Na Mwandishi Wetu-Dodoma
Utendaji mzuri katika eneo lolote ni tunu na uwezo wa kuleta mageuzi ya kweli kwenye jamii yoyote ile inayolenga kupiga hatua kufikia maendeleo endelevu yanayotokana na Dira ya Maendeleo iliyowekwa na jamii husika.
Kufikiwa kwa malengo hayo katika nchi yetu kunatokana na uongozi madhubuti na utendaji mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwekeza vyema katika Sekta ya Elimu, Nishati, Maji,Uchukuzi, Mawasiliano na Afya.
Msingi wa Mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka minne yanatokana na aina ya uongozi wa Rais Magufuli wa kuzingatia kuwapo kwa ushahidi wa mahusiano chanya kati ya “Kiongozi na Matokeo” sambamba na ukuaji wa uchumi.
Hivyo Basi, uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika sekta ya elimu umeonesha mafanikio makubwa kupitia Mpango wa Elimu Msingi (Basic Education) bila malipo wenye lengo la kuhakikisha kuwa kila mtoto wa Tanzania mwenye sifa ya kwenda shule anapata haki ya kupata elimu bila kikwazo cha ada na michango mingine.
Katika kukuza sekta hii Chuo Kikuu cha Sokoine kilipatiwa matrekta 10 mapya ili kufundishia wataalamu wa kilimo,katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kulifanyika ujenzi wa mabweni,halikadhalika mikopo kwa wanafunzi wa wa Elimu ya Juu imeongezwa hadi shilingi bilioni 450 kwa mwaka 2019/ 2020 ikilinganishwa na shilingi bilioni 427.5 zilizotengwa mwaka 2018/2019.
Hatua nyingine ni pamoja na ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi unaoendelea katika wilaya nyingi hapa nchini, ujenzi wa madarasa, matundu ya vyoo,maabara na miundombinu mingine ya sekta hii imechangia kukuza kiwango cha elimu.
Katika sekta ya nishati Rais Magufuli amewezesha kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa kufua umeme wa maji katika mto Rufiji unaojulikana kama mradi wa kufua umeme wa Mwalimu Nyerere utakaozalisha megawati 2115, hapa Mhe. Rais amewahi kunukuliwa akisema “Umeme ni Maendeleo, ni kichochea muhimu cha ukuaji wa uchumi kwa taifa lolote,bila ya kuwepo kwa umeme wa uhakika ndoto yetu ya kujenga uchumi wa viwanda haitatimia.”
Sekta ya uchukuzi nayo haikuachwa nyuma kupitia utekelezaji wa miradi ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro umefikia asilimia 70 na kipande cha Morogoro Makutopora unaendelea kwa kasi na umefikia asilimia 20 , mradi huu umetoa ajira kwa watanzania wapatao 6,335 sawa na asilimia 90 ya wafanyakazi wote.
Kukamilika kwa mradi huu kutachangia kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi kuongezeka na hivyo ustawi wa wananchi utaleta tija katika uzalishaji.
Uboreshaji wa miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam mwaka 2018/2019 unaendelea na unalenga kuifanya kuwa ya kisasa na kuwa na gati zenye uwezo wa kuhudumia meli nyingi na kubwa zaidi ya ilivyokuwa awali, kwa sasa gati namba 1 hadi 7 zimeboreshwa na ujenzi wa gati jipya la kuhudumia meli zilizobeba magari umefikia asilimia 65.
Bandari ya Tanga na Mtwara nazo zimeboreshwa na kuongeza uwezo wa kuhudumia meli kubwa na kwa idadi kubwa zaidi, usafiri katika maziwa yote nchini umeimarishwa kwa kujengwa kwa meli mpya na kukarabatiwa kwa zile zilizopo hivyo wananchi wanaotegemea usafiri huo katika ziwa Tanganyika, Victoria na Nyasa wameongeza kasi ya shughuli za kiuchumi.
Baadhi ya Miradi inayoendelea katika sekta ya uchukuzi ni pamoja na ile ya ujenzi wa barabara za juu kwenye makutano ya Ubungo, upanuzi wa barabara ya Kimara Mwisho hadi Kibaha Km 19.2 kutoka njia mbili hadi njia nane, ujenzi wa daraja jipya la Salenda na miundombinu ya mradi wa mabasi yaendayo kasi Awamu ya II na III.
Kufikia mwezi Februari 2019, jumla ya miradi 65 ya maji vijijini ilikamilishwa ambapo wananchi milioni 25.36 waishio katika vijiji hivyo wamenufaika kwa kupata maji safi na salama,hali hiyo inaendana na malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa.
Katika kusimamia rasilimali za nchi Rais Magufuli amewezesha kutungwa kwa sheria kwa ajili ya usimamizi thabiti wa rasilimali ya madini, Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusu Umiliki wa Maliasili Na.5 ya mwaka 2017 na Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi No.6 ya mwaka 2017 pamoja na kufanya marekebisho ya Sheria ya Madini sura ya 123.
Kwa upande wa Sekta ya Kilimo inayoajiri wananchi takribani asilimia 75 hadi 80 ambapo kwa kutambua umuhimu wa sekta hii Rais Magufuli alizindua Programu ya kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II). Programu hii inalenga kuleta mageuzi katika sekta hii kwa maana ya mazao, mifugo na uvuvi ili kuongeza uzalishaji na tija, kufanya kilimo kiwe cha kibiashara na kuongeza pato la wakulima hususan wakulima wadogo kwa ajili ya kuboresha maisha na usalama wa chakula na lishe.
Kwa kuwa Rais Dkt. Magufuli amewezesha ujenzi wa vituo vya afya 352 na hospitali za wilaya 67 na hospitali za kanda zinaendelea kujenga ni wazi kuwa mchango wake katika kuboresha maisha ya wananchi unamfanya kuwa na sifa za kutunukiwa shahada hii. Hakika usemi wa wahenga usemao chanda chema huvikwa pete leo umetimia kwa Mhe. Rais Magufuli kutunukiwa Shahada ya Sayansi ya Udaktari wa Falsafa.
0 comments:
Post a Comment