![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/ONE-1-1024x683.jpg)
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/TWO-1-1024x683.jpg)
Kamishna wa Madini Nchini David
Mulabwa akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Shirikisho la Kimataifa
la Vyama vya Wafanyakazi wa Sekta ya Madini na Viwanda uliofunguliwa leo
katika hotel ya White Sand jijini Dar es Salaam nyuma yake ni Katibu
Mkuu Msaidizi wa Shirikisho hilo kutoka nchini Uswiswi Kemal Ozkan.
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/EIGHT-1-1024x683.jpg)
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/THREE-1-1024x683.jpg)
Washiriki wa Mkutano wa Shirikisho
la Kimataifa la Vyama vya Wafanyakazi wa Sekta ya Madini na Viwanda
wakifuatilia mada wakati wa mkutano huo.
…………………….
Kamishna wa Madini nchini,
Mhandisi David Mulabwa amesema, Serikali ya Tanzania inatambua uwepo na
umuhimu wa wachimbaji wadogo wa madini nchini na hivyo kutekeleza sera
inayotaka sekta hiyo kusimamiwa kikamilifu na kuleta tija.
Ameyasema hayo leo tarehe 08
Oktoba, 2019 alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Kanda wa Shirikisho la
Kimataifa la Wafanyakazi wa Sekta za Madini na Viwanda wenye dhima
inayosema “Kuongeza uelewa kwa wafanyakazi juu ya Dira ya Madini kwa
Afrika” (Deepening workers understanding of the African Mining Vision).
Mkutano huu utafanyika kwa siku
mbili ukijumuisha nchi zilizopo Chini ya Jangwa la Sahara ambapo
Tanzania ni mwenyeji wa mkutano huo unaofanyika katika hoteli ya White Sand jijini Dar es Salaam.
Akijibu swali la mmoja wa wajumbe
wa mkutano huo kutoka nchini Ghana, Mhandisi Mulabwa alisema Serikali
kupitia Wizara ya Madini inatekeleza mipango mbalimbali katika
kuhakikisha sekta ya uchimbaji mdogo wa madini inakua na kuleta tija kwa
jamii na taifa kwa ujumla.
Akizungumzia jitihada hizo,
Mhandisi Mulabwa alisema ni pamoja na kurasimisha sekta ya uchimbaji
mdogo wa madini ili kuiwezesha serikali kuwahudumia wachimbaji hao kwa
ukaribu mkubwa.
Pamoja na kurasimisha shughuli
hizo Mhandisi Mulabwa alisema Serikali inatoa elimu kwa wachimbaji
wadogo katika maeneo ya usalama, mazingira na afya ili kuwawezesha
wachimbaji hao kufanya kazi zao katika mazingira salama na hivyo
kuepusha ajali zisizokuwa za lazima na hivyo kutunza nguvu kazi.
Aliongeza kuwa, Serikali imejenga
vituo vya mfano saba (7) nchi nzima vikiwa na lengo la kuonesha namna
bora ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini ya dhahabu pasipo kutumia
mercury ambayo ina madhara makubwa kwa watumiaji na jamii kwa ujumla.
Pamoja na vituo hivyo, Serikali
inafanya juhudi kubwa ya kuwaunganisha wachimbaji wadogo na taasisi za
kifedha na mabenki ili kuwawezesha kupata mikopo na kuwekeza katika
shughuli za uchimbaji.
Aidha, Mhandisi Mulabwa alisema,
Sheria za kazi zinasimamiwa ipasavyo katika sekta ya madini na kueleza
kuwa endapo mfanyakazi yeyote katika sekta hiyo amepatikana na udhahifu
akiwa kazini taratibu na kisheria zinafuata mkondo wake na endapo
itabainika mtumishi anahitajika kulipwa fidia, atalipwa fidia kwa mujibu
wa sheria.
Mhandisi Mulabwa alitumia fursa
hiyo kuwaalika wadau wote wa madini walioshiriki katika mkutano huo kuja
kuwekeza nchini huku akieleza kuwa fursa na maeneo kwa ajili ya
uwekezaji katika seka ya madini ipo.
Amesema serikali kupitia Tume ya
Madini inaendelea kupokea maombi ya leseni na kutoa leseni kwa wadau
watakaoonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya madini nchini.
“Maeneo ya uwekezaji yametengwa,
na maeneo yamelenga uwekezaji mkubwa na mdogo wa madini, hivyo yeyote
mwenye nia ya kuwekeza anakaribishwa” alisisitiza.
Akihitimisha hotuba yake Mhandisi
Mulabwa, aliwataka wadau hao kuelewa kuwa Tanzania haipo nyuma katika
kusimamia dira ya madini ya Afrika ya kuhakikisha rasilimali madini
inawanufaisha waafrika kwa manufaa ya bara Afrika kwa ujumla
Amewahakikishia wadau wote wenye
nia ya kuwekeza katika sekta ya madini nchini kuwa serikali ya Tanzania
itawapa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha wanapata fursa ya
kuwekeza nchini kwa wakati.
Aidha, amesema serikali ipo tayari
kufanya kazi na Shirikisho hilo ili kuhakikisha malengo ya kuanzisha
shirikisho hilo la kuhakikisha inawasaidia wafanyakazi kuongeza
uzalishaji na kuboresha maisha yao linafikiwa.
Akizungumza baada ya kumaliza
awamu ya kwanza ya mkutano huo Katibu Mkuu msaidizi wa Shirikisho hilo
kutoka nchini Uswiswi Kemal Ozkan alisema anaipongeza Serikali ya
Tanzania kwa kuweka kipaumbele katika kujali maslahi ya watumishi na si
makampuni na kuwawezesha wafanyakazi katika sekta ya madini na mafuta
kufanya kazi katika mazingira mazuri.
“Solidarity forever”
0 comments:
Post a Comment