METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, November 5, 2019

MHE BITEKO AWAHAKIKISHIA WANANCHI MGODI WA ACACIA KULIPWA FIDIA

Waziri wa Madini Mhe Doto Biteko (Mb) akijibu swali bungeni Jijini Dodoma leo tarehe 5 Novemba 2019 wakati wa mkutano wa kumi na saba.

Waziri wa Madini Mhe Doto Biteko (Mb) akijibu swali bungeni Jijini Dodoma leo tarehe 5 Novemba 2019 wakati wa mkutano wa kumi na saba.

Serikali kupitia wizara ya Madini imehakikishia wananchi mkoani Mra kuwa itawalipa fidia wananchi wote waliohakikiwa kwa ajili ya kupisha mgodi

Waziri wa Madini Mhe Doto Biteko ameyasema hayo leo tarehe 5 Novemba 2019 bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum mkoani Mara Mhe Agness Marwa aliyetaka kufahamu ni lini mgodi wa Acacia uliopo Nyamongo utalipa fidia kwa wananchi.

Amesema kuwa Serikali imeendelea kusimamia Sekta ya Madini kwa kuhakikisha Uwekezaji unafanyika kwa mujibu wa Sheria na Taratibu za Nchi ikiwemo kuhakikisha kuwa wananchi wanaoishi katika maeneo ambayo miradi ya uendelezaji migodi inataka kufanyika na kulazimika kupisha maeneo yao, wanalipwa fidia stahiki kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi na wanapewa makazi mbadala ambayo yana hali bora kuliko makazi waliyokuwa nayo awali.

Mhe Biteko aliongeza kuwa Uthaminishaji katika  maeneo yanayozunguka mgodi wa  North Mara na ulipaji wa fidia umegawanyika katika awamu nyingi kwa kuzingatia vijiji husika kuridhia. Kijiji cha Nyabirama chenye wakazi 1,974 waliothaminiwa katika awamu ya 20, 35 na 42 wote walilipwa fedha zao isipokuwa wakazi 64 ambao fidia yao iliyoidhinishwa ya shilingi bilioni 1.9 waliikataa na hundi zao zilibaki Ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya ya Tarime. Eneo la Kijiji cha  Nyabichune lilithaminiwa katika awamu ya 47 na kuidhinishwa shilingi millioni 224 kwa ajili ya  watu 69. Wizara iliagiza uthamini wa maeneo ya kijiji cha Nyabichune urudiwe kwa sababu wananchi walipunjwa.

Amesema, Mthamini Mkuu wa Serikali ameshakamilisha uthaminishaji kwenye  maeneo 1,838 ambapo tayari ameshawasilisha kwenye menejimenti ya  mgodi kwa hatua zake za ulipaji.

Aidha, Kuhusiana na suala la mgodi kubadilisha aina ya uchimbaji toka uchimbaji wa wazi (open pit) kwenda underground mining, uamuzi huo ulifikiwa baada ya mgodi kufanya utafiti ulioonesha kuwa gharama ya uchimbaji wa chini (underground mining) ilikuwa ni ndogo ukilinganisha na gharama za kuendelea na mgodi wa wazi.

Mhe Biteko amewatoa shaka wananci wa Tarime kuwa Wizara inafuatilia kwa karibu uchimbaji unaofanyika na mpaka sasa uchimbaji wa underground unafanyika eneo la Gokona kuelekea Nyabigena ndani ya maeneo waliyokuwa wakichimba tangu awali. Hivyo, hakuna eneo ambalo mgodi wa underground unachimba kwenye makazi ya watu.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com