Na Ismail Ngayonga,MAELEZO
DAR ES SALAAM
Maji ni hitaji muhimu sana katika
ukuaji wa uchumi na hii inatokana na ukweli kuwa maendeleo ya kiuchumi
ya nchi yoyote duniani yawe ya viwanda, kilimo na kadhalika yanategemea
maji.
Aidha Maji ni hitaji muhimu sana
katika uhai wa mwanadamu na viumbe wengine na ndio maana maji hayana
mbadala na pia bila maji hakuna uhai na hivyo serikali inaendelea
kutekeleza miradi mikubwa ya maji ili kuimarisha uendeshaji na utoaji wa
huduma ya maji kwa wananchi.
Huduma za maji mijini hutolewa
kupitia Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira kwenye Miji Mikuu ya Mikoa
23 pamoja na Dar es Salaam; Miji Mikuu ya Wilaya 99, Miji Midogo 14; na
miradi 8 ya maji ya Kitaifa ili kufikia malengo yaliyopo ya kuboresha
huduma hiyo katika Miji Mikuu ya Mikoa kutoka asilimia 86 hadi kufikia
asilimia 95 mwaka 2020
Taarifa ya Serikali kupitia Wizara
ya Maji inaonesha kuwa mwaka 2016, Uzalishaji wa majisafi maeneo ya
mijini umeongezeka kutoka lita milioni 385 kwa siku mwezi Aprili 2015
hadi kufikia lita milioni 470 kwa siku mwezi Machi, 2016 sambamba na
ongezeko la idadi ya wateja waliounganishiwa huduma ya maji kuongezeka
kutoka kutoka 362,953 mwezi Aprili, 2015, hadi wateja 405,095 mwezi
Machi, 2016 ambapo wateja 392,942 sawa na asilimia 97 wamefungiwa dira
za maji.
Aidha makusanyo ya maduhuli kwa
mwezi yatokanayo na yatokanayo na mauzo ya maji yameongezeka kutoka Tsh.
Bilioni 7.28 mwezi Aprili, 2015 hadi kufikia Tsh. Bilioni 8.50 mwezi
Machi 2016 sawa na ongezeko la asilimia 17.
Katika kukabiliana na changamoto
mbalimbali zilizojitokeza katika sekta ya maji nchini, Serikali ya Awamu
ya Tano chini ya Uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli, imeendelea
kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Miji Mikuu ya
Mikoa ili kufikia asilimia 95; na Miji Mikuu ya Wilaya, Miji Midogo na
Miradi ya Kitaifa kufikia asilimia 90 ifikapo mwaka 2020.
Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio
ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/2020, Waziri wa Maji,
Prof. Makame Mbarawa anasema katika mwaka 2018/2019, Serikali imeendelea
kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji mijini kwa kujenga,
kukarabati na kupanua miundombinu ya majisafi na majitaka pamoja na
kuzijengea uwezo Mamlaka za Maji Mijini.
Akbainisha baadhi ya Miradi
inayotekelezwa na Serikali katika Miji Mikuu ya Mikoa, Waziri Mbarawa
anasema katika Manispaa ya Kigoma Serikali kwa kushirikiana na na
Serikali ya Ujerumani na Umoja wa Ulaya inatekeleza mradi wa usambazaji
wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa gharama ya Euro milioni
16.32, ambapo hata hivyo mwaka 2018 Serikali imesitisha mkataba na
mkandarasi wa mradi huo kutokana na uwezo mdogo wa mkandarasi.
‘’Hadi kuvunjwa kwa mkataba,
utekelezaji wa mradi ulikuwa umefikia asilimia 87 na mradi ulikuwa
umeanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi, kutokana na hali hiyo, Wizara
imechukua jitihada za kuhakikisha huduma iliyokuwa ikitolewa kwa wakazi
wa Mji wa Kigoma inarejeshwa kwa kuajiri mkandarasi wa kuweka mitambo
ya muda ya kusukuma maji’’ anasema Waziri Mbarawa.
Kuhusu Jiji la Arusha,, Waziri
Mbarawa anasema Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB) inatekeleza mradi wa ujenzi wa miundombinu ya usambazaji
majisafi na uboreshaji wa huduma ya uondoaji wa majitaka katika Jiji la
Arusha kwa gharama ya Dola za Marekani Milioni 233.9.
Anaongeza kuwa Kazi
zinazotekelezwa ni pamoja na uchimbaji wa visima virefu 56, ujenzi wa
matanki 10; ujenzi wa mtambo wa kutibu na kusafisha maji, upanuzi na
ukarabati wa mtandao wa mabomba ya majisafi, upanuzi na ukarabati wa
mtandao wa majitaka, ujenzi wa mabwawa mapya 18 ya majitaka, ujenzi wa
ofisi ya Mamlaka; ununuzi wa vitendea kazi na kutoa mafunzo mbalimbali
kwa watumishi.
Akifafanua zaidi Waziri Mbarawa
anasema hadi mwezi Aprili 2019, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia
30 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2020, ambapo kukamilika kwa mradi huo
kutaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 40 kwa siku za sasa
hadi kufikia lita milioni 200 kwa siku na muda wa upatikanaji wa huduma
ya majisafi utaongezeka kutoka wastani wa saa 12 za sasa kwa siku hadi
saa 24.
Waziri Mbarawa anasema katika
Manispaa ya Lindi, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani na
Umoja wa Ulaya inatekeleza mradi wa majisafi na usafi wa mazingira
katika Manispaa ya Lindi unaogharimu Euro milioni 11.7 ambao ulitarajiwa
kukamilika mwaka 2017 lakini haukukamilika kutokana na uwezo mdogo wa
kiutendaji wa mkandarasi.
Anasema kuwa Serikali ilichukua
hatua ya kuvunja Mkataba na Mkandarasi huyo mwezi Oktoba 2018 ambapo
utekelezaji wa mradi ulikuwa umefikia asilimia 92.3 na unatoa huduma ya
maji kwa wakazi wapatao 81,343 wa Mji wa Lindi, ambapo kazi zilizobaki
ni kufunga mfumo angalizi wa uzalishaji maji, ununuzi wa gari la
uondoaji majitaka na kurekebisha maeneo yenye mapungufu katika mradi
huo.
Aidha Waziri Mbarawa anasema
katika mpango wa muda mfupi wa kuboresha huduma ya maji katika Mji wa
Njombe, Serikali imekamilisha ujenzi wa mradi wa maji wa chemchemi ya
Kibena uliogharimu Tsh. bilioni 1.1, ukihusisha ujenzi wa kidakio cha
maji, ulazaji wa bomba kuu lenye urefu wa kilomita 2.2 na ufungaji wa
pampu mbili za kusukuma maji zenye uwezo wa kuzalisha lita 72,000 kwa
saa.
Kukamilika kwa mradi huo
kumeongeza uzalishaji wa maji kutoka lita 480,000 hadi lita 864,000 kwa
siku na kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji katika Hospitali ya
Kibena, Chuo cha Uuguzi, na Ofisi za Makao Makuu ya Mkoa na hivyo
kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji katika Mji wa Njombe kutoka
asilimia 69 mwaka 2016 hadi asilimia 87 za sasa.
Ili kufanikisha malengo yaliyopo,
ni wajibu wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira katika miji mikuu
ya Mikoa kuimarisha hali ya Uzalishaji wa majisafi pamoja na kupunguza
kiwango cha upotevu wa maji pamoja na kuongeza ufanisi wa utoaji wa
huduma iliyo bora na endelevu kwa wananchi.
0 comments:
Post a Comment