Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge , Ajira na Wenye
Ulemavu, Jenista Mhagama baada ya futari aliyowaadalia watumishi wa
Ofisi ya Waziri Mkuu, kwenye makazi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini
Dodoma, Mei 28, 2019. Kulia ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Waziri
Mkuu na Bunge), Bibi Maimuna Tarishi na wapili kulia ni Katibu Mkuu,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uwekezaji), Bibi Dorothy Mwaluko.
Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akizungumza
katika futari aliyowaandalia watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwenye
Makazi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma, Mei 28, 2019. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu()
………………….
WAZIRI MKUU ATAKA WATUMISHI OWM WAONGEZE KASI
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka
watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu waongeze kasi ili utendaji kazi
Serikalini uweze kufikia hatua nzuri.
“Ninawashukuru watumishi wote kwa
ushirikiano mnaotupatia mimi pamoja na mawaziri wenzangu, makatibu wakuu
wote watatu, wakurugenzi mbalimbali na wakuu wa vitengo. Tunatakiwa
tuongeze kasi ili tufikie hatua nzuri ya utendaji kazi Serikalini,”
alisema.
Alitoa kauli hiyo jana usiku (Jumanne,
Mei 28, 2019) alipokutana na viongozi na watumishi wa ofisi yake na
kufuturu nao pamoja kwenye makazi yake jijini Dodoma.
Alisema utendaji kazi wa Ofisi ya Waziri
Mkuu ni mgumu kwa sababu unahusika na usimamizi wa shughuli za Serikali
nzima na watendaji wote wa Serikali. “Sekta yetu ni ngumu kwa sababu
sisi ni wasimamizi wa Serikali na watendaji wote wa Serikali. Tuna
wajibu wa kuwaunganisha watendaji wa wizara zote serikalini,” alisema.
“Sisi sote ni watumishi wa umma, kwa hiyo
mchango wenu una maana kubwa na unachangia kwa kiasi kikubwa mafanikio
ya Serikali nzima. Ninawapongeza kwa utumishi mwema na wenye uadilifu,”
alisema Waziri Mkuu.
Akizungumzia kuhusu umuhimu wa kufuturu
pamoja, Waziri Mkuu alisema mwezi wa Ramadhan ni muhimu kwa Waislamu
wote kwa sababu ni kipindi ambacho wanakamilisha nguzo kuu muhimu ya
uislamu.
“Tukio la Ramadhan linatoa ujumbe mzito
kwetu, ni wakati ambao tunatubu kwa maovu tuliyoyatenda. Wakati huu,
inasisitizwa tuweze kushikamana, tujenge tabia ya umoja na pia tuweze
kuvumiliana,” alisisitiza.
Mapema, akimkaribisha
Waziri Mkuu kuzungumza na watumishi hao, Waziri wa Nchi (OWM-SBAU), Bi.
Jenista Mhagama alisema uamuzi wake wa kuwaalika watumishi na kufuturu
nao ni dalili njema kuwa anathamini kazi zinazofanywa na watumishi walio
chini yake.
“Ni viongozi wachache sana wanaowakumbuka
watumishi walio chini yao. Tunakushukuru kwa kututhamini na tunaahidi
kukupa ushirikiano wa dhati unaoenda sambamba na utendaji kazi
uliotukuka,” alisema.
Akitoa shukrani kwa mwaliko huo, Katibu
Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Waziri Mkuu na
Bunge, Bibi Maimuna Tarishi alisema anatoa shukrani kwa niaba ya
watumishi wote na kuahidi kufanya kazi kwa bidii.
“Tunaahidi kuongeza juhudi zaidi kwenye kazi zetu ili tuweze kuwa watu wa kupigiwa mfano na wengine,” alisema.
0 comments:
Post a Comment