METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, November 6, 2019

SERIKALI YAJA NA JITIHADA ZA KUONGEZA WAWEKEZAJI KWENYE ZAO LA NAZI – MHE MGUMBA


Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akijibu swali bungeni Jijini Dodoma leo tarehe 6 Novemba 2019 wakati wa mkutano wa kumi na saba

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inafanya jitihada za kuongeza wawekezaji katika zao la nazi kwa lengo la kumpatia mkulima soko la uhakika na bei nzuri.

Jitihada hizo ni pamoja na kutoa elimu katika mnyororo wa thamani wa zao la nazi ikiwa ni pamoja na kuwapatia wakulima mashine za kukamua mafuta ya nazi.

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba ameyasema hayo leo tarehe 6 Novemba 2019 bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa Jimbo la Mafia Mhe Mbaraka Kitwana Dau ambapo ameongeza kuwa hadi kufikia tarehe 30 Septemba 2019 Vikundi vya Wajasiriamali vya Tujitegemee na Kaza Moyo vimepatiwa mashine zenye uwezo wa kukamua mafuta ya nazi lita 400 kwa siku ambapo lita moja huuzwa kati ya Shilingi 8,000 hadi Shilingi 10,000.

Aidha, Serikali inaendelea kutafuta masoko ya mazao yote ya kilimo likiwemo zao la nazi kwa kuwaunganisha wakulima na wanunuzi kupitia vikundi na vyama vya ushirika. 

Vilevile, Serikali inaendelea kuweka miundombinu ya usafiri kwa kuunda kivuko kitakachowezesha kuunganishwa kwa usafiri kutoka Mafia hadi Nyamisati Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti na hivyo kuwezesha wakulima wa Mafia kusafiri na mizigo yao ya nazi kwenda Dar es Salaam ambako watauza kwa bei nzuri katika masoko makubwa. 

Mhe Mgumba alibainisha kuwa sababu za kushuka kwa bei ya zao la nazi ni pamoja na; uwepo wa wanunuzi wachache wa nazi na hivyo kutokuwepo kwa bei ya ushindani ikilinganishwa na misimu iliyopita; kupanda kwa gharama za usafirishaji wa nazi kutoka Shilingi 2,800 miaka mitatu iliyopita na kufikia Shilingi 5,500 kwa gunia lenye nazi 200 mwaka 2019; kupungua kwa wanunuzi wakubwa wa viwanda vya mafuta na bidhaa za nazi.

Zingine ni kuongezeka kwa matumizi ya bidhaa mbadala za nazi kama vile mafuta ya kula ya mawese toka nje, na matumizi ya mafuta ya kupaka yasiyotokana na nazi; kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola na kushuka kwa mfumuko wa bei toka asilimia 11 kwa mwaka 2006 mpaka asilimia 4 mwaka 2018/2019; na kushuka kwa uzalishaji wa nazi nchini kutokana na magonjwa na mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo hayawavutii wawekezaji wa ndani na wa nje kwa sekta ya viwanda vya kuchakata nazi kutokana na hofu ya kukosa malighafi.

Mgumba ameongeza kuwa Wastani wa Uzalishaji wa nazi nchini Tanzania katika msimu wa 2018/2019 ulikuwa tani 530,000. Kutokana na uzalishaji huo, Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza barani Afrika kwa uzalishaji wa nazi tukifuatiwa na Ghana iliyozalisha wastani wa tani 366,183.

Serikali kwa kushirikiana na Sekta binafsi imeanzisha shamba lenye ukubwa wa hekta 54 katika kituo kidogo cha utafiti wa nazi cha Chambezi kilichopo Wilayani Bagamoyo. Shamba hilo litatumika kuzalisha miche bora ya minazi yenye ukinzani dhidi ya ugonjwa wa kunyong’onyea kwa minazi (Coconut Lethal Disease) na kuisambaza kwa wakulima kwa gharama nafuu.

Aidha, Serikali inahamasisha kilimo cha minazi katika maeneo mapya ili kuongeza uzalishaji wa nazi nchini ambapo msimu wa 2018/2019 ilizalisha jumla ya mbegu 11,000 na kusambazwa kwa wakulima katika mikoa ya Rukwa na Mwanza.

Ili kuhakikisha kuwa upatikanaji wa mbegu bora za zao la nazi nchini, Serikali inafanya mazungumzo na Jumuiya ya Asia - Pasific Coconut Community (APCC) ambayo hutunza “germplasm” ya minazi ili kuwezesha upatikanaji wa mbegu bora za minazi yenye kuongeza tija ili kukuza pato la wakulima.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com