Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya
Huduma za Meli Bw. Eric Hamissi akimpa maelezo Msemaji Mkuu wa Serikali
Dkt. Hassan Abbasi hatua iliyofikiwa ikiwemo vifaa ambavyo vimeshawasili
nchini mpaka sasa kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya kubwa ya abiria
ambapo Serikali imeweka Kiasi cha Shilingi Bilioni 89 katika mradi huu.
Meneja Mradi wa Chelezo na
Ukarabati wa Meli za MV. Victoria na MV Butiama Mhandisi Abel Gwanafyo
akimpa maelezo Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi (katikati) ya
hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Chelezo ambayo ni sehemu kubwa
itakayokuwa inapaki meli kwa ajili ya matengenezo na marekebisho
mbalimbali, Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli Bw.
Eric Hamissi
Baadhi ya Mafundi wakiendelea na
zoezi la uunganishaji wa vyuma kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya kubwa ya
abiria itakayofanya kazi katika ziwa victoria.
Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.
Hassan Abbasi akiwa katika picha ya pamoja na wakandarasi wanaojenga
meli mpya na wafanyakazi wa Kampuni ya Huduma za Meli alipotembelea eneo
hilo ili kujionea hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa meli hiyo itakayofanya
kazi katika ziwa victoria.
Muonekano wa Meli ya MV. Victoria inayokarabatiwa na Kampuni ya Huduma za Meli.
Muonekano wa Chelezo inayojengwa
na Kampuni ya Huduma za Meli ambayo ni sehemu kubwa itakayokuwa
inapaki meli kwa ajili ya matengenezo na marekebisho mbalimbali ambayo
imefikia asilimia 53 ya ujenzi na itaanza kutumika mwezi Machi 2020
…………………………………………….
Mkurugenzi wa Idara ya Habari –
MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi jana (Oktoba 31)
alitembelea mradi wa ujenzi wa meli ya kisasa ambayo ni meli kubwa
kuliko zote katika Ukanda wa Afrika Mashariki pamoja na ujenzi wa
chelezo kwa ajili ya matengenezo na marekebisho ya meli mbalimbali ikiwa
ni uwekezaji unaofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. John
Pombe Magufuli.
Akiwa katika eneo hilo, Dkt.
Abbasi alisema kuwa ujenzi wa meli mpya ni ahadi iliyodumu kwa zaidi ya
miaka 23 iliyopita, ambayo imetekelezwa katika kipindi cha miaka minne
ya uongozi wa Rais . Dkt Magufuli.
Aidha, Dkt. Abbasi aliongeza kuwa
ujenzi wa meli mpya itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 1, 200
umefikia asilimia 33 ya ujenzi na utakamilika mapema mwaka 2021, ambapo
Serikali imewekeza zaidi ya TZS Bilioni 150, kwenye mradi ya meli
pamoja na ujenzi wa chelezo.
Aidha, Dkt. Abbasi alishuhudia
ukarabati unaoendelea katika meli ya MV. Victoria, ambayo baada ya
kukamilika itasaidia kutoa huduma bora za usafiri kwenye eneo la Ziwa
Victoria.
Vilevile, akiwa ziarani hapo
Dkt. Abbasi alisema kuwa ipo miradi mingi kwenye eneo la Ziwa Victoria
na Ziwa Tanganyika, inatakayo gharimu zaidi ya TZS Bilioni 300.
Aliongeza kuwa hivi karibuni,
Serikali itasaini makubaliano ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa
meli katika eneo la Ziwa Tanganyika na uundaji wa meli 3 mpya na za
kisasa katika eneo la Ziwa Nyasa.
Akitaja, meli zilizokamilika
kutokana na utekelezaji wa ahadi za Serikali hadi sasa kuwa ni meli za
mbili za mizigo za MV. Ruvuma, na meli kubwa ya kisasa ya abiria ya MV.
Mbeya II na ambayo tayari imeanza kazi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa
Kampuni ya Huduma za Meli, Eric Hamissi, alisema kuwa ujenzi wa meli
hiyo mpya unaendelea vizuri, na Septemba 30, mwaka huu vifaa mbalimbali
kwa ajili ya ujenzi wa vilianza kuletwa na sasa kazi ya uunganishwaji wa
vyuma imeshaanza.
Aliongeza kuwa, ujenzi wa chelezo
umefikia 53%, na ifikapo Machi mwakani chelezo itanza kutumika kwa
ajili ya ujenzi wa meli mpya.
Aidha, Bw. Hamissi alisema
anaishukuru Serikali kwa ujenzi miradi hii miwili pamoja na ya
ukarabariti wa MV. Butiama na MV. Victoria inayoendelea kwani
itaigharimu Serikali TZS Bilioni 150, na hadi sasa Serikali imeshatoa
TZS Bilioni 70.8, sawa na 47% ya miradi yote minne.
Bw. Hamissi, aliongeza kuwa
miradi hii imesaidia kukuza uchumi wa Mwanza kwa kutoa ajira zaidi ya
watu 1,000 pamoja utumiaji wa malighafi na watoa huduma, hali
inayosaidia kuboresha maisha ya wananchi.
Alifafanua kuwa, huu ni
uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ambao haujawahi kutokea tangu
Uhuru na ni mapinduzi katika usafiri wa njia ya maji kwa kutekeleza
miradi mikubwa minne kwa wakati mmoja, na kuwa awali meli nyingi
zilijengwa kwa msaada mfano MV. Sangara.
Naye, Li Yonjee, Mtaalamu wa Meli
kutoka Korea Kusini, alisema anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa
kuwapa fursa ya kushiriki katika uundaji wa meli mpya ya kisasa,
watatumia ujuzi wao wa uundaji wa meli waliofanya katika nchi za Korea
ya Kusini, China na Japan, zikiwa ndio nchi kubwa za uundaji wa meli
duniani, katika kuunda meli mpya ya Tanzania.
Vilevile, Bw. Li alisema kuwa
wanaahidi kutimiza matarajio ya Serikali na watanzania kwa ujumla kwa
kuunda meli hiyo kwa mafanikio, pamoja kuikamilisha kwa wakati.
Aidha, Bhoke Siguta mwanamke
anayefanyakazi ya kuchomelea vyuma katika mradi wa uundaji wa meli mpya,
alisema anaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutekeleza miradi
mbalimbali inayogusa maisha ya watanzania, ikiwemo kutoa ajira.
Bi. Siguta alisisitiza kuwa,
kupitia mradi huu wa uundaji wa meli mpya ameweza kupata ajira,
inayompatia kipato cha kumsaidia kutunza familia yake.
Pia, ameshauri wanawake
kujishughulisha na kazi za uchomeleaji vyuma, kwani ni kazi nzuri na
zitawajengea uwezo zaidi wa kujiamini pamoja na kukuza kipato.
Awali, Dkt. Abbasi alikutana na
kufanya mazungumzo na uongozi wa Kampuni ya Huduma za Meli kuhusu
mikakati na maboresho ya kampuni hiyo.
0 comments:
Post a Comment