum
wanaishi bweni wakati wengine wanasoma kutwa.
Naye Mwalimu Mohamed Makana
ameishukuru serikali kwa kuikumbuka shule hiyo ambayo ilikuwa na
changamoto nyingi za miundombinu pamoja na vifaa vya kujifunzia na
kufundishia hasa kwa upande wa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Mwalimu Makana amesema shule hiyo
imepatiwa vifaa vya kufundishia na kujifunzia vya kutosha kwa ajili ya
watoto wenye mahitaji maalum ikiwemo kofia pamoja na miwani kwa ajili ya
watoto wenye ualbino.
Mwanafunzi Jesca Michael mwenye
ualbino ameishukuru Serikali kwa kuwalinda pamoja na kuboresha mazingira
ya kujifunzia na kufundishia huku akiiomba serikali kuendelea
kuwaangalia kwa ukaribu wanafunzi wenye mahitaji maalum ili nao
waendelee kupata elimu bora.
0 comments:
Post a Comment