METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, November 18, 2019

Shida ya Udumavu Rukwa Inaanzia kwenye Fikra Hizi – Meya wa Sumbawanga


Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Mh. Justin Malisawa (kaunda suti ya bluu) akifurahi pamoja na washiriki wa kongamao la wanawake wajasiliamali kuwezeshwa kiuchumi katika ukumbi wa Manispaa ya Sumbawanga.
Baadhi ya Wanawake wajasiliamali waliohudhuria katika kongamano lililolenga kutoa mafunzo ya kurasimisha shughuli zao paoja na kutambua fursa mbalimbali za kujipatia kipato zilizopo katika maeneo yanayowazunguka katika mji wa Sumbawanga.
Mstahiki Meya wa Manispaa  ya Sumbawanga Mh. Justin Malisawa
 
…………………..

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Sumbwanga Mh. Justin Malisawa amewataka wanawake mkoani Rukwa kuachana na dhana kuwa familia zinazopendelea kula mboga za majani ni masikini  na hivyo kupelekea kinamama wengi kushindwa kula mboga za majani kuhofia kuitwa masikini jambo linalopelekea udumavu kuendelea kuwepo kaika mkoa wa Rukwa.


Amesema kuwa udumavu unatokana na wananchi wa Mkoa wa Rukwa kula mlo wa aina moja pamoja na kuwa ni miongoni mwa mikoa mitano inayoongoza kwa uzalishaji nchini na kusisitiza kuwa mboga za majani ni muhimu kwa wanawake hasa wajawazito kwani huwasaidia kuwajenga na kumjenga kiumbe aliyemo tumboni mwake kukua kiafya na kiakili. 


“Na bahati mbaya tumejijengea utaratibu kwamba familia ambayo inayokula mboga za majani kwa wingi ni familia masikini, huo ndio ukweli ukimkuta mama Fulani kakarangiza mboga za majani, kesho mboga za majani, keshokutwa mboga za majani, majirani watamwita masikini wa kutupwa,” Alisema.


Mstahiki Meya ameyasema hayo kwenye kongamano la wanawake wajasiriamali lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa manispaa ya Sumbawanga, kongamano ambalo lilihudhuriwa na viongozi na wawakilishi wa taasisi mbalimbali ikiwemo mabenki, bima ya afya, SIDO, TRA, TBS na watumishi wa idara ya maendeleo ya jamii kutoka ofisi ya mkurugenzi wa manispaa.


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga  George Lupilya amesema kuwa Manispaa Sumbawanga kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii  imejipanga kuhakikisha inatekeleza maagizo na Sera mbalimbali  za nchi ili kuhakikisha Mwananchi anafikiwa kwa huduma za Kijamii na kujikwamua Kiuchumi.


Aidha, Kaimu huyo ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Kilimo amewaasa kinamama hao kuhakikisha wanajishughulisha na kilimo cha bustani za mboga mboga kwa kulima walau tuta moja ama mawili ili kuweza kupambana na udumavu pamoja na utapiamlo katika mkoa.


Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya jamii Manispaa ya Sumbawanga Frank Mateni amesema kuwa dhumuni la kufanya kongamano hilo ni kuamsha ari, kuwajengea uwezo wanawake wajasiliamali kuona ni fursa gani ambazo wanazo katika mazingira yao wanayoishi wanayoweza kuyatumia kujiongezea kipato.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na wanawake wajasilimali zaidi ya 570 wakiongozwa na viongozi wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Mkoa wa Rukwa.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com