Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akiwahutubia
wananchi wa Nduguti, wilayani Mkalama, kwenye mkutano wa hadhara Oktoba 5.2019.
Wananchi
wa Nduguti, wilayani Mkalama, wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wakati
akihutubia, kwenye mkutano wa hadhara Oktoba
5.2019.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na
Watumishi wa Halmashauri pamoja na Madiwani, katika ukumbi wa Halmashauri ya Mkalama, mkoani Singida. Oktoba 5.2019.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akimhoji
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Godfrey Sanga, kutokana na
matumizi mabaya ya fedha za Umma, Oktoba 5.2019. wakati alipozungumza na Watumishi
wa Halmashauri pamoja na Madiwani, katika ukumbi wa Halmashauri ya Mkalama, mkoani Singida. (Picha
na Ofisi ya Waziri Mkuu).
..............
*Agoma kuweka jiwe la msingi la hospitali ya wilaya hiyo
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemwagiza Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Singida, Bw. Adili Elinipenda
amchunguze Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkalama, Bw. Godfrey Sanga kwa
matumizi mabaya ya fedha za umma.
Baadhi ya tuhuma alizonazo ni
kujilipa posho ya safari Machi mwaka huu bila kusafiri, kuwasainisha
watumishi wa chini yake vocha na kisha kuwapa ‘asante kidogo’ kwa madai
fedha hizo zinaenda mkoani, kujilipa stahiki kabla ya wakati na kuagiza
gari liende gereji kwa matengenezo bila nyaraka zozote.
Ametoa agizo hilo leo jioni
(Jumamosi, Oktoba 5, 2019), wakati akizungumza na madiwani na watumishi
wa Halmashauri hiyo kwenye mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa
Halmshauri hiyo.
“Kuna watumishi wanne
uliwaambia wasaini vocha ya sh. 1,320,000. Hii ni kwa safari iliyopangwa
kati ya tarehe 15 na 24 Septemba, mwaka huu; ukawapa asante ya sh.
30,000 ukidai kuwa zinatakiwa mkoani. RAS ni kweli hela hiyo ililetwa
mkoani?” Alihoji Waziri Mkuu na kujibiwa na Katibu Tawala wa Mkoa, Dkt.
Anjelina Lutambi kwamba hakutoa hayo maagizo.
Alipoulizwa Mweka Hazina wa
Wilaya hiyo, Bw. Peniel Mbula kwamba fedha alilipwa nani, mweka hazina
huyo alijibu kwamba alikuwa Dodoma kikazi. Mhasibu aliyekaimu nafasi
yake, Bi. Lulu Hamadi aliwataja watumishi hao kuwa ni Stella Mawa,
Godfrey Mnubi, Richard Laizer na Method Kafuku.
Waziri Mkuu aliwasimamisha
watumishi hao na kuwauliza walilipwa hiyo posho ili waende wapi lakini
walikosa majibu. Ndipo akawaeleza kwamba walimkabidhi Mkurugenzi na
wakalipwa asante ya sh. 30,000.
Alipoulizwa kuhusu malipo ya
sh. 1,090,000 ambayo yalilipwa Septemba 9, mwaka huu yalikuwa ya nini,
Mkurugenzi huyo alijibu kuwa ni ya stahiki zake za kila mwezi ambapo
kati ya hizo, sh. 600,000/- ni za malipo ya nyumba; sh. 230,000 ni za
umeme na sh. 260,000 ni za simu. Lakini hakuweza kujibu ni kwa nini
amejilipa kabla mwezi haujaisha.
Kuhusu gari la elimu lenye
namba za usajili STK 913 lililopelekwa gereji kupakwa rangi kwa gharama
ya sh. milioni saba, Waziri Mkuu alitaka aoneshe dokezo lililotumika
kupitisha idhini hiyo na malipo hayo lakini akajibiwa kwamba hakuna
utaratibu wa kuandika dokezo pindi magari ya Halmashauri yanapoenda
kufanyiwa matengenezo bali wanapeana taarifa kwa mdomo tu.
“Kamanda wa TAKUKURU leta
maafisa kutoka mkoani waje wafanye ukaguzi wa kila jambo ambalo
limeainishwa. Hatuwezi kuacha Halmashauri iendeshwe kienyeji bila
kufuata taratibu. Mkalama inaonekana chafu kumbe tatizo ni mtu mmoja,
mnasaini vocha halafu mnamsingizia RAS,” alisema.
“Ajenda ya kikao changu nanyi
watumishi wenzangu, nilitaka tuambiane kwamba ni lazima tutunze mali na
fedha za Serikali. Waheshimiwa Madiwani ni lazima msimamie Halmashauri
yenu na mhoji kila senti imetumika vipi. Kama ni jengo nendeni mkakague,
kama ni kisima nendeni mkaangalie,” alisisitiza.
“Pia niwasihi Waheshimiwa Madiwani wenzangu, msikubali kutumika kupitisha matmizi ya fedha ambayo si sahihi,” aliongeza.
Watumishi wa Halmashauri hii
mfanye kazi, muache ubabaishaji sababu Serikali hii iko makini sana.
Msiishi kwa mazoea, kwa sababu wakati siyo wenyewe na tena muache
kutengezeza syndicates,” aliwaonya.
Pia amemuonya Afisa Manunuzi
wa wilaya hiyo, Bw. Dickson Mataramba aache kutumika na kufanya kazi kwa
mazoea kwa kupandisha bei ya sh. elfu 2000 hadi 3,000 kwenye vifaa
wanavyoagiza.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu
amekataa kuweka jiwe la msingi la Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya kwa
sababu lilikataliwa na Kiongozi wa mbio za Mwenge na uchunguzi wake
bado haujakamilika.
“Jiwe la msingi mlilonipangia
kuweka leo kwenye hospitali ya wilaya siweki hadi TAKUKURU wakamilishe
kazi ya uchunguzi kuhusu mikataba iliyotumika. Mkikamilisha uchunguzi
mniite, nitakuja kulizindua likiwa limekamilika,” amesema.
0 comments:
Post a Comment