![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/50328a9f-87bd-4e5e-952c-2c6cdc6a2772-1.jpg)
Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa akikata utepe kuzindua mradi wa mafunzo ya kilimo
kupitia tekinolojia ya kitalu nyumba kwenye viwanja vya Nanenane, Ngongo
mkoani Lindi, Oktoba 10, 2019. Wa pili kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Vijana, Kazi na Wenye Ulemavu,
Jenista Mhagama na kulia ni Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na
Michezo wa Zanzibar, Balozi Ali Karume. Wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa
Lindi, Godfrey Zambi na kushoto ni Tausi Hassan kutoka Shirika la
Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA). (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
********************************
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya tano imeamua kupambana na
ukosefu wa ajira kwa vijana kwa kuanzisha programu za kuongeza na
kurasimisha ujuzi.
“Mwelekeo wa
Serikali hivi sasa ni kuendeleza viwanda na viwanda hivi vinahitaji
malighafi kutokana na mazao. Tumeamua kuongeza malighafi kupitia kilimo,
lengo ni kuwafanya vijana waweze kuajiriwa kwenye sekta hii kubwa ya
uzalishaji,” alisema.
Ametoa kauli
hiyo jana jioni (Alhamisi, Oktoba 10, 2019) wakati akizindua mradi wa
kitaifa wa mafunzo ya ujenzi na kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia
ya kitalunyumba (greenhouse) kwenye viwanja vya maonesho vya Ngongo,
mjini Lindi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya vijana kitaifa
kwa mwaka 2019.
“Nataka
vijana muondokane na dhana ya kwamba kuwa na ajira ni lazima uwe umekaa
mezani na umeshika kalamu. Ajira ni kazi yoyote ya halali inayompatia
mtu kipato iwe ni biashara ndogondogo, mamalishe au bodaboda.”
Akifafanua
kuhusu teknolojia ya kitalunyumba, Waziri Mkuu alisema: “Programu hii
inasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu. Serikali inayoongozwa Mheshimiwa
Rais Dkt. John Pombe Magufuli imeweka msisitizo kwenye kilimo lakini
tunaangalia na aina ya kilimo tulichonacho.”
“Maeneo mengi
nchini hayana mvua za kutosha. Kwa hiyo tumeanzisha kilimo cha
umwagiliaji kwa njia ya matone na siyo kwa kuchimba mifereji.
Kitalunyumba kinahitaji nafasi chini ya robo eka, na humo ndani kuna
matuta manne tu. Kwa kutumia tenki la maji, unatumia maji kidogo sana
kwa kila mche, kwa sbabu yanatoka kwa matone,” alisema.
Alisema mtu
yeyote mwenye eneo la kutosha anaezaa kutumia teknolojia ya kitalunyumba
wakiwemo wafanyakazi ili wapate mazao ya kujiongezea mapato. “Unaweza
kulima mahindi ukala mwaka mzima, unaweza kulima vitunguu au mboga za
majani ukauza na siyo nyanya peke yake, hawa wamepanda nyanya kwa sababu
ni mfano tu,” alisisitiza.
Akitaja faida
zake, Waziri Mkuu alisema mche wa kwenye kitalunyumba unadumu kwa muda
mrefu, haupati magonjwa na unazaa kwa wingi. “Mche mmoja unaweza
kuzalisha kilo 30 na ndani ya kitalunyumba kimoja kuna miche 580.
Nimeambiwa nyanya tisa tu, zinajaa kilo moja. Hii ni fursa ambayo kila
mmoja anaweza kulima akiwa nyumbani kwake,” aliongeza.
Mapema, akimkaribisha
Waziri Mkuu kuzungumza na wananchi waliohudhuria uzinduzi huo, Waziri
wa Nchi OWM – Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye
Ulemavu, Bi. Jenista Mhagama alisema Serikali ilifanya utafiti na
kubaini kwamba asilimia 56 ya nguvukazi nchini ni vijana lakini
wanakabiliwa na changamoto ya kukosa ajira.
“Katika
utafiti mwingine wa Serikali, tulibaini kuwa kundi kubwa la vijana
linaajiri na kuajiriwa lakini pia vijana hawa wanakosa ujuzi
unaotambulika rasmi ndiyo tukaja na mkakati wa Taifa wa uwezeshaji wa
vijana kwa kuboresha mazingira na kuwapa stadi na ujuzi mbalimbali
unaohitajika katika soko la ajira. Stadi na ujuzi huu utawawezesha
kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.”
Alisema mradi wa
kitalunyumba ni mradi wa kiprogramu ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu na
umelenga kuwapa vijana stadi za kilimo ili waweze kujiajiri au kuajiri
wenzao. “Ofisi yako kupitia programu hii inatekeleza mradi wa kilimo cha
kisasa kupitia teknolojia ya kitalu nyumba (greenhose) kwa vijana.”
“Mradi wa
kitalunyumba ni ujuzi kwenye shamba wa kuwasaidia vijana kulima mazao
ambayo yatawasaidia vijana kupata masoko, yatawasaidia wajiajiri ama
kuajiri wenzao na kuongeza pato la Taifa,” alisema.
Alisema
uzinduzi uliofanywa katika viwanja vya Ngongo unawakilisha vitalunyumba
vyote nchini chini ya mradi utakaohusisha vijana 18,000 ambapo kila
Halmashauri ina vijana 100 wanaoshiriki kwenye mradi huo ambao
watanufaika na mafunzo ya kilimo cha kisasa.
Alisema hadi
Septemba 2019, jumla ya vijana 8,700 kutoka katika Halmashauri 83 za
mikoa 12 wamepatiwa mafunzo ya ujenzi na kilimo ndani ya kitalunyumba.
Mikoa hiyo ni Mwanza, Iringa, Ruvuma, Shinyanga, Geita, Mbeya, Lindi,
Dodoma, Kilimanjaro, Manyara, Kagera na Simiyu. Alisema maandalizi ya
kutoa mafunzo kwa vijana kutoka katika Halmashauri 102 zilizobaki za
mikoa 14 yamekamilika, na yataanza kutolewa kabla ya Novemba, 2019.
Alisema Ofisi
ya Waziri Mkuu imetoa zabuni za kuendesha mafunzo hayo kwa kampuni
zinazomilikiwa na vijana wa Kitanzania wenye taaluma za kilimo ambao ni
wahitimu wa elimu ya juu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA).
Kampuni zilizopewa kazi ya kufundisha vijana wenzao ni Sokoine University Graduates Corporation (SUGECO), Royal Agriculture Ltd na Holly Green Agriculture Group Ltd.
0 comments:
Post a Comment