*****************************
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania
(TBA), Arch. Daud Kondoro ajitathmini kuhusu utendaji kazi wake huku
akiwasimamisha kazi wakurugenzi watatu wa wakala huo.
“TBA
tunaihitaji lakini watu wake wana shida. Hatuwezi kuwaacha, TBA wasipewe
miradi kwa sababu hawawajibiki na wanadhani kwa kuwa ni taasisi ya
Serikali ndio wataachwa wafanye mambo ya hovyo.”
Waziri Mkuu
amewasimamisha kazi wakurugenzi hao leo (Jumatatu, Novemba 18, 2019)
wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) eneo la Njedengwa jijini Dodoma.
Wakurugenzi
waliosimamishwa kazi ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya
Ujenzi, Arch.Humphrey Killo, Kaimu Meneja wa Miradi, Abdallah Awadh na
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ushauri Arch. Hamis Kileo.
Waziri Mkuu
amechukua hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na utendaji kazi wa TBA
katika miradi mbalimbali waliyopewa na Serikali ukiwemo ujenzi wa jengo
la NEC ambalo ujenzi wake ulianza Julai, 2017 na ulitakiwa ukamilike
Juni 2018 kwa gharama ya sh. bilioni 13. Hata hivyo mradi huo bado
haujakamilika na ujenzi wake umesimama.
Akiwa katika
eneo la mradi wa ujenzi wa ofisi ya NEC Waziri Mkuu alihoji sababu za
mradi huo kutokamilika kwa wakati ambapo Kaimu Mkurugenzi wa Ujenzi
alisema jengo hilo limeshindwa kukamilika kwa sababu wakati walipokuwa
wanaanza kazi walibaini kuwa kuna vitu vilisahaulika wakati wa uandaaji
wa Bill of Quantities(BOQ). TBA ndio waandaaji wa ramani ya jengo hilo na ndio wajenzi.
“Bajeti ya
awali ilikuwa sh. bilioni 10 wakati wa uandaaji wa michoro ya ujenzi
gharama ziliongezeka na kufikia sh. bilioni 13 ambazo ndizo
tulikubaliana katika mkataba. Wakati tunaendelea na kazi tuligundua kuna
vitu vimesahaulika kwenye BOQ jambo lililoongeza bajeti ya ujenzi na
kufikia sh. bilioni 32.” Amesema Arch. Killo.
Waziri Mkuu
akahoji tena “kutoka sh. bilioni 13 hadi kufikia sh. bilioni 32 je
unaona inakuja vizuri hiyo” sh. bilioni 10 hadi sh. bilioni 13 tena hadi
sh. bilioni 32 inazungumzikaje hii na je mwenye jengo mlikubaliana
naye? Awali mwenye mahitaji alisema ana sh. bilioni 10 sasa imefikaje 32
je mlimshauri muhusika kuhusu ongezeko hili?
Kaimu
Mkurugenzi wa Ujenzi Arch. Killo alipotakiwa kueleza sababu za
kuongezeka kwa gharama za ujenzi huo amesema waligundua tofauti wakati
wakiwa kwenye eneo la ujenzi kwamba kuna kazi zilitakiwa zifanyike
lakini katika mkataba hazipo na hawakuwasiliana na muhusika.
Miongoni mwa
vitu vilivyosahaulika katika BOQ ya mradi huo ni pamoja na kutokuwepo
kwa ghorofa ya nne katika jengo moja wanalolijenga katika mradi huo
ambalo ni la ghorofa nane, pia hapakuwa na paa la jengo la kuhifadhia
vifaa mbalimbali vya NEC.
Waziri Mkuu
amesema miradi mingi inayojengwa na TBA katika maeneo mbalimbali
imeshindwa kukamilika kwa wakati, hivyo amemwagiza Waziri wa NchiOfisi
ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista
Mhagama asitishe mkataba huo wa ujenzi na atafutwe mkandarasi mwingine
aje amalizie.
“Jengo la
TAMISEMI lililopo katika mji wa Serikali limejengwa kwa gharama ya sh.
bilioni 1.7, nyie wataalamu gani na kwa nini tuendelee kuwaacha ndani ya
taasisi? TBA hamfanyi kazi vizuri wakuu wa mikoa na wilaya wanalalamika
majengo hayakamiliki ni Serikali gani itakayowavumilia, mmeshindwa
kutambua majukumu yenu.”
Waziri Mkuu
ameagiza mkandarasi atakayepatikana ahakikishe mradi wa ujenzi huo
unakamilika katika kipindi cha miezi sita kuanzia sasa na lijengwe kwa
kutumia mfumo wa force account.
0 comments:
Post a Comment