Madiwani
Mkoani Singida wametakiwa kulima mazao ya biashara kama vile Pamba na Korosho
ambapo mazao hayo ni ya kipaumbele Mkoani hapa, ili kuonyesha faida za kilimo hicho
kwa wananchi.
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amewaeleza hayo madiwani mapema leo
katika mkutano wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (Alat)-Mkoa, tawi la
Singida uliofanyika katika ofisi za halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.
Dkt
Nchimbi amesema madiwani wanapo hamasisha kilimo cha korosho na pamba kwa
vitendo hasa kwa wao kuwa na mashamba yanayoonyesha zao hilo linastawi vizuri,
wananchi wengi watahamasika na kujifunza kutoka kwao.
Ameongeza
kuwa mkutano huo ulenge hasa katika kuangalia namna bora ya kumtumikia
mwananchi na kuangalia njia mbalimbali za kumuokoa katika umaskini ili katika
kuelekea Tanzania ya Uchumi wa kati na viwanda, asiwe mtazamaji bali mshiriki
mkuu.
Dkt
Nchimbi amesisitiza kuwa mkutano huo utumike pia kubainisha rasilimali zilizopo
Mkoani Singida pamoja na fursa ambazo zinaweza kupatikana kutokana na uwepo wa rasilimali
hizo.
“Singida
tunazalisha ngozi na kuiuza ikiwa ghafi hivyo faida inakuwa ndogo, tumieni
mkutano huu kuangalia uwezekano wa kuanzishwa kwa kiwanda kikubwa cha ngozi, ili
tuanze sasa kuuza bidhaa za ngozi pamoja na kununua ngozi kutoka mikoa mingine
nchini”, ameeleza Dkt Nchimbi.
Ameongeza
kuwa ili kuboresha utendaji unaolenga kumsaidia mwananchi, maafisa utumishi
wanapaswa kuwasimamia watumishi ili waweze kufanya kazi kwa bidii na uadilifu
huku akiwataka wawapende watumishi wao.
Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (Alat)-Mkoa, tawi la Singida James
Mkwega amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa nasaha zake na kumuahidi kuwa mkutano huo utaweka
malengo ya kuendeleza mkoa.
Wakati huo huo, Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amewaomba wananchi wa Singida kumuombea
Mbunge wa Singida Mashariki Mhe. Tundu A. Lissu aliyejeruhiwa kwa risasi
nyumbani kwake Dodoma.
Dkt Nchimbi amesema
Lissu ni mwanasingida mwenzetu hivyo tunatakiwa kumuombea ili arejee katika
afya yake na kuweza kuendelea na majukumu yake ya kuwatumikia wana Singida na
Taifa kwa ujumla.
Aidha ameongeza kuwa
hakuna anayefurahishwa kwa kitendo alichofanyiwa Lissu na kuwataka wanasingida
na taifa kwa ujumla kuendelea kuliombea taifa liendelee kuwa kisiwa cha amani
na utulivu.
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akizungumza na madiwani mapema leo katika mkutano wa Jumuiya
ya Tawala za Mitaa Tanzania (Alat)-Mkoa, tawi la Singida uliofanyika katika
ofisi za halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.
Madiwani
na wajumbe wengine wa mkutano wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (Alat)-Mkoa,
tawi la Singida uliofanyika katika ofisi za halmashauri ya Wilaya ya Mkalama
wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida.
Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (Alat)-Mkoa, tawi la Singida James
Mkwega akizungumza katika mkutano huo mapema leo.
0 comments:
Post a Comment