METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, November 6, 2019

MHE BASHE ABAINISHA MKAKATI WA UPATIKANAJI WA MBEGU BORA YA VIUNGO VYA VYAKULA


Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Hussein Bashe (Mb) akijibu swali bungeni Jijini Dodoma leo tarehe 6 Novemba 2019 wakati wa mkutano wa kumi na saba

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Serikali inatambua umuhimu wa kuwekeza katika mazao mbalimbali ya kilimo yakiwemo mazao ya viungo ambayo mahitaji yake yanaendelea kuongezeka ndani na nje ya nchi.

Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imeanza kufanya utafiti wa kupata mbegu bora za mazao ya viungo na mazao mengine ya bustani (Horticulture) ili kuongeza uzalishaji na tija.

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Hussein Bashe ameyasema hayo leo tarehe 6 Novemba 2019 bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa jimbo la Mkinga Mhe Dunstan Luka Kitandula aliyetaka kufahamu kama Serikali ipo tayari kuwawezesha wakulima hao kupata mbegu bora ili waweze kuongeza uzalishaji wa mazao yao.

Amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inapitia Sera ya Kilimo ya Mwaka 2013 ambapo sekta ndogo ya mazao ya bustani (horticulture) ni miongoni mwa maeneo muhimu yanayozingatiwa. Vilievile, kutokana na umuhimu wa mazao ya horticulture, Serikali kupia Wizara ya Kilimo itafanya kikao cha wadau wa mazao hayo tarehe 8 Novemba, 2019 ili kuandaa Mkakati wa Miaka Mitano wa Kuendeleza Mazao ya Bustani. 

Mkakati huo unalenga kuongeza uzalishaji, ubora wa mazao, kuimarisha mifumo ya masoko ya mazao hayo. Aidha mkakati huo utakuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa unaolenga Taifa letu kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.

Aidha, pamoja na hatua hizo, Mhe Bashe ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutoa elimu ya kilimo bora cha mazao ya viungo, uhifadhi, usindikaji na masoko kwa kushirikiana na Sekta Binafsi kikiwemo Chama cha Wadau wa Mazao ya Viungo Tanzania (Tanzania Spices Association – TASPA), Sustainable Agriculture Tanzania (SAT) na vyama vingine vya wakulima. 

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com