METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, November 19, 2019

Mfumo wa TANePS Kuleta Tija na Ufanisi Katika Sekta ya Ununuzi ya Umma


Na Jovina Bujulu, MAELEZO, Dar es Salaam 

Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli imeendelea kujidhihirisha jinsi inavyofanya kazi kwa ufanisi na weledi kwa kuhakikisha inatekeleza mipango yake kwa kasi inavyotakiwa.  


Hatua hiyo inapelekea utendaji wa kazi za Serikali kuwa bora na zenye tija kwa wananchi siku hadi siku na zenye nia ya kuleta mabadiliko katika utekelezwaji wa miradi mbalimbali ambayo hutumia pesa nyingi za umma inayoendana na thamani ya pesa.


Kwa kuzingatia kuwa fedha zitumikazo katika utekelezaji wa miradi ya Serikali kwa kiasi kikubwa hutumika kupitia mfumo wa ununuzi wa umma. Ili kuleta tija kwa taifa, Serikali imeamua kuimarisha eneo hilo kwa kuanzisha Mfumo wa Ununuzi kwa njia ya Kielektroniki (TANePS) ambao unasimamiwa na Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) chini ya Wizara ya Fedha na Mipango.


Ili uwe endelevu, mfumo umetayarishwa kwa mujibu wa Sheria ya Ununuziwa Umma ya Mwaka 2011na Kanuni za Ununuzi wa Umma chini ya Tangazo la Serikali Na. 446 la Mwaka 2013. Sehemu ya XI ya Kanuni hizo inabainisha utaratibu wa mfumo wa manunuzi kwa njia ya mtandao kwa mujibu wa Kanuni ya 343,mambo yatakayotekelezwa kwa mfumo ni pamoja na usajili wa watumiaji, mchakato wa zabuni, ununuzi wa bidhaa, mnada wa mtandaoni, malipo ya ada mbalimbali pamoja na usimamizi wa mikataba mbalimbali.


Akizungumza mfumo huo hivi karibuni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James alisema kuwa mfumo umeanzishwa ili kuiwezesha Serikali kupata thamani halisi ya fedha zinazotumika kupitia ununuzi wa bidhaa, huduma na kazi za ujenzi. 


Mfumo wa ununuzi umeanza kutumika tayari kuanzia mwezi Machi 2018 kwa mujibu wa Kanuni ya 342(1) ambapo baadhi ya taasisi za umma zimeunganishwa baada ya kukamilisha taratibu muhimu ikiwemo mafunzo kwa watumiaji wa mfumo huo na mfumo huo upo wazi kwa wafanyabiashara kujisajili.


Akielezea baadhi ya faida za mfumo huo, Katibu Mkuu James alisema kuwa ni pamoja na kurahisisha ushiriki wa wazabuni kwenye michakato ya ununuzi na hivyo kuongeza ushindani na ufanisi na kupunguza muda unaotumika katika mchakato wa zabuni.


“Mfumo huu utaongeza uwazi na kupunguza vitendo vya rushwa ikiwa ni pamoja na kuongeza kiwango cha uwajibikaji kutokana na urahisi wa uhakiki wa michakato ya zabuni inayoendeshwa, kupunguza gharama za ununuzi kutokana na uokoaji wa muda,  pamoja na kupunguza muda wa kuandaa vikao na tathmini yake pamoja na kuimarika kwa utunzaji wa kumbukumbu za ununuzi.” alisisitiza Katibu Mkuu James.


Inakadiriwa kwamba kuanzishwa kwa mfumo huu kutaokoa wastani wa shilingi bilioni 34 katika miaka mitano ya kwanza, hali ambayo itaipunguzia Serikali mzigo mkubwa uliokuwa unatokana na matumizi yasiyo na tija ambayo yalikuwa kwenye mfumo wa kawaida.


Kwa kuzingatia manufaa ya mfumo huo, Serikali imeagiza PPRA kuhakikisha kuwa ifikapo tarehe 31, Desemba, mwaka huu ihakikishe kwamba taasisi zote za nunuzi nchini ziwe zimeungwa katika mfumo huo.


“ Natoa wito kwa wazabuni, taasisi binafsi na za umma  na wananchi kwa ujumla kuungana na Serikali kwa kutoa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha azma ya Serikali  ya kuwa na mfumo wenye tija kwa taifa” alisema James.


Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), Mhandisi Leonard Kapongo alisema baada ya kupatiwa maelekezo hayo Mamlaka ilianza kutoa  mafunzo kuhusiana na matumizi ya mfumo wa TANePS kwa maafisa wa ununuzi na TEHAMA wa taasisi za Umma. 


“Mpaka sasa Mamlaka imefanikiwa kuunganisha taasisi 418, huku  wataalamu waliopatiwa mafunzo kutoka taasisi nunuzi ikifikia 1,600 ambapo mara baada ya kupatiwa mafunzo taasisi zao huunganishwa kwenye mfumo na kuendelea kutekeleza michakato yote ya ununuzi inayofuata” alisema Mhandisi Kapongo.


Mhandisi Kapongo alitoa rai kwa wakuu wa taasisi kuhakikisha kwamba wanatumia mfumo huo kwani ni takwa la Sheria ya Ununuzi na Kanuni zake, na kwamba PPRA watafuatilia kwa karibu kuhakikisha matumizi sahihi ya mfumo huo.


Watoa huduma mbalimbali, wazabuni na makandarasi wameshauriwa kuchangamkia fursa ya kushiriki kwenye michakato ya zabuni kwa kujisajili TANePS kupitia tovuti ya mfumo ambayo ni, www.taneps.go.tz ambapo watapata maelekezo mbalimbali ya namna ya kujisajili.


Akizungumzia faida ya mfumo huo kwa wazabuni, Mhandisi Kapongo alisema kuwa ni mfumo uliorahisishwa sana kwa vile hawatahitaji tena kutumia makabrasha au kusafiri kwa ajili ya kuwasilisha zabuni zao. 


“Mambo yote hayo yatafanyika kwa njia ya mtandao, yakihusisha kutangazwa kwa mipango ya ununuzi ya mwaka, matangazo mahsusi ya zabuni na Wazabuni waliosajiliwa kuweza kupakua nyaraka za zabuni na kuziwasilisha kwa taasisi nunuzi kwa njia ya mtandao na majibu ya washindi wa zabuni yatatangazwa kwenye mtandao wa mfumo” alisema Mhandisi Kapongo.


Naye Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Balozi Dkt, Marten Lumbanga ameunga mkono mfumo huo na kuongeza kuwa utarahisisha kazi na kuweka uwazi kwa mapato ya Serikali yanayoingia kupitia ununuzi kwa taasisi za umma. 

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com