*************************
Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
DAR ES SALAAM
21.12.2019
AFYA bora ni nguzo na raslimali
muhimu katika kuchangia maendeleo ya mtu binafsi, familia na nchi
hususan katika kuleta maisha bora na kupunguza umaskini.
Serikali kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali imeendelea kutoa kipaumbele katika huduma za afya zenye
ubora na zinazowafikia wananchi wote ili kuboresha afya zao kwa
kuzingatia sera na miongozo iliyopo.
Sera ambayo imeendelea kutumika
katika kuelekeza utoaji wa huduma za afya ilipitishwa mwaka 1990, ambapo
tangu ilipopitishwa, yamekuwepo mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi na
kijamii, mabadiliko ya sayansi na technolojia na kuongezeka kwa
magonjwa.
Aidha mabadiliko na maelekezo
mbalimbali yaliyotolewa na Serikali yalitoa changamoto mpya katika
utoaji wa huduma za afya na yamechangia kwa pamoja kuifanya sera
iliyopitishwa mwaka 1990 kutokidhi mahitaji na matarajio ya sasa na ya
miaka ijayo.
Mwaka 1996 marekebisho ya sera
yalipitishwa kwa lengo la kuanzisha mfumo mpya wa utoaji na uendeshaji
wa huduma za afya katika ngazi ya wilaya, na katika marekebisho hayo
ushiriki wa sekta binafsi katika utoaji wa afya ulitambuliwa na kupewa
msukumo na kukasimu usimamizi wa utekelezaji katika mamlaka za Serikali
za Mitaa.
Serikali kupitia Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaratibu Mfuko wa Pamoja wa
Afya ulioanzishwa mwaka 1996 na kufadhiliwa na wadau 7, ambao ni
Denmark, Uswisi (SDC), Ireland, Canada, Benki ya Dunia, UNICEF na Korea
Kusini ili kuleta ufanisi na matokea makubwa katika utekelezaji wa
miradi ya afya nchini.
Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio
ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2017/2018, Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema
kupitia Sekretarieti ya Uratibu wa Mfukomajadiliano mbalimbali kati ya
Serikali na Wadau vimekuwa vikifanywa ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa
ya Serikali jinsi inavyotekeleza kazi zinazogharamiwa na fedha za Wadau.
Anaongeza kuwa wanufaika wa Mfuko
huu ni OR -TAMISEMI, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na
Watoto (Idara kuu ya Afya), Mikoa na Halmashauri zote nchini, ambapo
Fedha hizo hugawiwa kwa fomula kwa kuzingatia makubaliano kati ya
Serikali na Wadau wanaochangia Mfuko.
‘Serikali kupitia Wizara
yake inaendelea na juhudi za kuwaleta pamoja wadau wengine zaidi ili
wachangie katika Mfuko huo ili kuleta ufanisi na matokea makubwa katika
utekelezaji wa miradi ya afya nchini’’ anasema Waziri Ummy.
Waziri Ummy anasema kuwa Asilimia
90 ya fedha zote hupelekwa katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa, asilimia
6 ya fedha hizo hutumika katika Wizara ya Afya kwa ajili ya masuala ya
uratibu, usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa masuala mbalimbali
ya Kisera katika Sekta ya Afya.
Aidha Waziri Ummy anasema kuwa
asilimia 3 ya fedha hizo hupelekekwa katika Mikoa kwa ajili ya
kugharamia ufuatiliaji katika ngazi za Mamlaka za Serikali za Mitaa na
asilimia 1 ya fedha zote hupelekwa Makao Makuu ya OR– TAMISEMI kwa ajili
ya kugharamia ufuatiliaji katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Kwa mujibu wa Waziri Ummy, anasema
hadi robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2016/17, kiasi cha Tsh. Bilioni
88.8 kimepokelewa kupitia Mfuko wa Pamoja wa Afya na kati ya fedha
hizo, Tsh Bilioni 5.6 zilipokelewa na Wizara ya Afya, Tsh. milioni 865.1
zilipokelewa na OR-TAMISEMI, Tsh. Bilioni 2.6 zilipokelewa na Mikoa na
kiasi cha Tsh. Bilioni 79.7 zilipokelewa na Mamlaka za Serikali za
Mitaa.
‘Fedha hizi
hutumika kadiri ya Mkataba wa Makubaliano kati ya Serikali na Wadau wa
Maendeleo, ambapo asilimia 33 ya fedha zinazopelekwa katika Halmashauri
zinatakiwa kutumika kama nyongeza ya fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa
na asilimia 67 ni kwa ajili ya utekelezaji wa afua mbalimbali ambazo
zinalenga kuboresha huduma za afya nchini’’ alisema Waziri Ummy.
Waziri Ummy
anaongeza kuwa pamoja na kuzingatia vigezo vya usawa katika kugawanya
fedha za Mfuko, muelekeo wa Wadau kwa sasa ni kutoa umuhimu kwa ufanisi
katika utekelezaji wa kazi zilizokubaliwa ili kuongeza ufanisi katika
kazi zinazokubaliwa kuviwezesha vituo vya kutolea huduma za afya kupata
fedha kwa wakati na kuweza kufanya maamuzi ya haraka ya kutumia fedha
hizo kulingana na mahitaji ya kituo husika.
Akifafanua zaidi Waziri Ummy anasema Wizara
imeandaa utaratibu wa kuwezesha fedha za Mfuko kutumwa moja kwa moja
kwa vituo vya kutolea huduma za afya ili kuviwezesha vituo kununua dawa,
vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kulingana na mahitaji yao kwa haraka
na Halmashauri zitabaki na jukumu la kusimamia na kufuatilia matumizi ya
fedha hizo.
Mfuko wa Pamoja wa Afya ni Mpango
mahsusi, ulioanzishwa na Serikali kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa
fedha kupitia kamati za usimamizi za kutolea huduma za afya katika Mikoa
na Mamlaka za Serikali za Mitaa, hivyo ni wajibu wa Mamlaka hizo kuwajengea uwezo watoa huduma za afya utekelezaji wa afua mbalimbali ambazo zinalenga kuboresha huduma za afya nchini.
0 comments:
Post a Comment